Zanzibar yadhamiria kuimarisha usafi

NA DIRAMAKINI

KATIBU wa Kikosi Kazi cha Utekelezaji wa Mpango wa Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar (ZACCEP) ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatibu Makame amewataka watendaji kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Hayo ameyaeleza huko katika Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Maruhubi alipokuwa akizungumza na wajumbe wa kikao kazi cha Mpango wa Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya miezi mitatu Oktoba hadi Desemba, 2022.

Amesema, kila mjumbe anayewakilisha taasisi yake iliyopo kwenye mpango huo ni vyema kusimamia utekelezaji wa majukumu na kuwasilisha ripoti ili kuonyesha maendeleo na changamoto zilizopo.

Katibu huyo alisema,iwapo wajumbe hao watafanya kazi kwa ushirikiano na bidii kutasaidia kufikia malengo yaliyotarajiwa kuliko kufanya kazi kwa mazoea.

Alieleza kuwa, bado kumekuwa na mazingira machafu katika baadhi ya maeneo mbalimbali ya Zanzibar jambo ambalo ni hatarishi kwa kusababisha mlipuko wa maradhi ya kipindupindu,hivyo aliagiza taasisi husika kuchukua hatua stahiki kusimamia

"Kwani hatuwezi kudhibiti taka ikawa mfano kama Arusha na Moshi isiwe kila siku sisi tunakwenda kujifunza kwao,"alisema Katibu huyo.

Naye Mratibu wa Mpango wa Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar, Makame Ame Simai ameeleza changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye utekelezaji wa mpango wa kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambao ulitekelezwa na taasisi mbalimbali zilizopo katika mpango.

Alisema, changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango huo ni kukauka kwa visima 32 vilivyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa wakati wa kiangazi pamoja na kukosekana kwa gari la kusafirishia maji taka hasa kwa upande wa Pemba na sehemu husika ya kumwagia maji hayo.

Mjumbe kutoka Manispaa ya Magharibi ‘B’, Yussuf Mati Ali amesema wameondoa majaa mbalimbali ambayo sio rasmi katika maeneo ya kivigo Mwanakwerekwe, Taveta,Magirisi pamoja na Magereza na kusafisha mitaro ya Kombeni, Mazizini na Mwanakwerekwe.

Pia wamefanya ukaguzi kwa wafanyabiashara wa migahawa 83 na mamalishe 50 kwa upande wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ na baadhi walifungiwa na wengine kupigwa faini ya papo kwa papo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news