HAKI:Inaziba zote nyufa

NA LWAGA MWAMBANDE

UKISOMA Biblia Takatifu kitabu cha Mithali 14:34 utaona neno la Mungu linasisitiza kuwa, "Haki huinua taifa, bali dhambi ni aibu kwa watu wote."

Neno hilo fupi limebeba ujumbe mkubwa wenye thamani ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo kwa ustawi bora wa Taifa lolote duniani na Dunia kwa ujumla.

Neno haki kwa tafsiri ya kamusi ya Kiswahili sanifu lina maana ya jambo ambalo mtu anastahiki au kitu anachostahili kuwa nacho katika maisha yake.

Kwa tafsiri ya kamusi ya kisheria neno haki lina maana kile mtu anachostahili kuwa nacho au kile anachoruhusiwa kufanya, au kile anachostahili kupokea kutoka kwa wengine kwa mujibu wa sheria.

Aidha, kwa tafsiri hii tunaweza kuona kuwa sheria ndio msingi wa haki, sheria ndio inasema kile unachostahili kuwa nacho au unachoruhusiwa kufanya au unachotakiwa kupata kutoka kwa wengine. Kwa maana pana zaidi tunaweza kusema haki ni maslahi ya mtu ambayo yanatambuliwa na kulindwa na sheria.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande kwa msingi huo anasisitiza kuwa, kila mtu anawajibika kutenda haki mahali alipo, tunapaswa kuwatendea haki tunaoishi nao, tunaowaongoza, na tunaokutana nao popote tunapokuwa. Endelea;

1. Haki
Inainua taifa,
Inaziba zote nyufa,
Kuongeza maarifa,
Haiwajali washefa.

2. Haki,
Wa kufa lazima kufa,
Rufaa hata kwa lofa,
Majibu kwake ni dhifa.

3. Haki,
Siyo kama kwa Kayafa,
Mwenye haki kwenda kufa,
Mhalifu ale sifa.

4. Haki,
Hata dhiki yote hufa,
Bila pigo la kifafa,
Pesa wala siyo sifa.

5. Haki,
Tafuta upate sifa,
Baraka toka tarafa,
Kufika hadi taifa.

6. Haki,
Hufa wapasao kufa,
Hata na zao nyadhifa,
Siyo kwa kuwa malofa.

7. Haki,
Mahakama ina sifa,
Dhulumati inakufa,
Sheria kama za refa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news