Wizara yatoa maagizo NEMC

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Chilo ameliagiza Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kuomba fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi uliopo katika Kijiji cha Ntoba, Kata ya Ndala,wilaya ya Nzega, mkoani Tabora ambao kukamilika kwake kutawaondolea adha ya uhaba wa maji wafugaji na wakulima wa eneo hilo.
Ametoa agizo hilo leo,wilayani Nzega wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi baada ya kutembelea mradi huo ambao unajumuisha miradi mingine kama hiyo katika wilaya ya Bahi na Kongwa,mkoani Dodoma ambapo miradi hiyo kwa ujumla inagharimu Shilingi Bilioni Tatu.

“Tunawaomba wenzetu wa NEMC wanaosimamia mradi huu sasa waanze utaratibu wa kuomba fedha ili wakamilishe mradi huu na uanze kutumika kwa wananchi kama ilivyokusudiwa,mradi huu umekusudiwa wananchi wautumie na waweze kunufaika nao kwa shughuli za kilimo,mifugo na shughuli nyuingine,kwahiyo watoke wakaombe ili wakamilishe mradi huu na maeneo yote ya mabwawa yanayojumuisha mabwawa yaliyopo wilayani Bahi na Kongwa,mkoani Dodoma,” alisema

Akizungumza kwa niaba ya serikali ya wilaya,Kaimu Katibu Tawala wa wilaya ya Nzega alielezea mkakati wa kutunza mazingira huku akiweka wazi kampeni ya kila mtoto anaezaliwa katika wilaya hiyo kupandiwa mti mmoja na wazazi wake ili kuweza kuhifadhi mazingira na mtoto huyo akikua akute mazingira yakiwa salama.

“Mheshimiwa Naibu Waziri sisi kama serikali ya wilaya tuna kampeni maalumu ambayo ni endelevu tukimtaka kila mzazi wa mtoto anaezaliwa kupanda mti kwa kila mtoto anaemzaa ili tuweze kuhifadhi mazingira yetu maana bila kuweka mikakati basi vizazi vijavyo vitakuta jangwa tu,kwahiyo hiyo ni kampeni ya mkoa mzima wa Tabora na tunashukuru inaenda vizuri,”alisema

Miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii za wakulima na wafugaji katika wilaya ya Kongwa,Bahi na Nzega ilizinduliwa rasmi mwaka 2021 huku ikitarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mwaka 2024 huku gharama ya miradi hiyo ikitolewa na wahisani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news