Rais Dkt.Mwinyi:Nitashirikiana na vijana kuijenga nchi

NA DIRAMAKINI

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaahidi vijana kushirikiana nao katika kufanya kazi za ujenzi wa maendeleo ya nchi.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Kiongozi wa Matembezi ya Vijana wa (UVCCM), Lulu Saleh picha ya Rais wa Kwanza wa Zanziba,Hayati Abeid Amani Karume, wakati wa uzinduzi wa Matembezi ya Vijana wa (UVCCM) yaliyozinduliwa Januari 5,2023 katika viwanja vya Mapinduzi Square Michezani Muembe Kisonge Wilaya ya Mjini Unguja.(Picha na Ikulu).

Amesema, vijana ni nguzo muhimu katika kusukuma mbele maendeleo ya uchumi wa taifa ndio sababu ya Serikali za SMZ na SMT zimeteua vijana wengi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ili kuwapatia uzoefu wa kuongoza nchi yao kwa uwezo na weledi wa kuchapa kazi na kuijenga nchi kiuchumi na maendeleo.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo huko viwanja vya Mnara wa Kisonge, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi wakati wa shehere za uzinduzi wa matembezi ya vijana ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele chake ni Januari 12, mwaka huu.

Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, vijana wana nafasi kubwa ya kutumikia taifa lao na kuliletea maendeleo sambamba na kuwaasa vijana hao kwamba wanapaswa kujitambua kwa kujiweka imara ili kufanikisha malengo ya ukombozi wa kweli kwenye jamii zao.
“Kama nyote mnafahamu kwamba nchi yetu ilipata Uhuru tarehe 12 Januari mwaka 1964, kwa njia ya kufanya Mapinduzi ambayo kwa kiasi kikubwa yaliendeshwa na vijana wakati huo,” amesema Rais Dkt.Mwinyi.

Aidha, amewaeleza kwamba kazi iliyo mbele yao ni kujenga nchi baada ya kupata uhuru pamoja na kuwakumbusha kwenye suala muhimu la kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamamo katika jamii ambayo ndio chachu ya maendeleo ya nchi ilipofikia.Dkt.Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwashauri vijana hao kushikamana na kusaidiana katika kutafuta na kujitengenezea ajira ili kujitatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kujitafutia maendeleo.
“Tambueni Serikali yenu ya Awamu ya Nane inaunga mkono juhudi zenu zinazofanikisha kuondoa changamoto za ajira nchini na kujiletea maendeleo katika jamii zenu,”amesema Rais Dkt.Mwinyi.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuweka mazingira wezeshi kwa makundi yote ya vijana kwa lengo la kuwapatia fursa za ajira vijana kwa namna yoyote iliyo bora na sahihi kwa mijibu wa sheria na taratibu za nchi.
Akizungumzia suala la vikundi vya maendeleo ya vijana, Dkt. Mwinyi amewaahidi kwamba serikali itawapatia mikopo kwaaajili ya kuendeleza juhudi zao za maendeleo na kueleza kuwa atazisimamia mamlaka husika ili ziwape vijana kipaumbele kwenye wepesi wa kupata mikopo ili wanufaike na mipango ya serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Pia amesema, serikali zote mbili za SMZ na SMT zimeweka mifumo mizuri ya kuwawezesha vijana kupata ajira kupitia sekta za umma na binafsi, mifumo aliyoieleza kwamba imewaepusha vijana kuepukana na mambo maovu, kuwajenga vijana kuwa wazalendo raia wema kwa taifa lao na kuwafanya vijana kujiona fahari kufanya kazi za kujitolea katika kujiletea maeneleo ya nchi yao.
“Nyinyi Umoja wa Vijana wa CCM mna dhima kubwa ya kuwaongoza na kuwaelekeza vijana wenzenu kuwa na maono hayo,”Rais Dkt.Mwinyi amewashauri vijana hao.

Dkt.Mwinyi amewataka vijana kutumia mbinu tofauti kwa kuwafundisha vijana wenzao jinsi ya kuwa wazalendo kwa kujiepusha kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwemo matumizi ya dawa za kulenya, udhalilishaji na vitendo vyote vya uvunjifu wa sheria za nchi.

Akizungmza kwenye hafla hiyo, Mlezi wa Umoja wa Vijana wa CCM, Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi amewaasa vijana hayo kuzidisha nidhamu kwenye kutumikia chama chao na kuwaomba kuendelea kuisemea vizuri serikali yao na juhudi za maendeleo zinazofanywa na chama chao.
Aidha, amewaasa kuendelea kuchukua tahadahari kwenye jamii zao kwani bado ugonjwa wa korona upo duniani na Zanzibar ni kisiwa chenye mchanganyiko wa watu kutoka mataifa mengi hiyo aliwaomba vijana hao kushajihisha umuhimu wa chanjo ili kujinusuru sambamba na kuwaasa kuendelea kupiga vita dhidi ya udhalilishaji wa wanawake na watoto ilikujenga jamii iliyo bora.

Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Abdalla Juma Mabodi amewaasa vijana hao kuhubiri maridhiano ya nchi ili kudumisha jamii yenye umoja na mshikamano katika kujenga taifa lenye maendeleo ya amani na utulivu.

Amesema, Chama Cha Mapinduzi daima kinaungamkono juhudi za serikali na lazima kifuate maagizo na maono ya viongozi wa nchi.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM Taifa na Mjumbe wa Kamati ya Halmashauri Kuu taifa, Komredi Muhammed Ali Kawaida amesema, vijana watatumia fursa iliyotolewa na serikali ya kufanya mikutano ya hadhara kwa kuyasemea mazuri yote zanayofanywa na serikali za SMZ na SMT na kwamba chama chao cha CCM kitaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali mbili hizo.
Matembezi hayo ya vijana yataendelea kwa siku saba mfululizo yenye kauli mbiu yake “Uchumi wa buluu kwa maendeleo ya viwanda, vijana tuachangamkie fursa” yanajumuisha shughuli mbambali za ujenzi wa taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news