Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) yabaini kuimarika kwa uchumi nchini

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (Monetary Policy Committee-MPC) imebaini kuwa utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa mwezi Novemba na Desemba, 2022 ulikuwa na mafaniko nchini.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Emmanuel Mpawe Tutuba baada ya MPC kukutana Januari 30, 2023 ili kutathmini utekelezaji wa Sera ya Fedha, mwenendo wa uchumi na mwelekeo wa sera ya fedha.

Pia MPC imebaini, kiwango cha ukwasi kilikuwa cha kutosha kwenye uchumi,huku mikopo kwa sekta binafsi ikiendelea kuongezeka kwa kiwango cha juu cha takribani asilimia 21.

"Kasi hii ya ukuaji wa mikopo inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi katika robo ya nne ya mwaka 2022. Vilevile, vigezo vilivyowekwa kwa ajili programu ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) chini ya Mpango wa Extended Credit Facility (ECF) kwa mwezi Desemba 2022, vilifikiwa.

"Kuhusu mwenendo wa uchumi,kamati ilibaini kuwa changamoto za kiuchumi duniani ziliendelea kuathiri shughuli za uzalishaji na kuongeza mfumuko wa bei nchini, japo kwa kasi ndogo. Hii ni kutokana na kupungua kwa makali ya mvurugiko wa mnyororo wa ugavi na bei za bidhaa katika soko la dunia, vikiambatana na hatua zilizochukuliwa na nchi mbalimbali kwa ajili ya kupunguza athari za janga la UVIKO-19,"amefafanua Mwenyekiti wa MPC kupitia taarifa hiyo.

Pamoja na hayo, kamati ilibaini kuwa, mwenendo wa uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar ulikuwa wa kuridhisha katika kipindi cha robo tatu za kwanza za mwaka 2022.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa wastani wa asilimia 5.2, ukilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2021.

"Ukuaji huu ulichangiwa zaidi na shughuli za kilimo, ujenzi na uzalishaji viwandani. Kwa upande wa Zanzibar uchumi ulikua kwa asilimia 5.3 ukilinganishwa na asilimia 5.8, ukichangiwa zaidi na shughuli za malazi na chakula,
ujenzi, viwanda na upangishaji majengo.

"Kutokana na mwenendo huu na viashiria vya kiuchumi katika robo ya nne ya mwaka 2022,kamati inatarajia kuwa malengo ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2022 yatafikiwa.

"Katika mwaka 2023, uchumi unatarajiwa kuimarika zaidi kuliko mwaka uliopita kutokana na ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, uwekezaji wa Serikali kwenye sekta za uzalishaji na miradi ya kimkakati, kuimarika kwa shughuli za utalii, pamoja na mazingira ya biashara na sera wezeshi za fedha na bajeti. Vilevile, kuimarika kwa mnyororo wa ugavi duniani kutachangia ukuaji huu,"amefafanua Mwenyekiti wa MPC kupitia taarifa hiyo.

Wakati huo huo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, mfumuko wa bei uliongezeka kuendana na mwenendo wa bei za bidhaa kutoka nje ya nchi, japo kasi ya ongezeko imepungua.

Mfumuko wa bei kwa Tanzania bara uliongezeka kufikia asilimia 4.9 mwezi Novemba 2022, kabla ya kupungua hadi
asilimia 4.8 mwezi uliofuata.

Aidha, mfumuko wa bei ulikuwa chini ya lengo la asilimia 5.4 kwa mwaka 2022/23 na ndani ya vigezo vya mtangamano wa kiuchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) vya ukomo wa asilimia nane na wigo wa asilimia 3-7, mtawalia.

Mfumuko wa bei kwa Zanzibar ulikuwa asilimia 7.8 na asilimia 8.1 kwa mwezi Novemba na Desemba 2022, ukilinganishwa na lengo la asilimia 5.

