Simba SC:Mashabiki tarajieni mambo mazuri

NA DIRAMAKINI

IKIWA ni siku 18 zimepita tangu Simba SC ilivyopata ushindi mnono wa mabao 7-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Uwanja Benjamin Mkapa, klabu hiyo yenye maskani yake jijini Dar es Salaam inatarajia kufanya makubwa.

Kwa mujibu wa tathimini iliyotolewa leo na klabu hiyo imeeleza kuwa, "Bado tuna kumbukumbu nzuri katika mchezo huo ambao wachezaji wetu wawili John Bocco na Saido Ntibazonkiza walifunga mabao matatu kila mmoja ‘hat trick’ na moja likifungwa na Mlinzi Shomari Kapombe.

"Hata hivyo, leo tunashuka tena katika Uwanja wa Mkapa kuikabili Mbeya City tukiwa tumetoka kushinda mechi nne za ligi kati ya tano tulizocheza mwezi Desemba huku moja tukitoka sare.

"Katika mechi hizo tano, nne tulikuwa ugenini moja ya nyumbani huku tukifanikiwa kufunga mabao 19 na kuruhusu matatu tukipata ‘clean sheet’ mbili.

"Mchezo wa leo utakuwa ni wa kwanza wa ligi katika mwaka 2023 lakini pia utakuwa wa kwanza wa Kocha Mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’ ambaye amepewa kibarua cha kukinoa kikosi chetu Desemba 31, mwaka jana.

"Mchezo huo pia utakuwa wa kwanza tangu timu irejee kutoka Dubai ilipokuwa na kambi ya siku nane ya maandalizi ya michuano iliyopo mbele yetu.

Hali ya Kikosi

"Katika mchezo wa leo tutakosa huduma ya mshambuliaji Moses Phiri aliyekuwa majeruhi na sasa amerejea kikosini lakini hayuko fiti asilimia 100 kama ilivyo kwa winga Peter Banda ambaye naye ameanza mazoezi.

"Mlinzi wa kati Henock Inonga ambaye aliumia katika mchezo wetu dhidi ya Prisons pia hatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kutokana na kuendelea kuuguza jeraha lake.

Nyota wapya kutambulishwa mbele ya mashabiki

"Wachezaji wetu wapya watatu ambao tumewasajili katika dirisha dogo la usajili tutawambulisha mbele ya mashabiki wetu watakaojitokeza Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kuanza kwa mchezo wetu.

"Kiungo Hamed Ismael Sawadogo tayari yupo jijini Dar es Salaam pamoja na mshambuliaji Mohamed Mussa huku Jean Baleke akitarajia kutua nchini mchana na anatarajia kuwepo uwanjani usiku.

Mara ya mwisho walivyokutana

"Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya tulipata sare ya kufungana bao moja, ambapo bao letu lilifungwa na Mzamiru Yassin wakati City wakisawazisha kupitia kwa Tariq Seif,"imefafanua sehemu ya tathimini ya taarifa ya Simba SC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news