Vyombo huru vya habari ni nguzo muhimu kwa umma, utawala na sekta binafsi-Sheikh Ponda

NA DIRAMAKINI

KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema, vyombo vya habari vikiwa huru, malengo ya kuanzishwa kwake yatafikiwa kwa haraka.

Ponda ameyabainisha yao leo Januari 16, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari nchini.

"Kwanza kabisa yale malengo ya kuanzishwa chombo cha habari yatakuwa yamefikiwa, bila shaka chombo cha habari kinatakiwa kuwa huru. 
 
"Pia vyombo vya habari vikiwa huru vitaaminika kwa umma, vitakuwa vinaeleza au kuwasilisha fikra za umma kwa usahihi, hivyo chombo cha habari kitaaminika kwa umma.

"Pia, vyombo vya habari huru vitasaidia sana utawala (dola) pamoja na sekta binafsi kwa sababu vitasaidia kutathmini zile shughuli zao za kila siku,"amefafanua Sheikh Ponda.

Amefafanua kuwa, vyombo huru vya habari vitaandika kuhusu uchumi, watu au matakwa ya wananchi au ukosoaji ambao unalenga kuongeza ufanisi katika ngazi mbalimbali za uwajibikaji.

"Hii ni kwa sababu chombo cha habari ni kama kioo kwa vyombo vya dola na kioo vile vile kwa sekta binafsi, kwa pamoja watakuwa na nafasi nzuri ya kuweza kujitathimi au kutathmini ule utendaji kazi wao na kuangalia kama wanakwenda vizuri,"ameongeza.

Katika hatua nyingine, Sheikh Ponda amebainisha kuwa,vyombo vya habari vikiwa huru vitasaidia katika usambazaji wa elimu mbalimbali katika jamii.

"Na vitafikisha kwa namna sahihi na pia kuyafanya mataifa ya nje kufahamu ile hadhi ya taifa na kuweza kufanya uchumi wetu uweze kufahamika vizuri, jografia ya nchi, watu wake wana hadhi gani,fursa zilizopo, hali ya kisiasa na kuleta ushirikiano mzuri baina ya mataifa ya nje na Taifa,"amesema.

Uhusiano na Demokrasia

Sheikh Ponda akizungumzia kuhusu uhusiano wa vyombo vya habari na demokrasia nchini amesema,vitu hivyo vinategemeana kwa asilimia kubwa.

"Kwanza vyombo vya habari kukiwa na demokrasia, vitakuwa hai maana yake sheria itakuwa nzuri sio zile za ukandamizaji maana yake kinyume cha demokrasia, inakuwa ni dikteta yaani mabavu.

"Kwamba watu hawapati uhuru wa kutoa mawazo, kuzungumzia na kukosoa na kadhalika kwa hiyo kama hakuna demokrasia maana yake vyombo vya habari vitakosa uhai.

"Na hii tunao mfano mzuri Zanzibar ilipata Uhuru mwaka 1963, lakini baada ya kama mwezi mmoja hivi ikawa ile Serikali imepinduliwa ikaingia Serikali ya Mapinduzi, sasa kabla ya uhuru mpaka wanapata Uhuru Zanzibar walikuwa na magazeti zaidi ya 11 ya Kiswahili, Kiingereza na ya Kiarabu yakisomwa, lakini baada ya Mapinduzi hivi vyombo vyote vya habari vilikufa. Kwa hiyo unaweza ukaona tofauti ya demokrasia na siasa nyingine kama ambavyo ilikuwa Mapinduzi.

"Pili, demokrasia inakuza uchumi wa nchi katika namna kama hiyo, hivyo vyombo vya habari vinaweza kumudu kuwa na uchumi wake wao wenyewe kwa hiyo mwandishi wa habari atakuwa na uchumi wake yeye mwenyewe, chombo chenyewe kujimudu na waandishi, kwa hiyo sio rahisi mwandishi kununuliwa akapewa hongo ili aandike yale aliyompa hongo kwa sababu yeye mwenyewe ana uchumi mzuri.

"Pia, wao wenyewe wanaweza kuanzisha vyuo kwa ajili ya kuandaa wanahabari na pia demokrasia inasaidia katika kumuwezesha hata mtawala mwenyewe yaani ana nafasi nzuri ya kuvitumia kuweza kueleza mambo yenye manufaa ya kitaifa kwa wananchi wa kawaida, kwa maana hiyo hata utawala wenyewe unanufaika kutokana na uhuru wa vyombo vya habari,"amefafanua kwa kina Sheikh Ponda.

Wakati huo huo, Sheikh Ponda amebainisha kuwa, "La tatu, ni chachu ya amani katika nchi, vile vyombo vya habari vinaweza kusaidia sana kuwepo kwa hiyo demokrasia kunakuwa na uhuru na kwa vile kunakuwa kuna uhuru watu hawataweza kuwa na mtazamo wowote ule wa kimapambano, kwa sababu wanaweza kutoa yale maoni yao na mambo yao yanakwenda vizuri zaidi. Kwa hiyo kuna uhusiano mkubuwa sana kati ya demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari."

Mbali na hayo, Sheikh Ponda amesema kuwa, kama angekutana na kiongozi wa juu angemshauri mambo kadhaa kuhusiana na vyombo vya habari.

"Kumekuwa na lugha ambayo inatumika kwenye vyombo vya dola, wanatumia lugha kwamba sisi hatufanyi kazi kwa kusikiliza vyombo vya habari, hii mara nyingi imekuwa inatumika, kuna jambo zito na jamii au mhusika anarejesha hilo jambo, mhusika anatoa rejea ya chombo cha habari, basi mara nyingi viongozi wa dola huwa wana lugha kama hiyo kuonesha kwamba sisi hatufanyi kazi kwa kuzingatia vyombo vya habari.

"Kwa hiyo mimi kama ningekutana na kiongozi wa juu ningemshauri kwamba vyombo vya habari visitazamwe hivyo, bali viongozi wavitazame vyombo vya habari katika ujenzi wa taifa ambalo ni huru, lenye utawala bora, utawala wa haki. Kwa hivyo vyombo vya habari vina nafasi kubwa.

"Ni muhimu sana vikaangaliwa kama ni nyenzo muhimu sana katika taifa huru na kutenda haki.Vile vile ningemshauri kuhakikisha kwamba anaweka msingi imara wa sheria ili hii tasnia ya habari iepukane na sheria zinazopunguza uwezo wao wa kufanya kazi kwa maana ya sheria kandamizi, ili kuhakikisha kwamba hiyo sekta ya habari inapumua kutoka kwenye hayo mazingira ambayo yamejitokeza katika maeneo mengi,"amefafanua kwa kina Shekh Ponda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news