Wizara:Upungufu wa uzalishaji kwa msimu wa kilimo 2021/22 umeathiri mwenendo wa bei

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imesema, mwenendo wa bei za bidhaa umeendelea kuonesha tofauti za viwango vya bei za jumla na rejareja ambapo bei za baadhi ya bidhaa hasa za vyakula zimeongezeka kutokana na kupungua kwa uzalishaji kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 15, 2022 na Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud S. Kigahe (Mb) wakati akitoa taarifa ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu kwa mwezi huu.

"Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kufanya tathmini ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa lengo la kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mwenendo wa bei nchini.

"Taarifa hizi ni muhimu kwa ajili ya kuwawezesha wadau ikiwa ni pamoja na wazalishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali, walaji wa bidhaa hizo, wenye viwanda na wafanyabiashara kupata taarifa sahihi.

"Lengo likiwa ni kufanya maamuzi sahihi yatakayochangia kukuza uchumi na kipato katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, kaya na Taifa kwa ujumla.Mwenendo wa bei za bidhaa umeendelea kuonesha tofauti za viwango vya bei za jumla na rejareja ambapo bei za baadhi ya bidhaa hasa za vyakula zimeongezeka kutokana na kupungua kwa uzalishaji kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022,"amefafanua Mheshimiwa Kighae.

Aidha, pamoja na upungufu katika uzalishaji kutokana na hali ya hewa isiyoridhisha kwenye maeneo mengi nchini na nchi jirani, Mheshimiwa Kighae amefafanua kuwa, mahitaji ya bidhaa za vyakula kwenye nchi jirani yameongezeka na hivyo kuongeza bei.

Pia amefafanua kuwa, mwenendo wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli duniani zinazochangia mfumuko wa bei umeendelea kuimarika na bei za bidhaa hizo zimeendelea kushuka.

"Hivyo kupunguza gharama za uzalishaji, usafirishaji na uagizaji wa bidhaa na malighafimzinazotumika katika uzalishaji kutoka nje ya nchi.

"Bidhaa za vyakula zilizoathirika zaidi na upungufu wa mvua na hivyo bei zake kupanda ni pamoja na maharage na viazi mviringo,"amefafanua Mheshimiwa Kighae.

Katika hatua nyingine amefafanua kuwa,wizara inaendelea kuratibu ukusanyaji wa takwimu za bei za mazao kutoka kwenye masoko yaliyopo katika mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia Wakusanya Taarifa za Masoko (Market Monitors).

Mheshimiwa Kighae amefafanua kuwa, wizara pia inaratibu ukusanyaji wa taarifa za bei za bidhaa muhimu kama vile bidhaa za vyakula na vifaa vya ujenzi kupitia Maafisa Biashara wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini.

Vilevile, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeendelea kukusanya taarifa za bei kutoka katika masoko yaliyopo katika Mikoa yote ya Tanzania Bara kwa lengo la kukokotoa kiwango cha mfumuko wa bei kila mwezi.

Kutokana na takwimu hizo, Mheshimiwa Kighae amesema bei za bidhaa kwa kila mkoa hupatikana kwa kukokotoa wastani wa bei za mazao na bidhaa katika Mikoa hiyo.

Mahindi

Mheshimiwa Kighae amesema, bei ya mahindi kwa mwezi Desemba ni kati ya shilingi 750 na 1,890 kwa kilo.

Bei ya chini na ya juu imepanda kutoka 700 na 1500 kwa kulinganisha na mwezi Novemba. Mikoa yenye bei ya juu, Mheshimiwa Kighae amefafanua ni Kilimanjaro, Mara na Kigoma na bei ya chini ipo katika mikoa ya Iringa, Njombe, Songwe na Ruvuma.

Akizungumzia bei ya unga wa mahindi kwa mwezi Desemba, Mheshimiwa Kighae amesema ni kati ya shilingi 1,200 na 2,050 kwa kilo.

Pia bei ya chini ya unga wa mahindi imepanda kutoka 1,000 ukilinganisha na mwezi Novemba. Bei ya chini ipo katika mkoa wa Iringa na bei ya juu ipo katika mikoa ya Mara, Kigoma na Kagera.

Mchele

Mheshimiwa Kighae amebainisha kuwa, bei ya mchele kwa mwezi Desemba ni kati ya shilingi 2,200 na 3,500 kwa kilo.

Aidha,bei ya chini na ya juu imepanda kutoka 2,000 na 3,200 kwa kulinganisha na mwezi Novemba. "Mikoa yenye bei ya chini ni Katavi na Ruvuma na bei ya juu ipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Manyara na Arusha,"amesema Mheshimiwa Naibu Waziri.

Maharage

Kwa upande wa maharage, Mheshimiwa Kighae amesema, bei ya maharage kwa mwezi Desemba ni kati ya shilingi 2,200 hadi 3,650 kwa kilo.

