RC Amos Makalla afichua siri kuhusu Simba SC

NA DIRAMAKINI

MGENI rasmi wa Mkutano Mkuu wa Klabu ya Simba ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema mafanikio ambayo klabu hiyo imeyapata katika kipindi cha miaka minne ni makubwa na hawapaswi kuyabeza.

RC Makalla ambaye ni shabiki mkubwa wa klabu hiyo ya jijini Dar es Salaam amekumbusha miaka ya nyuma akiwa katika Kundi la Friends of Simba aliwahi kuifadhili timu kuweka kambi Tunduma ikiwa chini ya Kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kwa kuwa klabu ilikuwa haina pesa, hivyo hawapaswi kurudi huko.

Makalla amewasisitiza wanachama kuhakikisha wanachagua viongozi bora ambao watakuwa na uchu wa mafanikio na wataochaguliwa wahakikishe wanatimiza ahadi walizoweka ili timu ifanikiwe.

Pia Makalla ameupongeza uongozi kwa kumuajiri Mtendaji Mkuu wa Klabu, Imani Kajula kwa sababu anamfahamu ni mchapakazi na kumuajiri Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally.

“Ninawapongeza uongozi wa klabu kwa kupata CEO mzuri, namfahamu vizuri Kajula, hili ni jembe na litatusaidia sana pia tumepata msemaji mzuri, Ahmed Ally ‘Semaji la CAF’.

“Niwapongeze kwa mafanikio mliyopata, mlichukua ubingwa wa ligi mara nne mfululizo, kufika Robo Fainali Afrika ni jambo la kawaida kwa sasa si jambo dogo. Tusibeze mafanikio haya na lazima tumpongeze mwekezaji Mohamed Dewji ‘Mo’.

“Kuna kipindi niliifadhili timu kule Tunduma chini ya kocha Julio sasa tusirudi huko, wakati timu inaelekea Zanzibar ilibidi niongee na watu wangu kule watusaidie, lakini tumesahau hayo na tunasonga mbele,”amesema Makalla.

Post a Comment

0 Comments