Dkt.Kijazi awauma sikio wasajili wa hati nchini

NA ANTHONY ISHENGOMA

KATIBU Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi amewataka Wasajili Wasaidizi wa hati kote nchini kuzingatia maadili ya kazi zao, lakini pia kuhakikisha wanafikia viwango au vigezo walivyojiwekea kama ilivyo katika mkataba wa utoaji huduma kwa wateja wa Wizara ya Ardhi.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi akifuatilia jambo wakati wa Kikao kazi na Wasajili wasaidizi wa hati kutoka mikoa yote hapa nchini, kimefanyika jijini Dodoma.Kushoto kwake ni David Mshendwa Msajili wa Hati wa Wizara ya Ardhi.

Dkt. Kijazi pia amewataka watendaji hao kupunguza urasimu na mlolongo wa taratibu ambazo hazina tija katiza zoezi zima la utoaji hati kwani baada ya tathimini ya robo mbili za mwaka wa fedha Wizara yake imebaini kasi ya utoaji hati bado iko chini sana.

Katibu Mkuu Kijazi alisema hayo jana wakati akiongea na vyombo vya habari mara baada ya kufungua kikao kazi cha siku mbili kinachoendelea Jijini Dododoma kwa wasajili hao kujipanga upya na kuangalia namna bora ya kuboresha sekta yao ikiwemo uboreshaji wa makusanyo wa mapato ya serikali.

Dkt. Kijazi aliongeza kuwa kuna baadhi ya sababu ambazo pia zinatokana na watendaji wenyewe na hivyo kuwataka wabainishe sababu zinazosababisha zoezi la utoaji hati kusuasua wakati huo akiwataka kuwa na mipango ya utoaji elimu kwa umma ili kuhamasisha wananchi kuongeza kasi ya usajili wa hati.
‘’Lazima kila Mkuu wa Kitengo cha Usajili wa hati Mkoani hakikishe kila mwaka angalau hata kama hajafikia malengo kwa asilimia mia moja angalau awe amevuka robo tatu ya malengo ambayo tutakuwa tumejiwekea.’’Aliongeza Dkt. Allan Kijazi Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi.

Katibu Mkuu Kijazi aliviambia vyombo vya habari kuwa kimsingi Wizara yake inakutana na wasajili wa hati wa wasaidizi wa mikoa yote 26 hapa nchini ili kufanya tafakari ya kina katika utendaji wetu hasa katika sehemu hii ya utoaji hati.

Naye Msajili wa Hati Nchini Bw. David Mshendwa alisema wao kama sekta ya usajili wa hati wanakutana ili kufanya tathimini ya kuona ni namna gani wanaweza kuimarisha na kuongeza kasi ya utoaji hati.

Aidha Bw. Mshendwa alibainisha kuwa pamoja na masuala mengine pia kikao chao cha siku mbili kitaangazia namna bora ya kuzidhibiti mapato yatokanayo na zoezi la utoaji hati ambalo amekili pia linakabuiliwa na vitendo vya rushwa pamoja na kughushi nyaraka mbalimbali katika sekta ya ardhi.
Akiongea baada ya mahojiano na vyombo vya Habari Msajili Msaidizi Mwandamizi wa Mkoa wa Arusha Bi. Juliana Ngonyani alibainisha kuwa wako mjini Dodoma kuelezana na kujipanga upya kuangalia namna bora wanavyoweza kuongeza mapato ya serikali ikiwemo kutoa huduma kwa wananchi kama inavyotakiwa.

Sekta ya hati imegawanyika katika sehemu mbili moja ikiwa ni zoezi la utoaji na lingine likiwa ni zoezi la usajili wa hati na mazoezi yote mawili kimsingi yana athari katika mapato ya serikali hivyo ni lengo la serikali kukaa na kutathimini changamoto zilizopo ili kuzifanyia kazi kwa lengo la kuleta ufanisi katika sekta ya ardhi nchini.

Post a Comment

0 Comments