MBAGALA NI TAMBARARE

NA ADELADIUS MAKWEGA

NYUMBANI kwa mwanakwetu huko Mbagala kuna wakati walikuwa na timu kubwa mbili za soka nazo ni Abuja FC na AFC-TESEMA, habari za timu hizo za mpira wa miguu mwanakwetu anatambua kuwa wapo ndugu zake wa Mbagala tangu enzi kama Kenneth Mkapa, Mwinyi Juma Kondo na wengineo wanaweza wakazielewa vizuri na kuzisimulia zaidi yake mwanakwetu.
Kumbuka tu majina hayo mawili Kondo na Mkapa waliweza kulisakata kabumbu katika timu kubwa kubwa za Tanzania na hata timu yetu ya taifa.

Unapofika Mbagala sasa ukitafuta timu hizo hautazipata, lakini wale wachache wapenda kabumbu watakusimulia na kuyataja majina hayo ya Kondo, Mkapa na mengine mengi, lakini siyo jina la mwanakwetu yeye alikuwa bingwa wa kupiga madochi tu na akiwepo katika kikosi cha hamasa na mikwara ya mjini.

Wakati huo katika kucheza mechi za soka kulikuwa na aina mbili za mechi: Liwalo na Liwe na Mpira Kwapani. Liwalo na liwe hapa mnakwenda kucheza mechi kabla ya mchezo mnakubaliana na matokeo yoyote yatakayotokea hapo uwanjani, hapa hakuna kumpiga refa wala kufanya vurugu, hapa mkifungwa sawa na mkishinda al-hamndulilai.

Kwa Mpira Kwapani hapa mnakwenda katika mechi mnacheza mkishinda tu mechi ni furaha na mkifungwa kutafanyika hila zote goli kurudi mkirudisha mnawafunga –likishindikana hilo mnafanya vurugu mpira kwapani mnaondoka zenu na ushindi wenu wa kibabe au mmefungwa na yoyote atakayeleta vurugu kwa kuwa mna magangwe wengi, hapa wao watawashugulikia vizuri sana.

Hizi timu mbili za Mbagala yaani Temesa na Abuja zilikuwa timu ndugu, tena ndugu wa damu kwa kuoleana au udugu wa kiimani, mara nyingi mechi zao zikichezwa walikuwa wanatumia liwalo na liwe ili kuogopa ndugu kwa ndugu kugombana.
Shida kubwa za mechi za ushindi wa mpira kwapani ushindi wake ni wa kulazimisha , huo ni ushindi haramu, unawapo nguvu walioulazmisha ushindi kwa kutumia mabavu na hilo linawanyima nguvu wale wachezaji wa mpira wenyewe. Hilo linaweza kusababisha wachezaji kubweteka kwa kuwa tutashinda tu. Pia huu ushindi unaleta balaa la fujo na kuumizana na raha ya mchezo haipo tena.

Kwa timu yoyote ikizoea kushinda kwa kutumia mpira kwapani hata inapokwenda kucheza hawa magangwe wakikosekana inakuwa tayari imeshindwa mechi hiyo mapema kisaikolojia maana ni bingwa wa kuuweka mpira kwapani.

Hivi sasa soka limebadilika baada ya kuwa na sheria kali kwa timu zinazoonesha nidhamu mbovu uwajani ndiyo kusema hata balaa na mipira kuwekwa kwapani halipo tena maana sheria zinawabana

Mwanakwetu leo hii anakumbuka siku moja AFC TESEMA walicheza mechi moja na timu moja ya Sifa kutoka Tandika/Temeke liliibuka balaa kubwa. Siku hiyo mapema mwanakwetu alitoka nyumbani kwao kuelekea uwanjani akiambatana na kaka zake wa Mtaani akina Linus na Modestus Kazingoma. 

AFC TESEMA waliwekwa mpira kwapani na mchezo kuishia hapo hapo mwanakwetu alishituka yupo kwao kwa mbio kutokana na vurugu hizo huku kaka zake hawa wawili wakimlinda na kufika nyumbani salama.

Mwanakwetu siku ya leo amezikumbuka timu hizo za Mbagala lakini pia anatafakari nawe msomaji wake namna ya kukumbuka ukikubali kuucheza mpira kumbuka kuna kushinda na kushindwa.Je wewe ni wa mpira kwapani au liwalo naliwe?.Mwanakwetu ngoja niendelee kuiangalia picha hii ya Ken Mkapa na shati lake jekundu, nakumbuka tangu zamani alikuwa anapenda sana rangi nyekundu, sasa jangwani alikwenda kufanya nini? Ndugu yangu huyu ! Lakini hata kushangaa ngamia, vyura na mmbu pia hiyo ilikuwa ni haki yake maana Mbagala ni tambalale.

Mwanakwetu upo? Kwa heri

0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news