Al Hilal dhidi ya Simba SC leo ni kama Ligi ya Mabingwa wa Afrika

NA DIRAMAKINI

KOCHA Msaidizi wa Simba SC, Juma Mgunda amesema mchezo wa leo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal utakuwa kipimo kizuri kwao kuelekea mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya itakayopigwa Februari 11, 2023.

Mgunda amesema, Al Hilal ni moja ya timu bora barani Afrika ambapo itawapa mwanga wa hali ya ubora wa kikosi chao kuelekea mchezo wa Horoya.

Mgunda ameongeza kuwa, hata Al Hilal watapata maandalizi mazuri kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mamelodi Sundowns kwa kuwa wanakutana na timu bora.

“Al Hilal ni timu nzuri barani Afrika, tunategemea itakuwa kipimo kizuri kwetu kuelekea mchezo dhidi ya Horoya. Tumetoka kucheza mechi ya ligi na kikosi kimefanya mazoezi, tayari kwa mechi, niwatoe hofu Wanasimba kuwa tuna kikosi kipana na wachezaji ambao walikuwa majeruhi kwa muda mrefu tunategemea kuwatumia,” amesema Mgunda.

Kwa upande wake kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge amesema mchezo wa leo utakuwa ni kama wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa anaenda kukutana na timu bora zaidi.

Ibenge amesema anatamani Simba kuwa bora katika mchezo wa huu ili apate kuona mapungufu ya kikosi chake kabla ya kukutana na Mamelodi.

“Mchezo utakuwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, tunakutana na Simba timu imara zaidi. Itatupa mazoezi mazuri na kipimo.

“Tumekuwa na wiki nzuri ya maandalizi hapa Tanzania kabla ya kuelekea Afrika Kusini, ni matarajio yetu tutafanya vizuri,”amesema Ibenge.

Post a Comment

0 Comments