NECTA, hofu ya nini kushindwa kuwaheshimisha Tanzania One kama desturi?

NA PROF.FR.THADEUS MKAMWA

MAAMUZI ya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kutotangaza washindi katika mitihani ya taifa ni wazo zuri kinadharia kwa sababu linawapa moyo walioshindwa kwamba nao wana nafasi yao katika elimu.

Huenda ni nadharia nzuri ya kuwanyenyekesha washindi kwa kuwanyima haki yao ya kufurahia perfomance yao.

Katika High performance work systems hata viwanda, taasisi, na wafanyakazi wana haki ya kujua wameperform kiasi gani dhidi ya washindwanishwa.

Ndio maana kuna Fortune 500, nk. Ni wazo bovu kiuhalisia kwa sababu kudai kwamba ukimtangaza aliyeshinda kuliko wote ni kumpigia debe ni kujidanganya.

Wa kwanza ni wa kwanza tu hata umuite wa mwisho na debe amejipigia mwenyewe kwa performance yake.

Wewe mtangazaji unatangaza tu huongezi wala hupunguzi huo ushindi. Wito mzuri kwa shule zote zinazofanya vizuri zisikatishwe tamaa kwa kufunikwa katika blanketi la nadharia ambayo haina tija katika nyanja mbalimbali.

Sijui kwamba kuna siku ushindani utafifishwa duniani kwa nadhari za namna hii. Mfano, mfumo wa vyuo vikuu duniani una vipimo- wana rank chuo cha kwanza mpaka cha elfu hamsini na ushee, kwa hiyo shule chache za Tanzania kujua zipi ni top 10 au top 100 sio jinai na wala sio dhambi.

Mwaka huu zile shule zetu za mwisho Tanzania hazina sababu ya kujitafakari kwanza kwa sababu ziko katika mazingira magumu.

Zinaonewa huruma kwa kuwa kuzitangaza ni kuzidhalilisha au kuziaibisha na pia ni kuwaaibisha wamiliki wao.

Zaidi sana nionavyo mimi tunaziumiza zaidi kwa sababu shule hizo labda zisubiri mpaka Injili itakapotimia kwamba wa kwanza atakuwa wa mwisho na wa mwisho atakuwa wa kwanza.

Ni wazi sio wote wanaokuwa wa kwanza katika mitihani wanakuwa wa kwanza katika mitihani ya maisha.

Na sio wote wanaoshindwa katika mitihani ya taaluma wanashindwa maisha. Sasa, hofu ya nini kushindwa kuwaheshimisha Tanzania One kama desturi?.

Kwangu mimi naona wamekosewa jambo kubwa katika maendeleo yao ya kielimu katika uchanga wao. Tujenge elimu katika ukweli na uwazi.

Mwandishi Prof.Fr.Thadeus Mkamwa ni Makamu Mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha St.Augustine jijini Mwanza.

Post a Comment

0 Comments