Wapongezwa kwa kupiga hatua katika elimu

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango amesema, Mkoa wa Dodoma wamepiga hatua kubwa kwenye ufaulu nchini.

Hayo yamesemwa leo Januari 20, 2023 kupitia hotuba ya Makamu wa Rais iliyosomwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe.Angellah Kairuki (Mb) katika hafla ya kuufahamisha umma mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Mkoa wa Dodoma.

"Katika eneo la elimu, Mkoa wa Dodoma mmepiga hatua kubwa kwenye ufaulu. Taarifa za Baraza la Mitihani kuhusu ufaulu wa darasa la saba, zinaonesha kuwa Mkoa wa Dodoma uko katika kumi bora kwa ufaulu kitaifa na kwa mara ya kwanza Halmashauri ya Wilaya Bahi imeingia katika halmshauri kumi bora kitaifa.

"Nisisitize kuwa, Mkoa wa Dodoma una nafasi ya kufanya vizuri zaidi. Tuhamasishe upatikanaji wa chakula mashuleni ili wanafunzi wetu watulie na kusoma vizuri,"amesema.

Pia ametaka walimu kupewa ushirikiano, kwani wanafanya kazi kubwa ya kuliandaa taifa la kesho na kuwapa motisha kila wanapofanya vizuri.

"Motisha wapewe sio kwa wale wanaofanya vizuri kitaifa tu, bali hata wale wanaofanya vizuri kimkoa, kiwilaya, na hata katika kata. Serikali itaendelea kuwekakipaumbele cha juu kwa sekta ya Elimu ili watoto wetu wawe Watanzania bora wanaoipenda nchi yao.

"Hapa, nitoe wito kwa kila mzazi kuhakikisha watoto wanaoingia darasa la awali, darasa la kwanza, na kidato cha kwanza wanaripoti shuleni,"amesema Waziri Kairuki kwa niaba ya Makamu wa Rais.

Amesema, Serikali imefanya jitihada kubwa kuboresha miundombinu ya elimu na kuajiri waalimu kwa kiasi kikubwa. "Furaha ya Mheshimiwa Rais wetu ni kuona kila mtoto anaypaswa kusoma yuko shuleni, darasani.

"Tukitekeleza hilo, tutakuwa tumempatia Mhe.Rais malipo tuliyopaswa kumlipa. Niwasihi pia wazazi wote, washiriki katika mikakati mbalimbali na program za kuboresha elimu katika mikoa yenu.

"Ninawata viongozi wa mkoa kutumia fursa ya uwepo wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu vilivyoko katika mkoa wa Dodoma kuboresha huduma za kufundisha watoto wetu,"amesisitiza Makamu wa Rais kupitia hotuba iliyosomwa na Waziri Kairuki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news