Makamu Mwenyekiti CCM Zanzibar,Rais Dkt.Mwinyi atoa maelekezo kwa jumuiya za chama

NA DIRAMAKINI

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amezitaka jumuiya za chama hicho kujijenga kwa nguvu za kiuchumi ili zitekeleze majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipokuwa akimsikiliza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa,Mary Chatanda (wa pili kulia) alipokuwa akisoma taarifa ya jumuiya hiyo walipofika kuonana na Mhe.Rais kwa mazungumzo yaliyofanyika Ikuilu jijini Zanzibar.

Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Ikulu jijini Zanzibar alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Amesema, lazima jumuiya ziwe na nguvu za kiuchumi ili zitekeleze kazi zao kwa wakati na kuongeza kuwa jumuiya isiyo na nguvu za kiuchumi ni ngumu kufanikisha malengo yake, hivyo amewaasa kinamama hao kufanya wawezavyo ili kujiimarisha kiuchumi pamoja na kuwa na zana za kiuchumi vikiwemo vitendea kazi imara.

Rais Dkt.Mwinyi amewaahidi viongozi wa jumuiya hiyo kufanya kazi nao kwa karibu katika kufanikisha malengo ya jumuiya hiyo.

Amewataka viongozi hao kuitumia mikutano ya hadhara kuwaeleza wanachama wao mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa Ilani ya chama.

“Suala la kuitumia mikutano ya hadhara kuelezea mafanikio ya Ilani ya chama ni jambo la msingi, wenzetu wakifanya mikutano watazungumzia kasoro, lakini nyinyi itumieni mikutano kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi chote,”aliiwaasa wanajumuiya hao.

Pia amewataka viongozi hao kupata mafunzo ya mara kwa mara kwa lengo la kutekeleza kazi zao kwa ufanisi kwa mujibu wa taratibu za jumuiya yao.

“Kufanya mafunzo kwa vingozi ni jambo la msingi sana, baada ya kuchaguana, msipofundishana majukumu ya kazi basi kazi hazitofanyika kwa ufanisi, kila mtu atafanya vile anavyojua yeye, ni jambo la msingi sana kufanya mafunzo ili kila mmoja atambue wajibu wake, afanye kazi kwa ufanisi wa hali ya juu,"aliwashauri Rais Dkt.Mwinyi.

Hata hivyo, aliipongeza jumuiya hiyo licha ya majukumu yao kwenye chama, lakini bado wanasimamia wajibu wao kwa wananwake wenzao kwa kushirikiana na jumuiya za watetezi wa wanawake pamoja na vyombo vya kutunga sheria ili kuwatetea kisheria wanapokumbana na matatizo kwenye jamii zao.

Kuhusu kuwawezesha kiuchumi, Dkt.Mwinyi aliiahidi jumuiya hiyo kushirikiana nao katika kuzifikia fursa za kiuchumi ili kuziwezesha jumuiya nyingine ziwe na nguvu za kiuchumi.

Amesema,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kufanya kazi na asasi nyingine zikiwemo NGO’s na taasisi za vyama vya siasa ili kutimiza yote yanayowagusa wananchi.

Akizungumzia masuala ya mikopo kwa wanawake na watu wenye ulemavu, Dkt.Mwinyi alisema Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha inawafikia walengwa wengi kwa kupunguza msururu wa usumbufu kwenye upatikanaji wa fedha hizo ambazo hutolewa na halmashauri, fedha kutoka mifuko ya uwezeshaji inayotoa mikopo isiyo na riba,

“Tuna hakikisha kuwafikia walengwa zaidi na kuweka masharti nafuu kwa vigezo rafiki ili kuondosha uzito wa mchakato wa upatikanwaji wa fedha hizo,”ameahidi Dkt.Mwinyi.

Mapema akiwasilisha matarajio ya UWT mbele hafla hiyo, kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, 2022/2027 Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Halmashauri Kuu Taifa, alisema miongoni mwa matarajio ya jumuiya hiyo ni kuimarisha uhai wake na kuongeza wanachama wengi zaidi, kufanya ziara, kuandaa mikutano ya hadhara kwa kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025, kuwa taasisi na kubwa kifedha, yenye maendeleo makubwa kupitia mikakakti mbalimbali ikiwemo kuanzisha miradi mipya na kusimamia iliyopo kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi.

Alieleza mikakakti ya jumuiya hiyo kwa kuwatumia watanzania waishio ughaibuni katika kusukuma mbele maendeleo ya wanawake nchini, kutumiaji teknolojia ya kisasa kwa kusajili wanachama wake kwa njia ya kielektroniki yenye uwezo wa kutunza kumbukumbu za wanachama kwa upana na kufuatilia hali ya wanachama wake kwa kutanua wigo wa ufanyaji kazi kwa ngazi zote za kiutendaji ili kuimarisha ufanisi wa taasisi kwa matawi yake nchi nzima pamoja na kuanzisha tofuti ya UWT, online TV na mitandao ya kijamii.

Aliongeza mikakati mingine ya jumuiya hiyo ni kufanya mabadiliko ya ushawishi ili kuleta msukumo kwenye mifumo ya sera, sheria, haki ya umiliki wa ardhi kwa wanawake kisheria, mirathi, uongozi, ndoa harakari za uchaguzi na sheria za kimila.

Katika kuyatekeleza hayo aliseleza UWT itafanya kazi kwa karibu na vyombo vya kutunga sheria ikiwemo Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi na Tume za mabadiliko ya sheria kwa Bara na Zanzibar.

Aliongeza pia UWT inatarajiwa kuwa mtandao wa wanawake wenye nguvu zaidi na wenye uchechemuzi ndani na nje ya nchi ili kudhihirisha ukubwa na historia, ndani na nje ya Tanzania kwa kuimarisha vitengo maalumu vya utafiti, sera na maboresho ya malengo ya kwenye mpango mkakati wao.

“Tunatarajia kuwa na utendaji zaidi wa kufuatilia utelekezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM 2025 na mipango ya taifa ya maendeleo ikiwemo kufuatilia bajeti kwa muktadha wa kijinsia, kutumia mbinu mbalimbali za kuzuia na kushughulikia changamoto za wanawake ikiwemo, kujengea uwezo haki za kiuchumi na kiraia kama mbinu za kuwapunguzia changamoto zinazotokana na ukatili wa kijinsia na kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wanawake,”alisema Mwenyekiti huyo.

Hata hivyo, jumuiya hiyo ilimpongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa kuendelea kusimamia nyema masuala yanayowahusu wanawake nchini na kuwaungamkono kenye nyanja zote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news