VIJANA KUTOKA KAYA MASKINI WASHAURIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MAFUNZO YA UJUZI

NA MWANDISHI WETU

VIJANA kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu hapa nchini wameshauriwa kuchangamkia fursa za Mafunzo ya Kukuza na Kuendeleza Ujuzi yanayotelewa na Serikali kupitia vituo mbalimbali vya Mafunzo ya Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi.
Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA),Waziri Salum akisisitiza jambo kwa wanafunzi wanaosoma fani ya Ushoni (Ushonaji) katika Chuo cha Mafunzo ya Amali Mwanakwereke – Zanzibar.

Ushauri huo umetolewa Kisiwani Unguja - Zanzibar na Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA),Bw. Waziri Salum alipokuwa katika ziara ya siku mbili ya kutembelea wanafunzi kutoka Kaya maskini wanaosoma mafunzo ya Ujuzi kupita Mpango wa Ufadhili kwa Vijana kutoka Kaya Maskini na Wanaoishi katika Mazingira magumu.

Mkurugenzi Waziri alisema Serikali inawatambua na kuwathamini vijana hao na iko tayari kuwasidia waweze kujikwamua kiuchumi na kujihusisha katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali na uzalishaji mali aidha kwa kujiajiri wenyewe au kuajiriwa ili wajipatie kipato.
Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Waziri Salum akifurahi kazi iliyofanywa na mwanafunzi mlemavu wa miguu Rukia Haji Miraji kutoka Chuo cha Elimu Mbadala Forodhani Zanzibar.

Waziri aliweka bayana kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilizindua rasmi Mpango wa Ufadhili kwa Vijana kutoka Kaya Maskini na wanaoishi Katika Mazingira Magumu mwezi Disemba mwaka 2022 kwa lengo la kutoa Mafunzo ya Ujuzi kwa vijana 600 kutoka kaya maskini katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Aliongeza kwamba, amefarijika kuona vijana hao wanavyojituma na kuweka bidii kwenye masomo yao na kuwaasa wasikate tamaa ya kupambania kile wanachokiamini kwani watazifikia ndoto zao za kujikwamua kiuchumi na kujipatia kipato.
Wanafunzi wanaosoma fani ya uchomeleaji wa vyuma katika Chuo cha Mafunzo ya Amali Makunduchi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bw. Waziri Salum (hayupo pichani) alipowatembelea kuona maendeleo yao.

Awali Mkurugenzi Waziri alisema, wakati mafunzo hayo yanazinduliwa hawakujua kama wangepata wanafunzi wa makundi gani ila baada ya mafunzo kuanza vijana walemavu na wenye mahitaji maalum ni miongoni mwa waliopata fursa ya kusoma mafunzo hayo ya ujuzi kupitia Mpango wa Ufadhili kwa Vijana Kutoka Kaya Maskini.

“Fursa bado zipo na Serikali bado inawakumbuka, mkimalimaliza masomo jiungeni kwenye vikundi na mjisajili mfanye kazi kwa umoja ili muweze kuzifikia fursa nyingi zaidi,"alisema Waziri.
Wanafunzi wa fani ya umeme wa majumbani wakiendelea na mafunzo kwa vitendo katika Chuo cha Mafunzo ya Amali Makunduchi-Zanzibar.

Aidha Mkurugenzi Waziri alitoa ahadi ya kununua cherehani moja kwa mwanafunzi mlemavu wa miguu kutoka Chuo cha Elimu Mbadala Forodhani ambaye anatumia cherehani maalum baada kuona jinsi anavyojitahidi kusoma na kujifunza kushona licha ya ulemavu alio nao.
Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Waziri Salum akiongea na mwanafunzi mlemavu wa miguu Rukia Haji Miraji kutoka Chuo cha Elimu Mbadala Forodhani Zanzibar.

Mwanafunzi huyo Rukia Haji Miraji alimshukuru sana Mkurugenzi kwa ahadi hiyo na kusema yeye anatoka kaya maskini na hawezi kutembea kwa hiyo hata alivyochaguliwa kujiunga na masomo bado hakuwa na jinsi ya kufika darasani kwa hiyo ilimlazimu amuombe ndugu yake mtoto wa shangazi yake awe anampeleka darasani asubuhi na kumrudisha jioni.

Rukia alisema, alikuwa na mawazo sana baada ya masomo angefanyaje kazi kutokana na hali yake hivyo upatikanaji wa cherehani yake ni faraja na ni ukombozi kwake kwani ana uhakika wa kufanya kazi akimaliza masomo.
Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA),Waziri Salum (aliyekaa) katika picha ya pamoja na wanafunzi kutoka katika Chuo cha Mafunzo ya Amali Mwanakwereke - Zanzibar.

Jumla ya Vijana 600 walikusudiwa kunufaika na Mpango wa Ufadhili kwa Vijana Kutoka Kaya Maskini na Wanaoishi katika Mazingira Magumu Visiwani Unguja na Pemba na mafunzo hayo yanatolewa katika vituo 9 vya Mafunzo ya Amali visiwani humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news