MAPENZI:Upendo utawale

NA LWAGA MWAMBANDE

UKISOMA Biblia Takatifu katika kitabu cha Marko12:29-31, inasema upendo ni “amri ya kwanza”. Katika kitabu cha Mathayo 22:36-40 Biblia inasema upendo ni “amri kuu”. Tunaona upendo ni kitu cha msingi sana katika maisha yetu ya Ukristo na haya tunayoishi kila siku hapa duniani.

Picha na familyandmedia.

Biblia inasema “upendo ni Mungu” 1Yoh.4:8b; 16. Biblia inaendelea kusema katika upendo Mungu anakaa ndani yetu nasi ndani yake. Mungu anakaa ndani yetu katika Roho mtakatifu (1Yoh.3:24). Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi.(1Petro 4:8).

Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi. (Yohana 13:34-35).

Kwa msingi huo, kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote. (Mithali 10:12). Wapenzi ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. (1Yohana 4.11). 
 
Ukitafakari kwa kina kuhusu mistari hiyo ya Biblia hapo juu utaona namna ambavyo upendo una nguvu na ni muhimu katika maisha yetu ya kila siku. Kwa kuliona hilo, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,acha upendo utawale kwetu. Endelea;

1.Mapenzi ni kupendana,
Na tena ni kushibana,
Mapenzi ni kubebana,
Pia kushirikiana.

2.Mapenzi si kuzozana,
Wala siyo kugombana,
Mapenzi si kusigana,
Pia siyo kupigana.

3.Mapenzi kuongozana,
Tena na kukumbukana,
Mapenzi tembeleana,
Tena kutanakutana.

4.Mapenzi kujaliana,
Na tena kuinuana,
Mapenzi kutafutana,
Pia kuchukuliana.

5.Mapenzi kushangazana,
Pia kuzawadiana,
Mapenzi kualikana,
Kwa chakula cha mchana.

6.Mapenzi ni kukopana,
Na pia kugongeana,
Mapenzi kukumbushana,
Mambo kubadilishana.

7.Mapenzi sabahiana,
Na pia kuchekeshana,
Mapenzi kuridhishana,
Na wala si kutegana.

8.Mapenzi ni kungojana,
Pia kuvumiliana,
Mapenzi si kutengana,
Wala si kuumizana.

9.Mapenzi shereheshana,
Na glasi gongeana,
Mapenzi kutulizana,
Mazuri kufundishana.

10.Mapenzi ni kupeana,
Wala siyo kunyimana,
Mapenzi changamshana,
Wala si kununiana.

11.Mapenzi jadiliana,
Na kuzidi elewana,
Mapenzi ni kujengana,
Wala si kubomoana.

12.Mapenzi pendeleana,
Mlivyonavyo gawana,
Wala si kupumbazana,
Wala si kufukuzana.

13.Mapenzi kusifiana,
Wala si kushushuana,
Mapenzi ni kuungana,
Wala siyo kutengana.

14.Mapenzi shirikishana,
Wala si kukamuana,
Mapenzi pamoja vuna,
Na heshima tunziana.

15.Mapenzi sameheana,
Siyo kushitakiana,
Mapenzi bembelezana,
Wala si kufokeana.

16.Mapenzi kuchekeshana,
Na pia kutaniana,
Mapenzi kukimbizana,
Na mikono kushikana.

17.Mapenzi kumbatiana,
Na wenyewe busiana,
Mapenzi moyo tiana,
Na siyo kuangushana.

18.Mapenzi ni kujuana,
Wala si kutambiana,
Mapenzi furahishana,
Wala si kununiana.

19.Mapenzi ni dhana pana,
Ukiyapata wanona,
Mapenzi sogeleana,
Wala si kukimbizana.

20.Mapenzi ni kuuguzana,
Na pia ni kuponyana,
Si magonjwa kupeana,
Au hata kufishana.

21.Mapenzi kupotezana,
Na mikuki kuchomana,
Ni uuaji nauna,
Hapo tuseme hapana.

22.Mapenzi anayo Bwana,
Msalaba twauona,
Hakutaka kubishana,
Ili tuweze kupona.

23.Petro alimuona,
Wakati akipigana,
Sikio chini kaona,
Hakutaka kupigana.

24.Petro alimuona,
Wakati anamkana,
Na yeye hakumkana,
Wakazidi kupatana.

25.Pendo la Mungu twaona,
Achelewa kutuvuna,
Japo tunavyojiona,
Tunakwenda twajivuna.

26.Mapenzi tuweze ona,
Na Mungu ya kufanana,
Nasi budi kupendana,
Amani tutaiona.

27.Tuache kuumizana,
Na wenyewe kukwazana,
Hapo tutamalizana,
Amani hatutaona.

28.Mapenzi ni kupendana,
Mapenzi shangiliana,
Mapenzi shikwa shikana,
Furaha tutaiona.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news