MVUA INANYESHA, MAFURIKO KILA KONA

NA ADELADIUS MAKWEGA

KWA mazingira hayo ilionekana watu wawili wazima, mama mtu mzima sana, kijana wake kiume, binti mdogo na watoto wakiwa wanacheza kando, hilo lilithibitishwa na mazungumzo yaliyokuwa yanasikika kwa sauti zao za juu, huku wakiwa huru sana katika Tanzania ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mazungumzo hayo yalikuwa ni ya kidugu mno na kwa bahati nzuri mwanakwetu alikuwa upande wa pili wa eneo hilo ambalo lilikuwa na nyumba nzuri za kisasa, lakini likipakana na nyumba aliyofikia mwanakwetu.

Mazingira haya yalikuwa ya mikoa ya pwani ya Tanzania ambapo manyunyu yalikuwepo huku jua likiwa limekumbatiwa na koti la giza.

Mwanakwetu alifika katika makazi hayo baada ya kufanya kazi na kujilaza na asubuhi yake alipanga aondoke na mabasi ya saa nne kuelekea Dodoma.

Safari hiyo alipanga kuondoka saa nne ili apate wasaa wa kuichaji simu yake na kweli simu hiyo iliwekwa katika soketi na umeme ukawa unainga taratibu mithili ya mtoto anayenyonya titi la mama yake aliyekwisha shiba kumbe alikuwa na njaa kubwa.

Vilisikika vicheko vingi huku sauti ya kiume ikimwambia sasa mama ebu endelea na stori hiyo bwana ebo ! Sauti ya kike ya mama mtu mzima ilisema kuwa nilichanguliwa kuwa Mkuu wa Wilaya mara baada ya kujifungua mtoto wangu wa mwisho, Leila kwa hiyo nilifunga safari hadi huko na kufika mkoani na baadaye kwenda wilayani kuanza majukumu.

Wilaya hiyo ilikuwa na Halimashauri ya Wilaya moja ambapo kwa bahati nzuri Mkurugenzi alikuwa mwanamke mwezangu. Walinipokea vizuri na kuanza kazi vizuri sana.

Sauti ikaingilia sasa mama kama wangekupangia huko ukiwa mjamzito ingekuwaje? Mama mtu akasema nyie wanangu kuweni na heshima mnanifanya mie bibi yenu ehee, alafu akasema haya, “Zamani sikupata bahati ya kuona hilo, lakini mimi nilikwenda huko tayari nimeshajifungua huyu Leila alikuwa mtoto wangu wa mwisho-kitinda mimba.”

Mama huyu aliendelea kusema kuwa alikuwa amejifungua na bibi ya watoto wale alikuwa bado yu hai hivyo alifika na kukaa naye kwa siku kadhaa huku na yeye akiendelea na kazi vizuri sana na hata pale wilayani si wengi walitambua kama alikuwa na mtoto mdogo isipokuwa Mkurugenzi Mtendaji tu ambaye alikuwa akifika hata kwake mara nyingi na huku akimsaidia kumsukasuka nywele za kawaida.“Bibi ulikuwa mbahiri mno mnasukana wenyewe kwa wenyewe? ” Ilisikika sauti ya kike ikisema hilo.

Safari hizo za mama mkurugenzi za kutembeleana na yeye ndipo alipotambua kuwa mheshimiwa ana mtoto mdogo na anamnyonyesha na hilo alibaki nalo moyoni yeye mwenyewe.

“Wakati huo baba yenu alikuwa akitokea Dar es Salaam na kuja nilipo, lakini mama mkurugenzi yeye alikuwa akiishi na mumewe hapo hapo.”aliendelea kusimulia.

Mama wa mheshimiwa huyu alikaa alafu akaaga kuwa anaondoka zake kurudi nyumbani kwao Rufiji. Wakati bi mkubwa huyu anaaga mheshiwa huyu alianza kujiuliza nitafanyaje? Lakini alijipa majibu,

“Katibu wa CCM wa Kata mojawapo angemsaidia tu maana haikuwa shida ya kuwapata mabinti wa kazi katika eneo hilo.”

