KMC FC kurejea kambini Januari 7

NA DIRAMAKINI

MARA baada ya kikosi cha Timu ya KMC FC kurejea jijini Dar ea Salaam, uongozi umetoa mapumziko ya siku nne kwa wachezaji na kwamba watarejea kambini Jumamosi ya Januari 7, 2023 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo mwingine dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Januari 13, 2023 katika Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro.

Hayo yamebainishwa Januari 6, 2023 kupitia taarifa iliyotolewa na Christina Mwagala ambaye ni Afisa Habari na Mawasiliano KMC FC kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni imerejea ikitokea Mbarali mkoani Mbeya ambapo ilikuwa na mchezo wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara dhidi ya Ihefu uliopigwa Januari 3, 2023 na kupoteza kwa goli moja kwa sifuri.

Wachezaji wa KMC FC wamepewa mapumziko hayo wakati huu ligi ikiwa imesimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi na kwamba Jumamosi ya Januari 7,mwaka huu timu itaanza mazoezi ramsi kwa ajili ya mchezo huo ambao itakuwa ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar.

"Tunakwenda kwenye mapumziko mafupi wakati huu ligi ikiwa imesimama, tumetoka kupoteza mchezo muhimu ugenini, lakini bado tupo kwenye kiwango kizuri na baada ya timu kurejea, Kocha Mkuu Thierry Hitimana na wasaidizi wake watafanyia kazi mapungufu waliyoyaona na hivyo kuendelea kufanya vizuri kwenye michezo inayokuja,"amesema.

Afisa huyo amefafanua kuwa, kwaupande wa hali za wachezaji, bado kuna changamoto ya wachezaji watano ambao wana majeraha ambapo kati ya hao wachezaji watatu ni majeruhi wapya waliotokana na mchezo uliopita dhidi ya Ihefu huku wawili ni wale wamuda mrefu.

Majeruhi wapya ni Baraka Majogoro, George Makang'a pamoja na Ibrahimu Ame huku wale wa muda mrefu ni Hance Masound Msonga pamoja na Emmanue Mvuyekure ambapo wote wanaendelea na matibabu.

Post a Comment

0 Comments