Serikali yatoa msaada kwa waathirika wa mafuriko ya maji Mbeya

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu imetoa msaada kwa wananchi walioathirika na maafa ya mafuriko ya maji mkoani Mbeya, yaliyosabisha nyumba kubomoka, kuharibika kwa vifaa, vyakula, uharibifu wa mifugo na mazao yaliyoko mashambani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe.George Simbachawene akikitembelea moja ya nyumba ya watu walioathirika na mafuriko ya maji katika Kata ya Igawilo jijini Mbeya.

“Msaada huo unajumuisha magodoro 300 kwa kuanzia, mablanketi 1,200 ya wakubwa na wadogo, mikeka 600, madumu ya maji, sufuria, bakuli sahani pamoja na vijiko kwa kila familia ambayo imeathirika.”

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene alipotembelea maeneo yaliyoathirika wa mafuriko ya mvua katika kata saba mkoani Mbeya kutokana na mvua zilizonyesha Januari 7,2023.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe.George Simbachawene akikabidhi mablanketi ya msaada kwa ajili ya waathirika wa mafuriko ya maji Mbeya kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera (katikati) na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Tulia Ackson.

“Kwa mujibu wa Sheria Na. 6 ya Maafa ya Mwaka 2022 sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu tunayo dhamana ya kuwaunganisha wadau ili kuwasaidia watu walioathirika na tutafanya hivyo kwa kutumia ofisi zetu za mkoa na wilaya, naomba wadau wote wa ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya kutusaidia ili kuhakikisha watu hawa wanarudi katika hali yao.”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe.George Simbachawene akizungumza na mama ambaye ni moja wa waathirika wa mafuriko ya maji katika Kata ya Iduda jijijini Mbeya.

"Natoa pole kwa wote walioathirika, TARURA kwa kushirikiana TANROADS Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Mbeya Vijijini wahakikishe wanaenda kuona kwenye vyanzo kuangalia ni eneo gani maji yametoka kwenye mkondo wake wa asili."

Akimkaribisha Waziri wa Nchi, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Tulia Ackson ameishukuru Serikali kwa mchango iliyoutoa kwa waathirika wa mafuriko ya mvua mkoani Mbeya .
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe.George Simbachawene akizungumza na mkazi wa Kata ya Uyole (kushoto) ambaye ambaye ni mmoja wa waathirika wa mafuriko ya maji. 

“Naomba sisi kama halmashauri tusitoe vibali vya ujenzi kwenye maeneo ambayo ni mikondo ya maji, kwa sababu athari za mafuriko zinarudisha nyuma maendeleo ya uchumi kwa wananchi.”

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe.Juma Homera katika taarifa yake amesema watu waliopata athari za mafuriko ya maji, kaya 281 zenye watu idadi ya watu 1,405 ambao wanahitaji chakula takribani tani 50 kwa miezi mitatu ili ziweze kuwasaidia.

Post a Comment

0 Comments