Urafiki wa kidugu baina yake na mama Mkurugenzi ulisaidia kutambua kuwa mama wa mheshimiwa wake anarudi kwao Rufiji na mama mkurugenzi aliuliza sasa utakaa na nani wa kukusaidia kazi? Alijibiwa bado na maelezo ya matumaini ya kumpata binti huyo kutoka kwa Katibu Kata yalielezwa.

“Mwezangu pale kwangu nimeletewa binti mzuri, mrembo, mweupe mno mie nimepanga nimrudishe kwao, sitaki ugomvi na binti za watu nyumbani kwangu, huku mimi ni kiongozi wa serikali, maana asije akaja kunivunia ndoa yangu.” Mama Mkurugenzi akasema,

Waliulizana wakisema unaogopa hayo? Mama Mkurugenzi akasema ndiyo na kama unamtaka nikuletee aje kwako? “Hilo halina neno mimi namuomba tena sasa hivi.” Mama Mkurugenzi alivyomaliza zoezi la kumsuka akatoka na kwenda kwake na baada ya muda binti huyu alifika nyumbani kwa mheshimiwa kuanza kazi.

Alipofika hapa mheshimiwa huyu alibaini kuwa binti huyu alikuwa anachapa kazi mno, lakini Jumamosi huwa hafanyi kazi kabisa, majukumu yake ya Jumamosi yote aliyafanya Ijumaa na hiyo Jumamosi anakwenda kusali kanisani kwao, kumbe alikuwa Binti wa Msabato.

“Akienda kusali Sabato akirudi mara nyingi mikononi mwake alibeba zawadi nyingi na huku akiwaletea nyinyi na Leila, nyie mlikuwa wadogo wakati huo hamkumbuki tu. Zawadi hizo alikuwa akinunua kwa pesa yake mwenyewe ninayomlipa katika ujira wake wa mwezi.”

Mheshimiwa huyu wa zamani aliongeza kuwa hata aliofanya nao kazi na wengine waliomtembelea nyumbani kwake walimpenda sana, binti huyu kila alipokuwa akienda kusali kanisa alikuwa akivaa na kupendeza mno.

Alisema kuwa alikaa naye karibu miaka minne na mwaka wa tano alibaini kuwa binti huyu akawa anashindwa kupiga deki vizuri kwa kuwa kuinama alikuwa akishindwa na alivyokuwa mwema alilieleza hilo kiungwana kwa mheshimiwa huyu.

“Ninaomba nirudi nyumbani nikajitazamie maana hali yangu siyo nzuri.” Alipomuuliza kuwa mbona hizo ni dalili ni za ujauzito? Alijibu kuwa ni kweli na yeye alihisi kuwa na ujauzito huo. Akamwambia aende Hospitali ya Wilaya akapimwe , kweli alifanya hivyo na alipokwenda kupima iligundulika kuwa na ujaunzito wa miezi minne.

Mheshimiwa huyu alimuomba abaki hapo hapo hili ajifungulie nyumbani kwaka na ni jirani na hospitali kubwa lakini alisema hapana ni vizuri akajifungulie kwao. Kweli akamfungashia haki na zawadi zake kadhaa akasindikizwa na kwenda kwao.

Msomaji wangu kumbuka mwanakwetu hapo yupo upande wa pili wa nyumba hii anasikiliza mjadala huo, mara sauti ya kiume ambayo ni ya yule kijana wa mama huyu ikasikika ikisema sasa mama je ulitambua kuwa ujauzito huo ulikuwa wa nani? Mheshimiwa huyu mstaafu akasema nyie watoto mimi siyo nyanya wenu… Mara sauti ya binti mdogo ilisikika upande wa mazungumzo haya yalipokuwa yanafanyika, “Bibi umeme umekatika, bibi umeme umakatika…”

“Si walisema kuwa maji yalipungua, mbona sasa mvua zinayesha na mafuriko kila kona ? ” Hapo ilisikika sauti ya kiume.

Mwanakwetu akaitazama simu yake ikawa imejaa 59% akaitoa katika soketi na kuiweka chaji hiyo katika begi lake na kutoka katika nyumba hii na kuianza safari ya Idodomia.

Mwanakwetu upo?. Kwa heri?
makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news