Babu Tale amkaribisha Yammi huku akimfunda, asisitiza heshima kwa aliyemshika mkono

NA DIRAMAKINI

BAADA ya mwimbaji Staa wa Bongofleva nchini, Faustina Charles Mfinanga (Nandy) kumtambulisha msanii wake wa kike anayeitwa Yammi atakayepatikana kwenye rekodi ya lebo yake ya The African Princess,Meneja wa Diamond Platinumz na Mbunge wa Morogoro Kusini,Hamisi Shaban Taletale (Babu Tale) amempongeza na kumfunda msanii huyo.

Awali jijini Dar es Salaam, Yammi alizitambulisha nyimbo zake tatu zitakazopatikana kwenye EP yake iliyopewa jina la Three Hearts ikiwemo Namchukia, Tunapendezana na Hanipendi.

Ni katika uzinduzi huo ambao mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Pauline Gekul.

"Haya ndio mambo tunatamani kuyaona yanatokea kila leo kwenye sanaa yetu.Karibu Yammi, karibu kwenye biashara nzuri yenye kila aina ya maneno.

"Kuanzia sasa utapata marafiki wapya wengiiii...humo humo kuna wabaya na wazuri kuwa makini.. heshimu aliyekushika mkono...shangaa na ujiulize kwa nini kawaacha wengine kaamua kwenda na wewe...sio kwamba eti unajua sana kuliko wengine.

"Hapana hiyo ni bahati ambayo wenzio wengi wangetamani iwafikie...yess unakipaji ndio.Ila mwenzie ni nidhamu... nikiwa kama godfaza wa hii sanaa.. nakufungulia huu mlango karibu...nanakutakia mafanikio mema kwenye hii safari yako. Hongera sana,"amefafanua Babu Tale kupitia ukurasa wake wa Instargram.

Nandy anakuwa msanii wa pili wa kike kuanzisha lebo yake, wa kwanza akiwa ni Vanessa Mdee ambaye alikuwa na lebo yake ya Mdee Music.

Nandy amesema kuwa, lengo la kuanzisha lebo hiyo kuwasaidia na kuwainua wasanii chipukizi wa kike nchini na barani Afrika.

"Ninayo furaha kubwa kuileta kwenu rasmi THE AFRICAN PRINCESS LABEL…! 2023 lebel ambayo itahusisha wanawake tu! Kama tunavyoona industry ya watoto wa kike ni chache sana na uthubutu umekuwa ni mdogo so tunaimani na kuomba The African Princess Label itaongeza wingi wa vipaji vya watoto wa kike waliopo mtaaani wenye ndoto kubwa ya kuwa wanamziki.

Aidha, Nandy hakusita kumweleza Yammi kuwa ni miongoni mwa wasanii chipukizi ambao wamekirimiwa sauti nzuri na vipaji vikubwa.

...amepikwa na akapikika. Sasa ni muda wa Dunia kufurahia kipaji kutoka Tanzania," Nandy alieleza kupitia taarifa ya The African Princess Label.

Yammi amebainisha kwamba, hiyo ni ndoto iliyotimia na amewashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono hadi kufikia hatua hiyo muhimu.

"Nauacha ujumbe huu kwa dada, rafiki na shujaa wangu Nandy, sio tu kwa kutambua kipaji changu, lakini kwa maono ya kuongeza thamani katika muziki wa Tanzania kwa kuinua vipaji vya watoto wa kike, mimi ni dhahabu lakini bila kusafishwa ningebaki kuwa jiwe tu. Leo hii mimi ni msanii wa kwanza kuwa chini ya The African Princess Label,"alieleza Yammi.

Katika hatua nyingine, Yammi amesisitiza kuwa, "Kwako wewe shabiki yangu mpya kabla ya yote nasema asante kwa kuniamini, utakapoliskia jina langu “YAMMI” tambua umeona binti mwenye ndoto ya kuwa bora katika muziki, na utakapoisikia sauti yangu tambua ni sauti ya binti wa Malkia.

"Naianza safari hii nakuomba uwe nami leo, Naomba tuwe pamoja na ahadi yangu nitakuwa sababu yako ya kuupenda muziki,"alibainisha.

Post a Comment

0 Comments