Lissu asema anarejea nyumbani

NA DIRAMAKINI

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mheshimiwa Tundu Lissu amesema,atarudi nyumbani Januari 25,2023 na anatarajia kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kuunganisha Watanzania, kudumisha umoja na mshikamano. Pichani ni Mheshimiwa Rais Dkt.Samia akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Tundu Lissu tarehe 16 Februari, 2022 katika Jiji la Brussels nchini Ubelgiji. Mazungumzo hayo yalifanyika baada ya Rais Dkt.Samia kukubali maombi ya kiongozi huyo wa CHADEMA kukutana naye na kuzungumza jijini humo ambapo walizungumza masuala mbalimbali yenye maslahi na ustawi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ametoa kauli hiyo Januari 13, 2023 wakati akitoa salamu zake za mwaka mpya 2023 wakati akizungumza na Watanzania kwa njia ya mtandao akiwa nchini Ubelgiji.

Mheshimiwa Lissu amesema, 2023 ni mwaka wenye historia nzuri ya nchi na iwapo watu wataamua Katiba mpya itapatikana, akisisitiza hata kurejea kwake ni kwa kazi hiyo.

“Nitarudi nyumbani kutokea Ubelgiji, ninarudi nyumbani kuja kushiriki kuandika kitabu chenye kurasa 365 za mwaka huu 2023 ninaamini kwa umoja wetu tutaandika kitabu kizuri.

“Kwa vyovyote itakavyokuwa, mwaka huu utakuwa mwaka muhimu sana katika historia ya nchi yetu, ni mwaka ambao, kama tukiamua kwa dhati ya mioyo yetu, tutapata Katiba mpya na ya kidemokrasia, yenye mfumo huru wa uchaguzi, inayojali na kulinda haki za wananchi na inayoweka misingi imara ya uwajibikaji wa viongozi wetu kwa wanananchi.

“Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan) na chama chake (Chama Cha Mapinduzi-CCM) na Serikali yake wameshaahidi hadharani kwamba wako tayari kuanza safari hiyo ndefu na ngumu, tunawajibika kumjibu Mheshimiwa Rais kwa kuonesha na kudhihirisha kwa vitendo, kwamba na sisi pia tuko tayari na tumejiandaa kwa safari hiyo."

Hivi karibuni,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan alitangaza kuunda Kamati ya Watanzania itakayoishauri Serikali namna ya kukwamua mchakato wa Katiba kwa kuelekeza namna ya kwenda na suala hilo.

Rais Samia alitoa kauli hiyo Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na viongozi wa vyama 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

“Kwenye suala la Katiba,tunataka kuanza na kamati itakayokuja kutushauri. Katiba hii ni ya Watanzania. Tunaunda Kamati ya Watanzania wote ya kutushauri ni namna gani twende. Kwenye kamati hii kutakuwa na wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali.

"Watakuwepo wanasiasa, wawakilishi wa vyama vya kiraia, wawakilishi wa vyombo vya kiraia, wawakilishi wa jumuiya za kimataifa.

"Tutakuwa na uwakilishi kutoka sehemu zote. Kwa hiyo madai ya Katiba ya muda mrefu sasa yanakwenda kukwamuka na kufanyiwa kazi. Tutakuwa na kamati itakayofanyakazi kwa kupewa hadidu za rejea.

"Hatutakuwa na kamati ya lile vuguvugu. Tunataka wakati vuguvugu hilo linaendelea nchi inaendelea na shughuli zake za maendeleo. Tusipojenga vituo vya afya, barabara mtakuja kunipiga kelele, watu hawawezi kula Katiba…lazima shughuli zingine ziendelee,”alisema Rais Dkt.Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news