Aidha,kamati ilibaini kuwa katika chumi zote mbili, mfumuko wa bei ulikuwa mdogo kuliko nchi nyingi wanachama wa EAC na SADC kutokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kupunguza athari za ongezeko la bei za bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi pamoja na hatua za wananchi kutumia zaidi bidhaa mbadala kutoka ndani ya nchi.

Hata hivyo, mfumuko wa bei unarajiwa kushuka kutokana na kuanza kuimarika mnyororo wa ugavi na matarajio ya ongezeko la uzalishaji chakula.

Katika hatua nyingine, kamati imebainisha kuwa, ujazi wa fedha kwa tafasri pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 11.6 mwezi Desemba 2022, sambamba na lengo la asilimia 10.3 kwa mwaka 2022/23 kutokana na kuendelea kuimarika kwa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi. Aidha, ukuaji huu kwa mujibu wa MPC uliendana pia na malengo ya mfumuko wa bei ya asilimia 5.4.

Pia MPC imebainisha kuwa, ukusanyaji wa mapato ya Serikali ulifanyika kuendana na malengo katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2022/23.

"Ukusanyaji wa mapato ya ndani ulikuwa mzuri kwa Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo makusanyo yalikuwa asilimia 96.7 na asilimia 97.1 ya malengo, mtawalia. Matokeo haya yamechangiwa na kuimarika kwa mifumo ya usimamizi wa ukusanyaji mapato na utayari wa walipa kodi.

"Matumizi ya Serikali yalifanyika kuendana na malengo, sambamba uwekezaji kwenye sekta za uzalishaji na ujenzi wa miundombinu, pamoja na kukabiliana na madhara yatokanayo na athari mbalimbali za misukosuko ya uchumi wa dunia.

"Sekta ya nje iliendelea kuwa thabiti, licha ya changamoto za kiuchumi duniani zilizopelekea kuongezeka kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje,"imefafanua taarifa hiyo.

Kwa upande wa akiba ya fedha za kigeni iliendelea kuwa ya kutosha kugharamia takribani miezi 4.7 ya uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi.

MPC imebainisha kuwa, kiwango hicho ni ndani ya lengo la nchi la miezi isiyopungua minne na kigezo cha mtangamano wa kiuchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) cha kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza angalau miezi minne na nusu.

Aidha, sekta ya benki ilikuwa thabiti, yenye kiwango cha kutosha cha mitaji, ukwasi na yenye kutengeneza faida.
Rasilimali na amana ziliendelea kuongezeka kutokana na kuimarika kwa mazingira ya kibiashara, pamoja na matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kutoa huduma za fedha, ikiwemo kupitia huduma za uwakala.

MPC imebainisha kuwa, kiwango cha mikopo chechefu kiliendelea kupungua na kufikia asilimia 5.8 ya mikopo yote mwezi Desemba 2022, kutoka asilimia 8.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2021.

Aidha, kamati ilibaini na kutambua mafanikio haya kuzingatia kiwango cha asilimia 13 cha mikopo chechefu kilichowahi kufikiwa mwaka 2017.

"Maendeleo haya yanatarajiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa mikopo nafuu kwa sekta binafsi na hivyo kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa.

"Kwa kuzingatia mwenendo wa uchumi pamoja na matarajio katika nusu ya pili ya mwaka 2022/23, Kamati iliridhia Benki Kuu ya Tanzania kuendelea na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi katika uchumi kwa mwezi Januari na Februari, 2023.

"Uamuzi huu unalenga kukabliana na ongezeko la mfumuko wa bei, pamoja na kuchochea kuimarika kwa shughuli za uchumi nchini. Aidha, utekelezaji huu unaendana pia na mikakati iliyowekwa na Benki Kuu ili kufikia malengo ya sera ya fedha yaliyoainishwa kwenye programu ya IMF chini ya mpango wa ECF,"imefafanua taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, kamati inatarajia kuwa mfumuko wa bei utaendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 5.4, huku sera ya fedha ikiendelea kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi na shughuli za kiuchumi kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments