WIZARA:WANAHABARI KEMEENI UPOTOSHWAJI WA TAARIFA ZINAZOWEZA KULETA TAHARUKI KWA WANANCHI

NA MWANDISHI WAF

WITO umetolewa kwa waandishi wa habari kuandika na kuripoti habari sahihi zinazohusiana na magonjwa ya milipuko na kukemea taarifa za upotoshaji ambazo zinaweza kuleta taharuki na hofu kwa jamii.
Hayo yamebainishwa na Afisa Habari Mwandamizi kutoka kitengo cha Mawasiliano Serikali Wizara ya Afya, Bi. Catherine Sungura wakati wa mafunzo kwa kundi la pili la Waandishi, juu ya namna ya kuandika na kutoa elimu ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola endapo utaingia nchini.

Bi. Catherine amesema Waandishi wa habari ni kundi muhimu katika mapambano dhidhi ya magonjwa ya Mlipuko kwani wanahusika moja kwa moja katika kukabiliana nayo, na hutumia muda mfupi kufikia idadi kubwa ya watu.
“Waandishi mna wajibu wa kutoa elimu za mara kwa mara, kukemea juu ya upotoshaji wa taarifa zinazoweza kuleta tarahuki kwani jamii ina imani na nyie na inaamini kwa kile ambacho mmekuwa mkikiwasilisha kwao.”amesema Bi. Catherine.
Kwa upande wake Mratibu wa Kujikinga na Kudhibiti Magonjwa ya milipuko kutoka Wizara ya Afya Dkt. Joseph Hokororo amesema Serikali kupitia wizara ya Afya imejipanga kuhakikisha ugonjwa huo haungii nchini na halmashauri zote zimetenga vituo ambavyo vitatumika endapo ugonjwa huo utaingia nchini.
Dkt.Hokororo amesema kundi la waandishi wa habari ni miongoni mwa kundi ambalo lipo hatarini kupata maambukizi kutokana na kazi wanayofanya, hivyo wameona ni vyema waweze kuwapatiwa ABC za ugonjwa huo ili iwe rahisi na kwao pia kuweza kutoa elimu kwa jamii ya Watanzania.
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya waandishi wa habari kufuatia mafunzo hayo yaliyotolewa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Management Sciences for Health (MSH) Bi. Aziza Masudi ameshukuru wizara kwa kuwapatia wanahabari wa mkoa wa Dar es salaam mafunzo hayo na wameahidi kuyatumia vyema katika kutolea elimu sahihi kuhusiana na ugonjwa wa Ebola.
“Tunashukuru kwa mafunzo ya kuongeza uelewa zaidi katika kupambana na ugonjwa wa Ebola, na sie tutatumia kalamu zetu na taaluma zetu kwa ufanisi katika kutoa elimu sahihi kwa Watanzania, kikubwa tunaomba ushirikiano kutoka kwetu pindi tutakapouhitaji.”amesema Bi. Aziza.
Mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari mkoa wa Dar es Salam juu ya kuandika na kuripoti habari sahihi za namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola yanatarajia kuhitimishwa Desemba 12, 2022 kwa kundi la Mwisho la waandishi wa habari kuweza kupatiwa mafunzo hayo na ili kuweza kufikia waandishi 120 watakaopatiwa mafunzo hayo kwa mkoa wa Dar es Salaam pekee.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news