Rais Dkt.Mwinyi:Elimu ni kipaumbele changu cha kwanza

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imejipanga vizuri kuiletea mabadiliko makubwa katika Sekta ya Elimu visiwani humo ili kuongeza ufaulu kwa wanafuzi wengi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi ya kompyuta mpakato mwanafunsi wa Skuli ya Sekondari ya Lumumba kidato cha nne Msabaha Shaban Kassim, kwa kufanya vizuri mitihani yake ya kidato cha nne mwaka 2022 na kupata Daraja la Kwanza kulia ni Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe.Leila Mohammed Mussa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Tanzania, Mhe. Prof.Adolf Mkenda, hafla hiyo ya kukabidhiwa kompyuta kwa wanafunzi wa kidato cha sita na cha nne waliofanya vizuri mitihani yao kwa mwaka 2022, iliyofanyika Januari 11, 2023 katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Januari 11, 2023 Ikulu mjini Unguja alipowakabidhi kompyuta wanafunzi 1,142 waliofanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha nne na sita ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake kwao.
Amesema, bila elimu hakuna taifa linalofanikiwa kwa maendeleo na kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imejipanga kufanya mageuzi makubwa kuondosha changamoto zinazoikabili wizara hiyo na kuongeza kuwa elimu ni kipaumbale chake cha kwanza.
“Huwezi kupata maendeleo yoyote uliyoyakusudia kuyafanya kama huna wataalamu, kwa hiyo elimu itaendelea kuwa kipaumbele cha kwanza cha Serikali,”ameeleza Dkt.Mwinyi.

Ameeleza Serikali ilivyojipanga kuboresha miundombinu kwa kuelendelea kujenga skuli mpya za ghorofa zenye kompyuta, maktaba na maabara kwa msingi na sekondari pamoja na kuondosha mikondo kwenye skuli zote za serikali ili wanafunzi wasome mara moja tu kwa awamu.
Dkt.Mwinyi ameongeza kwamba, mwaka huu wa 2023 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kujenga madarasa mapya mengine yasiyopungua 2000 ambayo yatasheheni vitendea kazi vikiwemo madawati, vifaa vya maabara na vitabu pamoja na kuongeza wataalamu wakiwemo walimu wa Sayasi na Hesabati.

“Tuna uhaba wa walimu katika fani mbalimbali hususanI walimu wa sayansi na Hesabati, kwa hiyo lazima tuongeze walimu wa sayansi, lazima tuongeze walimu wa hesabati, lazima tuongeze mafunzo kwa waalimu ili watoe watalamu wengi wa sayansi,” ameeleza Dkt.Mwinyi.

Aidha, amewataka watendaji wa Wizara ya Elimu kurejesha utamaduni wa ukaguzi kwa skuli ya serikali pamoja na kuangalia upya suala la lugha kwa wanafunzi wa madarasa ya msingi ili kuondosha changamoto ya kutojua lugha kwa wanafunzi kwenye skuli za serikali.
Hata hivyo, Dkt.Mwinyi amewaomba wadau wote wa Elimu Zanzibar kuendelea kuiunga mkono serikali katika kufanikisha azima ya Mapinduzi ya kuimarisha elimu visiwani inaongezaka na kueleza kuwa serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu badala yake ushirikiano wao utaleta tija kuongeza maendeleo kwenye sekta hiyo.

Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Prf.Adolf Mkenda alieleza hatua ya Dkt.Mwinyi kuwazawadia wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye mitihani yao ya taifa itachochea juhudi za kuongeza ufaulu visiwani na kueleza wanafunzi hao mbali na kunufaika kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lakini pia wananufaika kupitia udhamini wa Samia Suluhu Hassan ambao unatoa udhamini wa masomo ya elimu ya juu wa asilimia mia moja kwa wanafunzi wote wanaofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi.

Prof.Mkenda amesema Zanzibar ilitoa skuli 10 kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi na kunufaika na udhamini huo ikiwemo Skuli ya Sekondari ya Lumumba.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa amemshukru Dk.Mwinyi kwa ugawaji wa kompyuta hizo na vishkwambi kwa walimu wa skuli zote za serikali za Unguja na Pemba na kueleza kuwa vifaa hivyo vitaongeza nguvu kwenye mradi mkubwa kwa wa e.WEMA wizarani hapo na kueleza kuwa mradi huo utaunganisha wizara na taasisi zake zote, wanafunzi na walimu wa skuli zote za msingi na sekondari na kila mtendaji wa Wizara na Idara zake.

Aidha, Waziri Lela amesema mradi huo utaisaidia wizara, idara na taassisi zake kupata taarifa wanazozihitaji kitaaluma kwa usahihi na wakati bila ya kutumia mtandao na kueleza kwamba mradi huo upo chini ya Idara ya Tehama kutoka Wizara ya Elimu, Zanzibar inashirikiana na Serikali ya Ausralia ambao pia utahusisha ofisi zote za elimu za mikoa,wilaya na vituo vya elimu.
Jumla ya wanafunzi 1142 waliofaulu daraja la kwanza walikabidhiwa kompyuta mpakato na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi, Ikulu Zanzibar ambapo wanafunzi 449 kati ya hao kutoka kidato cha nne na wanafunzi 693 wa kitato cha sita kwa skuli za Serikali na binafsi kwa upande wa Unguja.

Kwa upande wa Pemba jumla ya wanafunzi 288 walipata daraja la kwanza kati ya hao137 kidato cha nne na 151 kidato cha sita.
Aidha, jumla ya vishkwambi 6,600 kutoka Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambavyo ni sehemu ya vishikwambi vilivyotumika kwenye sensa ya watu na makaazi Tanzania ya mwaka 2022,Dkt.Mwinyi alivikabidhi kwa walimu wa skuli za serikali za Unguja na Pemba chini ya usimamizi wa walimu wakuu wa skuli hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news