Rais Dkt.Samia aruhusu mikutano ya vyama vya kisiasa nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza kuondoa rasmi tangazo la zuio la kufanya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa nchini.
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ametangaza hayo leo Januari 3, 2023 wakati akizungumza na Viongozi wa Kitaifa wa Vyama vya Siasa Ikulu jijini Dar es Salaam.

"Kwa sheria zetu ni haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano yao ya hadhara...nimekuja kutangaza kuondoa zuio la kuzuia mikutano ya hadhara na ninasema kwamba, sasa linaondoka,"amesisitiza.

Rais Dkt. Samia amesema, jukumu sasa linabaki kwa vyama vya siasa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola kama sheria na kanuni zinavyoelekeza ili vipatiwe ulinzi.

Pia amesema hatua waliyoifikia katika mazungumzo baina ya vyama hivyo na Serikali kwa sasa, mikutano hiyo haitazuiliwa tena.

"Ruhusa ya mikutano ya kisiasa itatolewa, wajibu wetu sisi Serikali ni kuwalinda mfanye mikutano yenu salama mmalize vizuri, kufuata kanuni ndio wajibu wenu vyama vya siasa.

“Ni haki kwa vyama vya siasa kuendesha mikutano ya hadhara lakini ndugu zangu tuna wajibu. Kwa upande wa serikali tumeshajipa wajibu wetu kuwa ni kulinda mikutano ya vyama vya siasa, wajibu wenu vyama vya siasa ni kutupa taarifa kama sheria na kanuni zinavyosema kisha vyombo vinatoa ruhusa.

“Wakiona kuna hatari hawatoi ruhusa kwa hatua tuliyofika ruhusa za kufanya mikutano zitatolewa kwa sababu wajibu wetu ni kuwalinda mfanye mikutano kwa usalama, mmalize vizuri muondoke vizuri.

"Mimi siwaiti nyie vyama vya upinzani, vyama vya kuwaonyesha changamoto zilipo, mnapinga nini, mnampinga nani, ndani ya Tanzania tunapingana kweli, tunaonyeshana changamoto ziko wapi, kasoro ziko wapi na mkinionyesha nikiwa msikivu nikazitekeleza nitaongeza imani kwa wananchi.”

“Mazungumzo baina ya Serikali na vyama vya siasa bado yanaendelea, kuna mambo mengi ambayo itabidi tuitane, tuzungumze, tushauriwe, tukubali, tukatae kwa hoja lakini hivyo mazungumzo na maridhiano bado yanaendelea,"amesisitiza.
Mikutano hiyo ilizuiwa muda mfupi baada ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuingia madarakani kupitia uchaguzi mkuu wa 2015.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news