UTAJIRIKE MANDONGA

NA LWAGA MWAMBANDE

NYOTA ya Bondia Mtanzania Karim Mandonga (Mtu Kazi) ameendelea kung'ara siku hadi siku. Hii ni kutokana na juhudi zake binafsi ambazo zimewezesha kukubalika haraka katika kazi zake za ubondia.

Na Watanzania licha ya kufurahia kazi ya mikono yake, wameendelea kumpa zawadi mbalimbali ikiwemo magari ikiwa ni kama njia ya motisha ili aweze kufanya vizuri zaidi.

Hivi karibuni alianza kupokea zawadi ya kwanza ya gari ya Nadia kutoka kwa mfanyabiashara Dick Sound na baadaye Subaru Impreza kutoka Kampuni ya Mo Green International baada ya kumtwanga Mkenya Daniel Wanyonyi ambaye alimshinda katika raundi ya tano kwa TKO akitumia ngumi aliyoipa jina la Sugunyo.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande licha ya kumtakia kila la heri Mandonga pia amesema anatarajia ngumi mpya inayoitwa 'Mo Strong Kantangaze' itaendeleza ushindi zaidi. Endelea;


1:Utajirike Mandonga, jasho lako linalipa,
Wanyonyi livyomgonga, uwakilishi walipa,
Magari yanajipanga, ya kwako si ya kukopa,
Nadia sasa Subaru, hongera sana Mandonga.

2:Nadia sasa Subaru, hongera sana Mandonga,
Unazidi pata nuru, maendeleo yasonga,
Sasa wapata uhuru, mambo yako kuyapanga,
Mali ikiongezeka, na walaji wanazidi.

3:Mali ikiongezeka, na walaji wanazidi,
Ni vema ukazishika, na tena uwe stadi,
Zisije zikatoweka, ziliwe na makuwadi,
Mali za jasho na damu, hakikisha zakutoa.

4:Mali za jasho na damu, hakikisha zakutoa,
Kwa matumizi muhimu, upite ukikohoa,
Muda kutesa kwa zamu, kwa jasho ulilotoa,
Heri tunakutakia, katika maisha yako.

5:Heri tunakutakia, katika maisha yako,
Bora zidi kuvutia, masponsa kuja kwako,
Na uzidi jipatia, mali nyingi huko kwako,
Waliokupa magari, pongezi zifike kwao.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news