Wasanii Bongo waingia kwenye rada za DCEA kwa 'kutukuza' dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imewaonya wasanii wanaotumia na wanaohamasisha matumizi ya dawa za kulevya kupitia nyimbo zao huku ikiahidi hatua kali zitachukuliwa dhidi yao, kwani wapo macho saa 24.

"Na wasanii wanahamasisha matumizi ya dawa za kulevya,Vdawa hizo wengine wanahamasisha bangi, lakini tutalifanyia kazi, lakini katika hilo kama kuna wasanii ambao wanadhani badala ya kutunga nyimbo za kuelimisha jamii, wao wanatunga nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya.

"Sheria yetu inasema kwamba hao lazima tuwachukulie hatua za kisheria, kwa sababu hili tunaendelea nalo. Waaambieni Watanzania kuwa, dawa za kulevya zina madhara na wala hazifai kutumiwa na Mtanzania yeyote na mtu yeyote, si Mtanzania tu na mtu yoyote kwa maana ya binadamu;

Hayo yamebainishwa leo Desemba 7, 2022 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Gerald Musabila Kusaya wakati akizungumza na waandishi wa habari.

"Na hilo sasa tuwaambie wasanii, kama kuna msanii ambaye anadhani kupata umaarufu kwa kupitia nyimbo za kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya, hilo hatutamuacha hata mara moja, sheria itachukua mkondo na siku ya siku tutawaita (wanahabari) ili kusudi muone kitu gani ambacho tumekifanya kwa hao wasanii ambao wanataka kupata umaarufu kwa kutumia dawa za kulevya.

"Mbona mashairi yapo ya aina nyingi, unashindwaje kuhamasisha vitu vyote hivyo, si uhamasishe hata kilimo bora basi, au hata biashara kwani lazima uhamasishe matumizi ya bangi na matumizi mengine,kwa hiyo tutakuwa mstari wa mbele, na kuhakikisha hatutaruhusu Mtanzania yoyote afanye uhamasishaji wa dawa za kulevya,"amefafanua Kamishna Jenerali Kusaya huku akionekana kuchukizwa na tabia za namna hiyo.

Siku za karibuni baadhi ya wasanii wamekuwa wakijihusisha kutengeneza nyimbo zenye maudhui ya kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya, jambo ambalo mamlaka inalikemea kwa nguvu zote kwa kuwa, wao ni kioo cha jamii na hawapaswi kuwa sehemu ya kubomoa bali kujenga jamii iliyostaarabika na inayopiga vita dawa za kulevya.

Pia kupitia mkutano huo na waandishi wa habari, Kamishna Jenerali Kusaya amesema operesheni endelevu ambayo inaendelea kila kona ya nchi imefanikiwa kukamata kilo 16.643 za dawa za kulevya.

Kati ya dawa hizo, kilo 15.19 ni heroin, gramu 655.73 ni Cocaine huku gramu 968.67 zikiwa ni za Methamphetamine zilizowahusisha jumla ya watuhumiwa saba ikiwa ni mafanikio ya operesheni iliyoendelea mwishoni mwa mwezi Novemba, mwaka huu.Kwa kina soma hapa

Wakati huo huo, Kamishna Jenerali Kusaya amebainisha kuwa, kutokana na kuimarika kwa udhibti wa dawa za kulevya nchini, wahalifu wa dawa za kulevya wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali ili kufanikisha uhalifu wao.

"Hata hivyo, mamlaka ipo macho na inaendelea kukabiliana na mabadiliko ya mbinu hizo. Tunashirikiana na makampuni ya usafirishaji wa vifurushi, vyombo vyote vya ulinzi na usalama na wadau wengine katika kudhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kukabiliana na mbinu mpya za usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya,"amefafanua Kamishna Jenerali Kusaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news