NA MWANDISHI WETU
JUKUMU la kuzuia vitendo vya kihalifu na maovu katika jamii linapaswa kufanywa na kila mtu katika eneo lake badala ya kuliachia Jeshi la Polisi peke yake kama watu wengi wanavyofanya.
Wakili wa Serikali mwandamizi kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar Hamisa Mmanga, aliyasema hayo huko Fuoni Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akiwasilisha mada katika ziara za kutoa elimu ya kisheria kwa jamii (outreach program) ikiwa ni mwendelezo wa shamra shamra za Wiki ya Sheria Zanzibar ambayo kilele chake ni Februari 13, mwaka huu.
Amesema kushamiri kwa maovu katika jamii kama vile biashara na matumizi ya Madawa ya kulevya, udhalilishaji au migogoro ya ardhi huchangiwa kwa kiasi kikubwa na tabia ya muhali iliyojengeka kwa watu wengi na hivyo kushindwa kuwafichua watendaji wa maovu katika jamii.
Amesema ni vyema pale inapotokea ishara tu ya jambo ovu lolote wananchi wanapaswa kutoa taarifa badala ya kukaa kimya kwa kuogopa kuonekana mbaya na watendaji wa makosa hayo.
“Chukulia mfano mtaani kwenu wamekuja watu wasioeleweka, wakaanza kuvuta Bangi au madawa yoyote, wewe ukakaa kimya, au mwanafamilia ametenda kosa ukaendelea kukaa kimya, tambua kuwa unatengeneza mazingira ya kufanyika makosa zaidi. Ikiwa utaenda kupeleka Taarifa kwa Sheha au Polisi itakuwa umesaidia kuiepusha jamii kuharibika dhidi ya makosa ambayo yangefanywa zaidi na muhusika,” amesema Wakili Hamisa.
Mmoja wa wakaazi hao wa Fuoni Bi Salma Ali alitaka kujua sababu zinazopelekea kukamatwa wasambazaji na watumiaji Madawa ya kulevya kuwa ni vijana wadogo masikini, wakati wafanyabiashara wakubwa wa Madawa ya kulevya wanafahamika bila kuchukuliwa hatua.
Amesema wananchi wengi wana hamu ya kuona wafanyabiashara wakubwa wa Madawa ya kulevya wanaotoa dawa hizo nje ya nchi wakitiwa hatiani na kupewa adhabu, badala ya kila siku kuonekana vijana wadogo watumiaji peke yao ndio wanaotiwa hatiani.
“Kila siku tunaona na kusikia wanaokamatwa ni watoto wetu wadogo wanaotumia Unga lakini hayo Mapapa yanayofanya biashara na kutuletea hapa hatuyaoni kufungwa wala kukamatwa, na yanajulikana mambo haya vipi,”aliuliza Bi Salma.
Ameongeza kuwa kma kuna mwananchi yeyote mwenye taarifa ya wafanyabiashara Wakubwa na wadogo anapaswa kulijulisha Jeshi la Polisi ili lifanye kazi yake.
“Sisi tunataka hao wanaojulikana Mapapa wa Madawa ya kulevya waripotiwe katika Jeshi la Polisi. Uzuri zaidi ni kwamba Jeshi linatunza siri ya mtoa taarifa. Wala mwananchi aliyetoa taarifa hiyo hatoitwa mahakamani,”alifafanua Wakili Issa.
Katika kuonesha ushirikiano thabiti wametoa namba za simu kwa wananchi hao kuwapigia muda wote kunapokuwa na tukio au viashiria vyovyote vya uhalifu kama Madawa ya kulevya, udhalilishaji au hata migogoro ambayo huleta tafrani katika jamii.
Ziara hiyo iliyoandaliwa na Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar kwa kushirikiana na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ilikuwa na lengo la kuwafahamisha wananchi sheria kama njia moja wapo ya kusaidia kupunguza migogoro ikiwemo ya Ardhi, vitendo vya udhalilishaji, madawa ya kulevya na uhalifu katika jamii.