Bei ya chini amesema,imepungua kwa shilingi 260 kwa kilo ikilinganishwa na mwezi Novemba. Bei ya juu imepanda hadi shilingi 3,650 kutoka shilingi 3,250 mwezi Novemba.

Amesema, bei ya chini inapatikana katika Mkoa wa Katavi na bei ya juu ipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Manyara na Tabora.

Viazi Mviringo

Aidha, kwa upande wa bei ya viazi mviringo, Mheshimiwa Kighae amesema, kwa mwezi Desemba ni kati ya shilingi 688 na 1,875 kwa kilo.

Amesema,bei ya juu ya viazi mviringo imepanda kwa shilingi 375 ikilinganishwa na mwezi Novemba. Bei ya chini ipo katika mikoa ya Njombe, Songwe na Mbeya na bei ya juu ipo katika mikoa ya Mara na Dar es Salaam.

Unga wa Ngano

Akizungumzia, unga wa ngano, Mheshimiwa Kighae amesema, bei ya unga wa ngano kwa mwezi Desemba ni kati ya shilingi 2,000 na 2,500 kwa kilo.

Bei ya unga wa ngano imeonesha uhimilivu ikilinganishwa na mwezi Novemba. Bei ya juu ipo katika mikoa ya Manyara, Rukwa na Songwe na bei ya chini ipo katika maeneo mengi nchini.

Sukari

Kwa upande wa sukari, Mheshimiwa Kighae amesema, bei ya sukari kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 2,600 na 3,000 kwa kilo.

Bei hiyo,amesema imeonesha uhimilivu ikilinganishwa na mwezi Novemba. Hali hiyo inatokana na jitihada zinazoendelea za kuvutia uwekezaji na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa sukari nchini.

Mafuta ya Kupikia

Mheshimiwa Kighae amesema, bei ya mafuta ya kupikia ya alizeti kwa mwezi Desemba ni kati ya shilingi 4,500 na 7,750 kwa lita.

Vile vile, bei ya mafuta ya kupikia ya Mawese (Korie na Safi) kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 5,000 na 7,600 kwa lita.

Bei ya chini ya mafuta ya kupikia ya alizeti, Mheshimiwa Kighae amesema ipo katika mikoa ya Manyara, Iringa, Tabora na Dodoma na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Mtwara, Mara, Kigoma na Ruvuma.

Saruji

Akizungumzia kwa upande wa mwenendo wa vifaa vya ujenzi, Mheshimiwa Kighae amesema, bei ya saruji kwa mwezi Desemba ni kati ya shilingi 15,000 na 24,000 kwa mfuko wa kilo 50.

Bei hiyo imeonesha uhimilivu ikilinganishwa na mwezi Novemba. Amesema, mikoa yenye bei ya chini ni Tanga, Dar es Salaam, Mtwara, na Pwani na bei ya juu ipo katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Katavi.

Nondo

Kwa upande wa bei ya nondo mm 12 kwa mwezi Desemba, Mheshimiwa Kighae amesema ni kati ya Shilingi 22,650 na 28,000.

Pia amesema,bei ya nondo mm 12 imeonesha uhimilivu ikilinganishwa na mwezi Novemba. Bei za chini zipo katika mikoa ya Kilimanjaro na Dar es Salaam na bei ya juu ipo katika mikoa ya Katavi, Kagera, Iringa na Njombe.

Mheshimiwa Kighae amefafanua kuwa, bei ya nondo mm 10 kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 18,000 na 22,500.

Bei ya nondo mm 10 imeonesha uhimilivu ikilinganishwa na mwezi Novemba. Bei za chini zipo katika mikoa ya Iringa, Kilimanjaro na Mara na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Tabora, Kagera, na Songwe.

Bati

Bei ya bati nyeupe geji 28 kwa mwezi Desemba,Mheshimiwa Kighae amesema ni kati ya shilingi 30,500 na 38,000. Bei ya chini ipo katika Mkoa wa Iringa na bei ya juu ipo katika mikoa ya Manyara na Mara.

Pia amesema, bei ya bati nyeupe geji 30 kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 23,000 na 27,500. Bei ya juu ya bati imeshuka kutoka shilingi 28,500 ukilinganisha na mwezi Novemba.

Bei ya chini ipo katika Mikoa ya Shinyanga, Songwe, Njombe, Mbeya, Katavi Tanga na Dodoma na bei ya juu ipo katika mikoa ya Mara, Kilimanjaro, na Manyara.

Sabuni

Wakati huo huo, Mheshimiwa Kighae akizungumzia kwa upande wa mwenendo wa bei ya bidhaa nyingine amesema hali ya uzalishaji wa bidhaa za sabuni nchini imeendelea kuimarika.

"Nchi yetu ina jumla ya viwanda vikubwa vinane vya sabuni (Detergent and Bar soaps) ambavyo vinahudumia soko la ndani na pia soko la nje hasa katika nchi za Uganda, Burundi, Malawi, Zambia na DRC.

"Aidha, kiasi kikubwa cha sabuni zinazotumika hapa nchini hutengenezwa na wajasiriamali wadogo waliopata mafunzo kutoka SIDO, VETA, na taasisi binafsi.

Hata hivyo, kutokana na mahitaji ya sabuni kuwa makubwa kuliko uwezo uliopo wa uzalishaji wa ndani, sabuni zenye viwango tofauti vya ubora huagizwa kutoka nje, na hivyo kumwezesha mtumiaji wa mwisho kuwa na uchaguzi wa aina ya sabuni kulingana na mahitaji yake,"amefafanua Mheshimiwa Kighae.

Amebainisha kuwa, Serikali kupitia Sera ya Maendeleo ya Viwanda inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa za sabuni hususan sabuni za maji na sabuni za unga ikiwa ni pamoja na kurahisisha taratibu za uingizaji wa malighafi muhimu zinazotumika katika uzalishaji wa sabuni kutoka nje ya nchi.

Sabuni za Miche

Akizungumzia kwa upande wa mwenendo wa bei ya sabuni aina ya Jamaa, White wash na MO kwa mwezi Desemba amesema ni kati ya Shilingi 3,500 na 4,000. Bei ya chini ipo katika mikoa mingi nchini na bei ya juu ipo katika Mkoa wa Rukwa.

"Bei ya Sabuni aina ya Takasa, Kiboko na Kuku kwa mwezi Desemba ni kati ya shilingi 1,600 na 3,500. Bei ya chini ipo katika mikoa ya Katavi, Dodoma, Geita na Morogoro na bei ya juu ipo katika mikoa ya Rukwa na Ruvuma.

"Bei ya sabuni aina ya magadi kwa mwezi Desemba ni kati ya shilingi 1,000 na 3,500. Sabuni za magadi zipo aina mbili nazo ni miche myembamba na miche minene. Bei ya chini ipo katika mikoa ya Katavi, Kigoma, Mwanza, Mtwara na Tanga na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Njombe na Dodoma,"amesema Mheshimiwa Kighae.

Nchi jirani

Mheshimiwa Kighae amesema,kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kwenye kiasi cha mavuno ya mazao muhimu ya chakula kama mchele, mahindi, maharage na viazi mviringo, mahitaji ya bidhaa hizo kwenye nchi jirani yamekuwa makubwa kuliko uzalishaji, hivyo kuchangia kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula nchini na nchi jirani.

Mwenendo wa Bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki (TZS)
Chanzo: World Food Programme (WFP) na Global Product Prices

Aidha, amesema kwa ujumla bei za vyakula katika nchi nyingi duniani zimepanda ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka 2021.

Pia amesema,mfumuko wa bei za vyakula hasa nafaka kama vile ngano umetokana na athari hasi za vita kati ya Urusi na Ukraine na majanga mengine kama vile UVIKO 19 na ukame ulioathiri uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2021/2022.

Hata hivyo, mfumuko wa bei nchini Tanzania ni wa kiwango cha chini zaidi ikilinganishwa na nchi jirani ambapo Tanzania mfumuko wa bei kwa mwezi Novemba ni asilimia 4.9, Kenya asilimia 7.38, Uganda asilimia 10.6 na Rwanda asilimia 21.7.

Masoko

Mheshimiwa Kighae amesema, wizara itaendelea kuimarisha upatikanaji wa taarifa za uhakika za bei za bidhaa na masoko, kufanya uchambuzi na kusambaza kwa wadau.

"Tutaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kupitia Idara mpya ya Uwekezaji Viwanda na Biashara iliyoanzishwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini tupate taarifa za kuaminika kwa wakati kutoka maeneo yote nchini.

"Napenda kutumia fursa hii kuwahimiza Maafisa Biashara kote nchini kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu mwenendo wa bei kwenye maeneo wanayosimamia ikiwa ni pamoja na kukusanya taarifa za bei na kuziwasilisha kwa wakati Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara,"amebainisha Mheshimiwa Kighae.

Mbali na hayo Mheshimiwa Kighae amewahakikishia Watanzania kuwa, Serikali inaendelea kufuatilia na kufanya tathmini ya bei za bidhaa muhimu ili kulinda maslahi ya wadau wote ikiwa ni pamoja na wazalishaji, wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa husika.

"Aidha, ninapenda kutumia fursa hii kuwahimiza wafanyabiashara kote nchini kuendelea kuzingatia misingi ya ushindani wa haki katika kufanya biashara ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi wote,"amesema Mheshimiwa Kighae.

Mheshimiwa Kighae amebainisha kuwa, Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha uzalishaji wa mazao ya chakula ili kudhibiti mfumuko wa bei nchini.

"Tunapoelekea kwenye kipindi cha sherehe za mwisho wa mwaka, napenda kutoa rai kwa wafanyabiashara kote nchini kuepuka tabia ya upandishaji holela wa bei za bidhaa na kuzingatia maadili ya kibiashara na ufanyaji biashara wakati wote,"ameongeza Mheshimiwa Kighae.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news