Waziri Dkt.Ndumbaro atoa maelekezo Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, asisitiza maadili na uwajibikaji

NA MWANDISHI LRCT

TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania (Law Reforms Commission of Tanzania – LRCT) ni injini ya Sekta ya Sheria nchini ambayo imeundwa na Serikali na kukasimiwa majukumu ya kurekebisha sheria nchini ili kuhakikisha uwepo wa haki na maendeleo ya taifa kwa wananchi ambapo ni vema kutekeleza majukumu kwa kuzingatia maadili, sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza na viongozi wa Wizara na watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watumishi hao kuhusu Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma yanayofanyika Jijini Dar es Saalam.

Hayo yameelezwa na Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria wakati akifungua mkutano wa kikao kazi cha mafunzo baina ya viongozi wa Wizara na watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania yanayofanyika kwa siku tatu kuanzia leo kwenye ukumbi wa Ofisi za Bunge, Dar es Salaam.

Waziri Dkt. Ndumbaro amesema kuwa LRCT ni injini ya kurekebisha sheria nchini hivyo amewataka watumishi kutambua kuwa wamebahatika kupewa jukumu la kufanya kazi kwenye Tume na amewahimiza kuzingatia maadili, sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma kwa vitendo, kwa kujitoa sadaka na kutumikia cheo alichopewa ili kuwapatia wananchi huduma stahiki.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Sheria kwa Umma wa Wizara ya Katiba na Sheria, Griffin Mwakapeje, akichangia mada kuhusu Maadili katika Utumishi wa Umma wakati wa mafunzo ya siku tatu kuhusu Sheria na Taratibu za Utumishi wa Umma yanayotolewa kwa watumishi wa Tume hiyo yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

“Hii ni taasisi ya umma, na siyo ya kwenu binafsi, lazima msimame kwenye sheria, taratibu na kanuni na siyo kutoka nje ya sheria, taratibu na kanuni kwa kuwa sisi wote ni watumishi wa umma na hakuna mwenye hati miliki ni muhimu mfanye kazi kwa kuzingatia uzalendo, tuchape kazi kwa bidii, tuheshimu mamlaka ili kuifanya Tume ing’ae, iendelee kuwa na thamani na kukubalika”, amesisitiza Mhe. Dkt. Ndumbaro.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Marry Makondo akizungumza na viongozi wa Wizara na watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kuhusu Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma yanayofanyika Jijini Dar es Saalam.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Mary Makondo amesema kuwa viongozi na watumishi wa tume watapatiwa mafunzo kuhusu maadili kwa watumishi wa umma, utawala bora na kutokomeza rushwa katika utumishi wa umma.

Amesema,lengo la wizara kutoa mafunzo hayo ni kuhakikisha yanawawezesha kutekeleza majukumu yao kisheria kwa ajili ya haki na maendeleo ya taifa ili kuwa na uwajibikaji kwa kuzingatia maadili ya watumishi wa umma na mafunzo hayo yanatolewa na Ofisi ya Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, TAKUKURU na Sekretariati ya Viongozi ya Maadili ya Umma.
Mwenyeketi wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania, Mhe. Jaji Mstaafu January Msofe, akizungumza wakati akichangia mada katika mafunzo ya siku tatu kuhusu Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma yanayotolewa kwa watumishi wa Tume hiyo yanayofanyika Jijini Dar es Saalam.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Tume, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Januari Msofe amesema kuwa Tume imezingatia maelekezo ya Waziri Dkt. Ndumbaro hususani masuala ya maadili kwa kuwa maadili ni kila kitu, maadili ni popote iwe nyumbani, kazini na mbele ya jamii hivyo pamoja na mafunzo yaliyotolewa leo viongozi na watumishi wametambua kuwa ni muhimu kuendelea kujifunza ili kuweza kutekeleza vema majukumu na kuhudumia wananchi.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Casmir Kyuki ameishukuru Wizara kwa kuendeleza utaratibu wa kusimamia Tume hiyo na anaamini kupitia mafunzo hayo watumishi watatoka na mwamko mpya wa kutekeleza majukumu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news