OMEA...tamthilia punguza, usije ukaunguza

NA LWAGA MWAMBANDE

KISWAHILI ni lugha moja miongoni mwa lugha za Kibantu inayozungumza katika Bara la Afrika, hasa Afrika Mashariki yenye asili ya watu wa mwambao.

Muhimu omea maji, hadi chakula kiive.

Hii ndiyo lugha rasmi ya Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo licha ya kuhusishwa na lahaja za Kiarabu, bado imeendelea kuwa na utajiri mkubwa wa maneno.

Ni kwa umuhimu huo, Julai 7, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza rasmi tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.

Taarifa hiyo ilitangazwa kwenye makao makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa wakati wa mkutano wa nchi wanachama wa shirika hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Twitter wa UNESCO wakati huo, azimio maalum la kuitangaza siku hiyo lilipitishwa na wanachama wote bila kupingwa.

Hatua hiyo iliikifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa na kuwa na siku maalum ya kuadhimishwa.

Kiswahili hadi sasa tayari kinatambulika kama miongoni mwa lugha rasmi kwenye Muungano wa Afrika, na kinatumika kama lugha rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bunge la Afrika na ni moja ya lugha za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi duniani.

Awali Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Prof.Kennedy Gastorn alibainisha kuwa, siku hiyo ilichaguliwa kwa sababu Julai 7, 1954, Tanganyika African National Union (TANU) kwa maana ya chama tawala cha Tanganyika wakati huo kilichoongozwa na (Hayati) Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kilitangaza Kiswahili kuwa nyenzo muhimu katika kupigania Uhuru.

Katika miaka ya 1950 Umoja wa Mataifa ulianzisha Kitengo cha lugha ya Kiswahili cha Redio ya Umoja wa Mataifa, na na sasa Kiswahili ndiyo lugha pekee ya Kiafrika ndani ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Kimataifa katika Umoja wa Mataifa.

Aidha, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kupitia azimio lake la 71/328 la Septemba 11, 2017 kuhusu lugha nyingi, lilikaribisha utekelezaji wa siku maalumu kwa kila lugha rasmi ili kufahamisha na kuongeza ufahamu wa historia, utamaduni na matumizi yake, na kuhimiza Katibu Mkuu na taasisi kama vile UNESCO kuzingatia kupanua mpango huu muhimu kwa lugha zingine zisizo rasmi zinazozungumzwa kote ulimwenguni.

Kwa msingi huo, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anaendelea kusisitiza kuwa, lugha ya Kiswahili imepanuka na ina maneno mengi yaliyobeba maana nzuri katika shughuli zetu na maisha ya kila siku. Endelea;

1:Tamthilia punguza, usije ukaunguza,
Chakula bora kuwaza, pika hadi kumaliza,
Kisha utajituliza, ufanye unaloweza,
Muhimu omea maji, hadi chakula kiive.

2:Kande ili kuziweza, ziive bila saza,
Omea na fululiza, na moto ukiongeza,
Hapo vema utaweza, ziive kwa kukoleza,
Muhimu omea maji, hadi chakula kiive.

2:Muda nimekuchunguza, michezo ndiyo wawaza,
Muda moto kukoleza, wewe uko kuigiza,
Hao jua wakuchuza, chakula utaunguza,
Muhimu omea maji, hadi chakula kiive.

3:Muda ukipitiliza, ushauri kuubeza,
Chakula ukaunguza, na njaa ukatulaza,
Kwenu jua taongoza, mume ukimchukiza,
Muhimu omea maji, hadi chakula kiive.

4:Siyo najipendeza, haya ninakueleza,
Au ninakuchokoza, kuvunja lako baraza,
Nafanya kujiongeza, usije njaa tulaza,
Muhimu omea maji, hadi chakula kiive.

5:Eti unajieleza, kazi zote unaweza,
Kuona wakiigiza, chungu bila kuunguza,
Jua unajipoteza, majuto kwako ajuza,
Muhimu omea maji, hadi chakula kiive.

6:Ongeza maji ongeza, omea nakuchagiza,
Raha zako kipunguza, umakini taongeza,
Na kupiga utaweza, chakula cha kukoleza,
Muhimu omea maji, hadi chakula kiive.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news