Rais Luiz Inacio Lula da Silva aapishwa rasmi, ambeza mtangulizi wake

NA DIRAMAKINI

LUIZ Inacio Lula da Silva wa Brazil kupitia Chama cha Wafanyakazi (PT) ameapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Brazil akiwa amerejea tena katika nafasi hiyo ambayo aliitumikia kuanzia mwaka 2003 hadi 2010.
Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Jamhuri ya Shirikisho la Brazil akiwapungia mkono wafuasi wake Januari Mosi, 2023. (Picha na Ricardo Stuckert).

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 77 ameapishwa Januari Mosi, 2023 ikiwa ni muhula wake wa tatu baada ya kumshinda Jair Messias Bolsonaro anayeegemea katika siasa kali za mrengo wa kulia mnamo Oktoba,2022 wakati wa kinyang'anyiro kikali zaidi cha urais katika miongo kadhaa iliyopita katika Taifa hilo la Amerika Kusini.

Lula alimshinda Bolsonaro kwa chini ya asilimia mbili ya kura kupitia duru ya pili ya uchaguzi. Kiongozi huyo wa siasa kali za mrengo wa kulia alikataa kukubali kushindwa na kutilia shaka mfumo wa kupiga kura wa kielektroniki nchini humo.

Ameahidi nini?

Lula da Silva wakati akila kiapo cha urais katika ya Bunge la Congress jijini Brasilia ameapa kudumisha, kutetea na kuilinda Katiba ya nchi hiyo.

Pia ameahidi kuwaokoa watu milioni 33 kutokana na njaa kali na watu milioni 100 kutoka katika umaskini uliotamalaki ikiwa ni nusu ya wakazi milioni 215 nchini humo.

Amesema, anakwenda kuijenga upya Brazil iweze kutoka katika magofu ambayo Serikali ya awali iliyaacha, ingawa alisema hayo bila kumtaja mtangulizi wake Bolsonaro kwa jina.
"Kati ya magofu haya ya kutisha, pamoja na watu wa Brazil, ninachukua jukumu la kujenga upya nchi na kuifanya kuwa taifa la watu wote na lenye usawa,"alidai Rais Lula da Silva.

Lula ameukosoa utawala wa mtangulizi wake Bolsonaro akidai, timu yake ya mpito ilibaini fedha za umma kuvujishwa vibaya kwa maslahi ya wachache.

"Wao (utawala uliopita) walivuruga rasilimali za Wizara ya Afya. Walisambaratisha Elimu, Utamaduni, Sayansi na Teknolojia. Waliharibu ulinzi wa mazingira. Hawakuacha rasilimali kwa ajili ya chakula cha shule, chanjo au usalama wa umma,"alisema.

Pia aliituhumu Serikali ya Bolsonaro kwa kufanya mauaji ya halaiki kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo kushughulikia janga la UVIKO-19 ambalo liliua zaidi ya Wabrazil 680,000.

Rais huyo amewaambia wafuasi wake kwamba, Brazil haihitaji kukata msitu wa Amazon kwa ajili ya kilimo kama ilivyofanywa awali.
<p>Brazil’s President Luiz Inacio Lula da Silva waves to supporters on the day of his swearing-in ceremony, in Brasilia, Brazil, January 1, 2023. — Reuters</p>
Picha na Reuters.
 
Katika hafla hiyo ya uapisho, zaidi ya wawakilishi kutoka nchi 50 walikuwepo katika Bunge la Congress miongoni mwao ni Mfalme Felipe IV wa Hispania na marais wa Argentina, Bolivia, Colombia, Chile, Paraguay, Uruguay na Ureno.

Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier pia alihudhuria. Ingawa, Rais aliyemaliza muda wake Bolsonaro hakuwepo, baada ya kuondoka kwenda Florida nchini Marekani siku ya Ijumaa.

Baada ya hafla hiyo, Lula alipanda gari la kifahari la Rolls-Royce hadi Ikulu ya Planalto kuvishwa mkanda wa urais (Presidential Sash) mbele ya umati wa wafuasi 30,000 kutoka chama chake cha wafanyakazi.

Bolnsonaro alikuwa amekataa mara kwa mara kukabidhi mkanda kwa mrithi wake, kulingana na mila, na miongozo ya mataifa mengi ya Amerika ya Kusini.

Mkanda ni ishara muhimu ya mwendelezo wa urais, na huvaliwa tu na rais. Thamani yake kama ishara ya ofisi ya mkuu wa nchi inaweza kulinganishwa na ile ya taji katika mahekalu ya kifalme.

Rais anapoondoka madarakani huwa anawasilisha rasmi mkanda kwa mrithi wake ikiwa ni sehemu ya sherehe za kuapishwa rasmi.

Mikanda ya rais kwa kawaida huwa ya rangi nyingi na kubwa sana na imeundwa ikifanana na bendera ya taifa, hasa zile za marais wa Amerika Kusini.

Wakati huo huo, usalama uliimarishwa nchini kote, baada ya uchaguzi wa urais ambao ulikuwa na mvutano zaidi hususani wafuasi wa Bolsonaro waliohofiwa huenda wangezusha vurugu.

Baadhi ya wafuasi waaminifu zaidi wa Bolsonaro, ilifikia hatua wakashinikiza mapinduzi ya kijeshi yafanyike ili kumweka kiongozi huyo wa mrengo mkali wa kulia madarakani.

Kabla ya kuapishwa kwa Lula, polisi walisema walimkamata mtu aliyejaribu kuingia eneo hilo akiwa amebeba kisu na fataki.

Siku chache, mfuasi wa Bolsonaro alikamatwa kwa kutega lori lililokuwa na vilipuzi karibu na uwanja wa ndege wa Brasilia.
Lula aliongoza Brazil kutoka 2003 hadi 2010, wakati ambapo serikali yake ilipata mafanikio kutokana na utekelezaji wa programu mbalimbali za kijamii ambazo ziliwaondoa mamilioni ya watu katika lindi la umaskini.

Hata hivyo, ufisadi wakati wa utawala wa Lula ulitajwa kushamiri na pia alihukumiwa kifungo cha muda mrefu kwa ufisadi na utakatishaji fedha, ingawa hukumu hiyo ilibatilishwa baadae mwaka 2021.(Mashirika).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news