AJE KULA MAHARAGE

NA LWAGA MWAMBANDE

KUFUATIA kuadhimishwa kwa mafanikio makubwa kwa Siku ya Kimataifa ya Mikunde kwa mwaka 2016, kila tarehe 10 Februari, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) huadhimisha Siku ya Kunde Duniani.

FAO inataja jamii ya kunde kuwa ni maharage, kunde, mbaazi, njegere na njugu mawe ambapo kwa mwaka huu wa 2023 kauli mbiu ilikuwa ni 'Mikunde kwa Mustakabali Endelevu'.

Kwa mujibu wa shirika hilo, kauli mbiu ya mwaka huu inaangazia jinsi jamii ya kunde zinavyoongeza ustahimilivu wa mifumo ya kilimo na kuboresha maisha kutokana na kiwango chao cha maji kidogo, kustahimili ukame na upinzani dhidi ya majanga yanayohusiana na hali ya hewa.

Pia inaangazia sekta ya kunde duniani, na jinsi inavyoweza kuwa kichocheo chanya katika kuhakikisha uthabiti wa minyororo ya ugavi ya kikanda na kimataifa, kuwezesha watumiaji kupata vyakula vyenye lishe bora, na kuchangia matumizi endelevu ya maliasili katika uzalishaji wa mapigo ya moyo.

"Kunde huchangia kwa njia mbalimbali kuelekea mabadiliko ya mifumo yetu ya chakula, na inaweza kutusaidia kushughulikia matatizo mengi ya kiafya na kimataifa, Kunde zinaweza kuchangia kuongeza uimara wa mifumo ya kilimo na kusaidia kuboresha bioanuwai ya udongo," alikaririwa Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu.

Miongoni mwa faida za kula vyakula jamii ya kunde ikiwemo maharage ni kupata virutubisho kama protini, vitamini B, A na K madini ya shaba, chuma, na manganese.

Pia, vyakula hivyo husaidia kushusha sukari na kuboresha kiwango cha insulini, hupunguza uwezekano wa kupata kisukari,hupunguza cholesterol mbaya mwilini, husaidia katika kupunguza uzito, husaidia hatari ya kupata saratani, hupunguza uwezekano wa kupata presha na uboresha afya ya mifupa.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kwa manufaa hayo tele, yafaa tuhimizane kula vyakula vya jamii ya kunde kwa wingi kwa afya bora. Endelea;


1. Alika mtu mzima, apate chakula chema,
Afya yake iwe njema, hata aweze kulima,
Magonjwa yaweze koma, yale yanavumavuma,
Aje kula maharage, wala siyo nyama choma.

2. Mialiko ukisoma, mingi ni ya nyama choma,
Kotekote inavuma, Dasalamu na Dodoma,
Wasomi tunawasoma, hiyo wasema si njema,
Aje kula maharage, wala siyo nyama choma.

3. Tena ile nyama choma, nyama nyekundu ni noma,
Ndivyo hao wanasema, na maneno yanavuma,
Lakini hivi twasema, mialiko yazizima,
Aje kula maharage, wala siyo nyama choma.

4. Maharage wanasema, mwilini yafanya vema,
Mimea haina homa, kama kulakula nyama,
Kuitumia ni vyema, hata mialiko vema,
Aje kula maharage, wala siyo nyama choma.

5. Uliko huko nasema, njoo tule kile chema,
Maharage yako vema, afya haiwezi goma,
Takwenda kwa kusimama, cheche zako ukitema,
Aje kula maharage, wala siyo nyama choma.

6. Vyakula wanavisema, mwilini kuleta homa,
Tena hiyo nyama choma, nayo waisemasema,
Ipo kutoiva vema, kuleta mwili kuuma,
Aje kula maharage, wala siyo nyama choma.

7. Mbogamboga pia njema, magonjwa unasukuma,
Kinga mwili yawa njema, hakuna kukusakama,
Lishe kamili ni vema, mtoto mtu mzima,
Aje kula maharage, wala siyo nyama choma.

8. Kazi kumeng’enya nyama, tumbo laweza kugoma,
Kazi inaposimama, mtu wawa wimawima,
Pakiwa na lishe njema, hayo hatuwezi sema,
Aje kula maharage, wala siyo nyama choma.

9. Mara mojamoja nyama, kutafuta nayo njema,
Kidogo kwa wingi homa, mwilini ni uhasama,
Tule kwa kiasi nyama, japo utamu wavuma,
Aje kula maharage, wala siyo nyama choma.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news