Waziri Mkuu atoa maagizo ujenzi Shule ya wasichana Dkt.Samia Suluhu Hassan

NA OR TAMISEMI

WAZIRI Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wakandarasi wanaojenga Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan iliyopo Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa ili waanze kupokea wanafunzi.

Ametoa agizo hilo Januari 6, 2023 mara baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo inayotarajia kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano Julai, 2023.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa,Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameamua kuwekeza kwenye elimu ya mtoto wa kike kwa kujenga shule za wasichana nchi nzima ili kumpunguzia changamoto zilizokuwa zikimkabili. “Si kwamba amemtenga mtoto wa kiume hapana, ameamua kwenda nao wote.”

Mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili kwa gharama ya shilingi bilioni 4 kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), awamu ya kwanza ilianza Aprili 2022 na inatarajiwa kukamilika Januari 30, 2023 ambayo itagharimu shilingi bilioni tatu. Shule hiyo itakapokamilila itapokea wanafunzi 1,080 ambapo awamu ya kwanza itapokea wanafunzi 600.

Aidha, awamu ya kwanza imehusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo mabweni matano, bwalo, vyumba 12 vya madarasa, jengo la utawala, nyumba ya mwalimu, mfumo wa maji safi na maji taka, vyoo matundu 16, uzio, kichomea taka, chumba cha jenereta na njia za kutembelea.

Pia, awamu ya pili ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni moja itahusisha ujenzi wa madarasa 10 yenye ofisi za walimu tatu, chumba cha ICT, Maktaba, nyumba nne za walimu na mabweni manne.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news