Balile: Serikali imetupa heshima kubwa wadau wa habari, mwezi huu tunatarajia itafanya jambo

NA DIRAMAKINI

IKIWA zimebaki siku kadhaa Serikali iweze kutimiza ahadi yake kwa wadau wa habari kuhusu kufanya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari Na.12 ya 2016, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Deodatus Balile ameendelea kuonesha moyo wa shukurani kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Shukurani hizo zinakuja ikiwa Desemba 17, 2022 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye aliwahikikishia wadau wa sekta ya habari nchini kuwa, marekebisho ya sheria hiyo yatafanyika Januari, 2023.
“Hakuna furaha, amani na maendeleo kama uhuru wa habari katika jamii hiyo haupo, hivyo ni muhimu kulinda uhuru wa habari ili vitu hivi viwepo kwenye jamii. Hilo linawezekana na huo ndio msingi wa kongamano hili ambalo linalenga kuleta maendeleo, furaha na msingi wa taifa letu.

“Sheria na kanuni mbalimbali zinaendelea kufanyiwa mabadiliko kwa mujibu wa sheria. Uhuru wa habari unapaswa kulindwa kwa mujibu wa sheria sio utashi wa viongozi. Kiongozi yeyote atakayekuja atalazimika kuulinda uhuru huu kwa mujibu wa sheria hata kama hataki,"alifafanua Mheshimiwa Nape Mheshimiwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 nchini.

Kongamano hilo lilifanyika Desemba 17, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam huku akiahidi marekebisho hayo kufanyika mapema mwezi huu wa kwanza.

Aidha,Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deogratius Balile amesema mwaka 2023 Serikali itaonesha kwa vitendo kile ilichokiahidi tangu mchakato wa mabadiliko ya vipengele vya sheria ya habari uanze.

Amesema, isingekuwa rahisi huwa na matumaini hayo iwapo Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ingeamua kuyapa mgongo malalamiko ya wadau wa habari kuhusu vipengele vinavyozuia ukuaji wa sekta ya habari nchini.
Balile akizungumza na mwandishi wa habari hizi amesema, ushirikiano wa Serikali hususani Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari chini ya Waziri Mheshimiwa Nape Nnauye, umeifanya tasnia ya habari kuwa na matumaini tele ndani ya mwaka huu.

“Mheshimiwa Nape atakumbukwa katika hili, lakini nguvu kubwa kaipata kutokana na Mheshimiwa Rais kuwa positive na jambo hili. Ni matarajio yetu kwamba, mwaka huu wa 2023 utaleta mageuzi katika tasnia ya habari.

“Sisi huku kwenye mikutano ya wadau tumeshamaliza ambapo kikao cha mwisho tulifanya Novemba 21, 2022 na baadaye tukaongeza na Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 lililofanyika Desemba 17, 2022. Hivyo kilichobaki ni Muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kuwasilishwa bungeni baadaye mwezi huu,”amesema Balile.

Amesema, wadau wa habari wanaamini kuwa mawazo yao waliyokubaliana na Serikali katika maeneo yote, ndiyo yatakayokuwemo katika muswaada huo.

Mwenyekiti huyo wa TEF amesema, matarajio ya wadau wa habari ni kuona msuwada huo wa mabadiliko ya sheria ukisomwa bungeni Januari, mwaka huu.

“Kwanza kabisa utapitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kisha utajadiliwa na Kamati ya Makatibu Wakuu na baada ya hapo utajadiliwa na Kamati ya Baraza la Mawaziri.

“Ukitoka hapo utajadiliwa na Baraza la Mawaziri, tunarajia itakuwa kati ya Januari 13 na 14, matazamio yetu ni kwamba utasomwa bungeni kwa mara ya kwanza Januari 31, mwaka huu kisha tutakutana na wadau kuzungumza na wabunge baadae utasomwa kwa mara ya pili na utajadiliwa,”amesema Balile.

Balile amesema kwamba kupitia kauli ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, aliyotoa siku ya Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 muswada huo utawasilishwa bungeni katika bunge linalokuja.

“Kwa kauli ile ya Mheshimiwa Waziri tunaimani kuwa muswaada huo utaingia katika bunge hili la Januari na maisha mengine yaendelee,”amesema Balile.

Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya Sera na Sheria nyingine katika sekta ya habari amesema kuwa, hizo wataziona mbele ya safari.

Desemba 17, 2022 akizungumza katika Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022, Waziri Nape alisema kuwa Serikali ina mpango wa kurekebisha sekta ya habari kupitia mfumo wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kuunganisha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010.

“Pamoja na kupitia upya sera ya nchi ya vyombo vya habari, serikali inapanga kuunganisha sheria zinazohusu masuala ya vyombo vya habari na utangazaji, kwa kuwa zote mbili sasa ziko chini ya wizara moja.

“Ninathibitisha kuwa Serikali itatuma bungeni kwa ajili ya kupitia marekebisho ya vifungu vya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016...Januari mwakani (2023),” alisema Waziri Nape.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news