Banda, Phiri wajiunga na kikosi cha Simba huko Dubai

NA DIRAMAKINI

WINGA wa Kimataifa wa Klabu ya Simba kutoka nchini Malawi, Peter Banda ameanza mazoezi mepesi leo baada ya kukaa nje kwa takribani miezi miwili akiuguza jeraha la mguu.

Banda aliumia kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara dhidi Singida Big Stars uliopigwa Uwanja wa Liti, Novemba 9, 2022.

Banda amesafiri pamoja na kikosi jana kuelekea Dubai kwenye kambi ya mazoezi ya siku saba kujiandaa na mashindano mbalimbali yaliyo mbele ya klabu hiyo yenye maskani yake jijini Dar es Salaam.

Kwenye mazoezi ya kwanza leo hii, kwa mujibu wa taarifa kutoka klabu hiyo, Winga Banda amefanya mazoezi binafsi akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.

Kwa mujibu wa Daktari wa Timu, Edwin Kagabo, Banda atafanya mazoezi hayo kwa siku tatu kabla ya kukabidhiwa kwa kocha wa viungo kwa ajili ya kurejesha utimamu wa mwili na kujiunga moja kwa moja na wenzake.

Naye Moses Phiri amejiunga na kikosi leo akitokea nyumbani kwao Zambia ambapo kuanzia kesho ataanza programu maalumu ya mazoezi.

"Kurejea kwa Banda na Phiri ni furaha kwa Wanasimba katika nyakati hizi ambazo ligi imepamba moto na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inakaribia kuanza mapema mwezi ujao.

"Majeuruhi pekee ambaye amesalia ndani ya kikosi chetu ni Henock Inonga ambaye kwa sasa anauguza jeraha la kidonda baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons,"imefafanua sehemu ya taarifa ya Simba SC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news