CHUO CHA VETA CHA NYAMIDAHO KILICHOPO KATIKA HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU CHAKOSA WANAFUNZI

NA RESPICE SWETU

IMEFAHAMIKA kuwa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) cha Nyamidaho kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, hakina wanafunzi wa kutosha.

Hayo yamebainika wakati wa kikao cha wadau wa elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Kasulu wiki iliyopita.

Akichangia wakati wa mjadala wa kikao hicho, Mkuu wa Chuo cha Ufundi VETA cha Nyamidaho, Hamenya Ntabaye alisema kuwa, chuo hicho kilichojengwa kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho kujitegemea mara baada ya kuhitimu mafunzo yao, kina upungufu mkubwa wa wanafunzi ikilinganishwa na nafasi zilizopo.
Akizungumza kwa uchungu kuhusu hali hiyo, mkuu wa chuo hicho (mwenye karatasi mkononi) amesema, pamoja na kuwepo kwa mabweni maalumu yaliyoandaliwa kwa ajili ya wanafunzi wa kike, hakuna mwanachuo wa kike hata mmoja aliyepo katika mabweni hayo.

Kupitia kikao hicho, wadau wa elimu Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, wameweka maazimio mbalimbali likiwemo la kuwahamasisha wakazi wa eneo hilo na jamii nzima kupeleka watoto wao kwenye chuo hicho.

Awali katika kikao hicho, wajumbe walipokea taarifa ya Sekta ya Elimu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu iliyosheheni mafanikio lukuki yaliyotokea katika kipindi cha miaka miwili.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari, uboreshwaji wa miundombinu na kupanda kwa kiwango cha ufaulu hususan katika mtihani wa kumaliza kidato cha sita ambapo kwenye mtihani huo, Shule ya Sekondari ya Kasangezi iliyopo kwenye halmashauri hiyo imefanya vizuri na kuwa ya kwanza kimkoa.

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa Shule 5 za msingi na 4 za Sekondari katika kipindi cha mwaka 2020 na 2022.

Sanjari na mafanikio hayo, taarifa hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa idara ya elimu msingi na sekondari, ilizibainisha pia changamoto zilizopo kwenye idara hizo kuwa ni pamoja na upungufu mkubwa wa walimu ambapo idara ya elimu awali na msingi yenye mahitaji ya walimu 2136 inao walimu 859 tu sawa na upungufu wa walimu 1277.

Kwa upande wake, idara ya elimu ya sekondari yenye mahitaji ya walimu 436, ina jumla ya walimu 310 ikiwa na upungufu wa walimu 126.

Kikao hicho kilitumika pia kutoa tuzo na zawadi kwa shule na walimu waliofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa upimaji wa darasa la nne, mtihani wa kuhitimu darasa la saba na kidato cha sita huku wadau wa elimu wakipewa vyeti kutambua mchango wao.

Akiahirisha kikao hicho, mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu amewataka wakazi wa halmashauri ya walaya ya Kasulu kushirikiana na serikali katika kuinua kiwango cha elimu na kufuata maagizo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa likiwemo la chakula cha wanafunzi shuleni.

"Maagizo hayo ni ya serikali na mimi nikitamka maana yake imetamka serikali haijalishi nitakuwa nimeyatoa kwa mdomo au kwa maandishi ni lazima yaheshimiwe,"amesisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news