Waziri Dkt.Tax ateta na wageni mbalimbali wa Kimataifa

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Januari 9,2023 amekutana kwa mazungumzo kwa nyakati tofauti na wageni mbalimbali waliomtembelea ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma

Wageni hao ni Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), Bi. Mahoua Parums; Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Bianadamu na Watu, Mhe. Jaji Iman Aboud na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF), Bi. Shalini Bahuguna.
Akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Dkt. Tax amempongeza Mhe. Balozi Nabil Hajlaoui kwa hatua ya Ubalozi huo kufungua ofisi jijini Dodoma ikiwa ni ishara ya Ufaransa katika kuuunga mkono harakati za Serikali ya Tanzania za kuimarisha makao makuu ya nchi Dodoma.

“Mhe. Balozi nchi zetu zimekuwa na uhusiano wa kirafiki uliodumu tangu Tanzania ilipopata uhuru wake, na tumeendelea kuungana mkono katika ngazi ya nchi na hata kimataifa, na kwa hili mnalolifanya hapa Dodoma linadhihirisha kuimarika kwa ushirikiano wetu,” alisema Dkt. Tax.

Akizungumza katika kikao hicho Balozi wa Ufaransa alisema nchi yake imeamua kufungua ofisi ya ubalozi jijini Dodoma kama njia mojawapo ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Ufaransa pamoja kuunga mkono hatua ya Serikali ya kuhamishia makao makuu yake jijini humo.

Ameongeza kusema mwezi Juni 2023 Ufaransa inatarajia kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Paris hadi Dar es Salaam kupitia Zanzibar. Itakumbukwa kuwa mwaka 2021 Shirika hilo lilianzisha safari zake Zanzibar kupitia Nairobi, Kenya.

Amesema kuanzishwa kwa safari hizo za moja kwa moja zitawawezesha watalii kutoka Ufaransa kuja moja kwa moja nchini na hivyo kupunguza urefu wa safari na hivyo kufanya watalii na wafanybiashara wengi kuja kuangalia fursa na kutembelea vivutio vya utalii nchini kwa urahisi.

Mhe. Balozi pia amesema Ubalozi pia utaendeloea kutoa mafunzo ya lugha ya kifaransa kwa watumishi wa umma ambapo ikwa kuanzia wanaendelea na mafunzo hayo kwa watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Ulinzi na katika Chuo cha Idara ya Uhamiaji mjini Moshi.

Mhe. Balozi pia ameongelea nia ya nchi yake kuunganisha nguvu na Tanzania katika sekta ya nishati mbadala ili kuiwezesha Tanzania kujitosheleza na nishati hiyo nchini na hivyo kukuza uchumi wake.
Katika mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), Bi. Mahoua Parums, Mhe. Dkt. Tax amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Shirika hilo katika zoezi linaloendelea la kuwarejesha kwa hiari wakimbizi kwenye nchi zao za asili.

Kwa upande wake, Bi. Parums ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuhifadhi wakimbizi licha ya changamoto mbalimbali zilizopo. Amesema Shirika lake linathamini mchango huo wa kibinadamu wa Tanzania kwa wakimbizi hao na kwamba litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwarejesha kwa hiari wakimbizi wa Burundi.
Akizungumza na Mhe. Jaji Iman wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Bianadamu na Watu, Mhe. Dkt. Tax amesema Serikali ya Tanzania kama mwenyeji wa Mahakama hiyo iliyopo Arusha itaendelea kutekeleza makubaliano ya mkataba wa uenyeji kama ulivyoainisha.

Naye Jaji Iman amemhakikishia ushirikiano Dkt. Tax na kwamba wanaipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza makubaliano ya mkataba wa uenyeji ambapo hadi sasa Mahakama hiyo imepatiwa eneo la ukubwa wa ekari 25 kwa ajili ya kujenga ofisi zake za kudumu jijini Arusha.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa UNICEF nchini ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kusimamia na kutekeleza kikamilifu mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayohusu masuala ya haki za watoto ikiwemo afya, elimu na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF), Bi. Shalini Bahuguna alipomtembelea ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma, Januari 9,2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news