WAZAZI NA USINGIZI MNONO

NA LUCAS MASUNZU

“Sasa ninawasaidiaje wanangu? Tunaelekea kufunga usajili, lakini ada ya mtihani bado hamjalipa, naomba niwasikilize mmoja baaada ya mwingine mnasemaje? ”. Hayo yalikuwa ni maelezo ya Mkuu wa Shule, Bi Jackline Anselimi, aliongea hivyo mbele ya wanafunzi wake, wakiwa ofisini kwake waliokuwa wakidaiwa ada ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2021 ambayo ilikuwa ni shilingi 50,000.

Wakati huo nilikuwa nimeketi kwenye moja ya kochi lililomo ndani ya ofisi ya mwalimu Jackline kusubiri kuhudumiwa.

“Mimi nimeambiwa na mzazi wangu atanitumia kesho jioni,” alisema hivyo mwanafunzi Leokadia. Mwalimu Jackline alisema wewe wa jioni sina shida na wewe, nawe Amina unasemaje? Mwanafunzi huyu aliamua kumsukumizia mzigo mzazi wake, “Naomba uongee na mzazi wangu atoe jibu mwenyewe.”.

Mwalimu mkuu huyu alikuwa na utamaduni wa kuongea na wazazi wa wanafunzi mara kwa mara alimwambia Amina nitajie namba ya simu ya mzazi wako. 

Wakati huo alikuwa ananyanyua simu yake ya mkononi. Baada ya kuwasiliana naye mzazi huyo alisema pesa zikipatikana tutalipa tu, mwalimu huyu mwema alitaja tarehe ya mwisho ambayo alidhani pesa hiyo mzazi huyu ataipata.

Hatimaye ilikuwa zamu ya mwanafunzi wa mwisho aliyekosa karo, inaonekana mwanafunzi huyo alikuwa anakwepa asifikiwe, lakini mwisho alifikiwa. 

Alipoulizwa kuhusu ada ya mtihani alisema moyoni “Mimi hata sijui ninajibu nini? ” Sura yake ilijieleza hivyo. Wakati huo mwanafunzi huyo alikuwa akilengwalengwa na machozi na baada ya muda machozi hayo yalimdondoka kama matone ya mvua.

Kumbuka nipo kando nashuhudia linalotendeka mara nilijikuta ghafla huruma imenitembelea nikaamua kumuazima hiyo pesa ili alipe ada ya mtihani kwa sababu muda wa kulipia ulikuwa unaelekea ukingoni. Huku mfumo wa usajili hufungwa baada ya kipindi cha usajili kumalizika.

“Mzazi wako atakapokutumia pesa kumbuka kunirejesha pesa yangu.” Nilimwambia kwa lugha ya upole kuogopa kumuongezea simanzi mwanafunzi huyu.

Mwanafunzi huyo alifurahi sana, lakini kidonda cha kukosa karo kilichomwa tena na sindano ya moto na maneno haya, “ Kumbuka sana mzazi wako akikutumia pesa hakikisha kurudisha pesa uliyopewa”. Mwalimu Jackline alliiwekea msisitizo deni msaada hilo.

Binti alisimama alipokuwa ameketi akiinamisha shingo yake katika sketi yake na kujipangusa machozi usoni mwake kuelekea darasani kuendelea na vipindi vilivyokuwa vimesalia. 

Hapo tulibaki wawili tu Mwalimu Jackline na mie mimi, mwalimu huyu aliniambia kuwa watoto wanaotoka familia zenye uwezo mdogo wanapata shida sana, kuna wanafunzi wawili pia walikumbwa na shida hiyo hiyo na walisaidiwa pia kwa hisani yake.

Je? Hoja hiyo ya ilani kwa kila mwanafunzi aliyekosa ada ingefanywa hadi lini na je maeneo yote watakuwapo wahisani kama Mwalimu Jackiline na mimi ?.

Mwalimu Jackline aliniambia kuwa baadhi ya wanafunzi huchukiwa na wanafunzi wenzao kwa tabia mbaya kama vile udokozi, uchoyo na ugomvi lakini si kwa mwanafunzi aliyekuwa wa mwisho kutoka ofisini kwa Mwalimu Jackline. 

Mwanafunzi huyo alikuwa ni mwema sana, mpole, mtiifu na aliyekuwa anaheshimu walimu na watumishi wengine shuleni hapo kama vile wapishi. 

Wanafunzi wenzake aliokuwa anasoma nao walimpenda sana, ikitokea mwanafunzi ana changamoto ya kuongezewa damu binti huyo hakusita kujitoa hadi wanafunzi wenziye wakambatiza jina la dada mzuri, jina ambalo lilifanya jina alilopewa na wazazi wake lisimee kwa urahisi pale shuleni. 

Kwa uaminifu wake, baada ya mwezi mmoja dada mzuri alikumbuka kunipatia pesa yangu baada tu ya kutumiwa na mzazi wake.

Maisha yaliendelea mie nikiendelea kutafuta ugali wangu na wanangu, kuna siku moja sina ile na lile nikiwa nimepumzika zangu nyumbani iliingia namba ngeni kwenye simu yangu. 

Nilipokea simu hiyo, “Unaongea na dada mzuri” Nilijibu ndiyo haujambo? Za siku nyingi? Uko wapi siku hizi? Nilimuuliza maswali mfululizo mithilini ya hakimu mahakamani. 

Aliniambia hajambo ananishukuru kwa kumuazima ada ya mtihani. Vilevile, alinitaarifu kuwa alipata divisheni II na anasoma Chuo Kikuu cha Mt. Augustino-Mwanza

Kabla hatujaagana aliniambia jambo hili,“Sasa hivi washindwe wenyewe, Rais Samia Suluhu Hassan amebeba msalaba wangu, natamani nirudie kidato cha sita, elfu hamsini ya mtihani kidato cha sita imefutwa, sasa hivi kuna usawa hakuna cha mtoto wa tajiri kuwahi kulipa na mtoto wa masikini kuaibika kwa kuchelewa kulipa, tena kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita,sasa hivi ni bure.”

Akiwa anaaendelea kuzungumza kwa sauti iliyojaa utomvu wa furaha aliniambia kuwa, “Mama Rais anapiga jarife lake sawa bini sawia na ana hakika safari yetu ipo mikononi mwa nahodha makini na tutafika salama safari yetu maana karo shuleni ilikuwa ni wimbo kubwa lililokuwa kikwazo kikubwa safarini” Mara simu ikakatika nikitamani kuendelea na mazungumzo hayo.

Simu hiyo ilipokatika nilisema kuwa kwa sasa ni kweli ada kidato cha tano na sita ilifutwa kufuatia maelekezo ya Serikali kama ilivyowasilisha katika bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba alisema kwa hatua hiyo elimu bila ada itakua kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita lengo likiwa ni kupunguza gharama kwa wazazi na walezi wa wanafunzi hao.

Hongera kwa Serikali kuubeba mzigo huo uliokuwa msalaba mzito kwa dada mzuri ambao ulikuwa msalaba wa wazazi na walezi wengi nchini Tanzania.

Sasa wazazi na walezi wengi wanalala kwa amani japokuwa Januari 2023 inapiga hodi wakiwa na usingizi mnono.Tunakuombea dua njema kwa Mungu upate kuwa na afya njema ili uzidi kubeba misalaba mingine ya Watanzania.

theheroluke23@gmail.com
0733346877

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news