DCEA yataja majina ya watuhumiwa saba waliodakwa na dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imekamata kilo 16.643 za dawa za kulevya jijini Dar es Salaam.

Kati ya dawa hizo, kilo 15.19 ni heroin, gramu 655.73 ni Cocaine huku gramu 968.67 zikiwa ni za Methamphetamine zilizowahusisha jumla ya watuhumiwa saba ikiwa ni mafanikio ya operesheni iliyoendelea mwishoni mwa mwezi Novemba, mwaka huu.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 7, 2022 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Gerald Musabila Kusaya wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Kamishna Kusaya amesema kuwa, ukamataji wa kilo 15.19 za dawa za kulevya aina ya heroin zilizowahusisha watuhumiwa watatu ni mwendelezo wa operesheni zilizopita.Hawa hapa

"Watuhumiwa hawa ni washirika wa Kambi Zuberi Seif na wenzake waliokamatwa wakiwa na kilo 34.89 za heroin katika operesheni ya mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2022,"amebainisha Kamishna Jenerali Kusaya.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa, ni Suleiman Thabit Ngulangwa mwenye umri wa miaka 36 ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Salasala, Sharifa Seleman Bakari miaka 41 ambaye ni mkazi wa Maji matitu Mbagala na Farid Khamis Said mwenye umri wa miaka 22 mkazi wa Maji matitu Mbagala na wote wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Kamishna Jenerali Kusaya amewataja watuhumiwa wengine wannne ambao walikamatwa na gramu 655.75 za Cocaine na gramu 968.67 za Methamphetamine ambao walikamatwa wakiwa katika harakati za kusafirisha dawa hizo za kulevya kwenda nje ya nchi.Mahakamani tayari

"Watuhumiwa hao wanne ni Hussein Rajab Mtitu mwenye umri wa miaka 28 anayejulikana pia kama Chodri Mohamed ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kibonde maji, Mbagala. Mwingine ni Jaalina Rajab Chuma mwenye umri wa miaka 31 anayejulikana pia kama Jaalina Mohan ambaye ni mjasiriamali na mkazi wa Tandika, mwingine ni Shabani Abdallah Said miaka 36 mkazi wa Kilimahewa huko Tandika, hawa pia ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

"Mwingine ni Irene Dickson Msekula mwenye umri wa miaka 39 ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Ndala mkoani Shinyanga. Watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu za kiupelelezi kukamilika,"amefafanua Kamishna Jenerali Kusaya.Viongozi wa dini waguswa

Kwa nini DCEA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015.

Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news