JE UNATAMBUA HILI?

NA ADELADIUS MAKWEGA

PICHA unayoiona hapa chini, msomaji wangu inawaonesha Waziri wa Utamaduni, Sanaa, na Michezo nchini Tanzania, Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana (katika), Mhe. Pauline Gekul, Naibu Waziri (kulia) na ndugu Saidi Otumani Yakubu (kushoto) Katibu Mkuu, muda mfupi baada ya Waziri na Katibu Mkuu kula kiapo Ikulu ya Dar es Salaam siku ya Februari 15, 2023.
Mwanakwetu anakuletea tafakari ya picha hiyo, lakini kwanza ni vizuri ulifahamu jambo moja juu ya wizara wanayofanyia kazi viongozi hao, mpaka saa tangu uhuru imebahatika kuwa na Manaibu Waziri kadhaa, kulingana na taarifa ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Iliyokuwa Tanganyika iliyotolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ndugu Sethi Kamuhanda Disemba 9, 2011 ukurasa wake wa 17 na 18 inayataja majina kadhaa yaliyoshika nafasi hiyo kwa kipindi tofauti: Mhe. Daniel Nicodemes Nsanzungwanko, Mhe. Mudhihir Mudhihi, Mhe. Joel Bendera, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi, Mhe. Dkt. Makongoro Mahanga, Mhe. Dkt, Fenella Mukangara, Mhe. Juma Nkamia, Mhe. Annastazia Mabula, Mhe. Juliana Shonza na sasa ni dada yetu mpendwa Bi Pauline Gekul.

Ukitazama kwa umakini jina la Mhe. Dkt. Fenella Mukangara linaonekana kwa waliwahi kuwa Manaibu na baadaye katika Mawaziri.

Katika orodha za viongozi hao mwanakwetu pia amekutana na orodha ya waliowahi kuwa Makatibu Wakuu tangu uhuru nao ni Ndugu. A. K . Tibandebange, Ndugu B.J. Mkale, Ndugu Bernad Mulokozi , Bibi Zahara Nuru, Dkt. Ben Moses, Injinia . Paul Nkanga, Ndugu Paul Sozigwa, Ndugu Wilifred Mwambulambo, Ndugu Elly Ntango, Ndugu Silvano Adel, Bibi Rose Lugembe, Ndugu Rafael Mollel.

Wengine waliowahi kushika nafasi hiyo ni Ndugu Silvanus Odunga, Ndugu Abubakari Rajabu, Ndugu Kenya Hassan, Ndugu D. Sepeku, Ndugu Raphael Bagama, Bibi Kijakazi Mtengwa, Dkt. Frolence Turuka, Seith Kamuhanda, Bibi Sihaba Mkinga, Prof. Elisante Ole Gabriel, Bibi Susana Mlawi, Dkt Hassan Abbasi na sasa ni ndugu yetu Said Othumani Yakubu(mwanakwetu anamuita Kaka Mkuu)

Utamaduni ni jinsi binadamu anavyokabili maisha katika mazingira yake. Hiyo inajumuisha mambo mengi kama vile ujuzi, imani, sanaa, maadili, sheria na desturi ,haya mambo ndiyo yanamtofautisha binadamu na wanyama. Utamaduni ni suala la msingi katika kwa jamii ukihusisha yale yote yanayopokezwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Hapo kuna fasihi, mafungamano, ndoa, michezo, ibada, sayansi na teknolojia na hata mavazi.

Ndiyo maana unasikia hawa wanavaa mgololi, hawa rubega hawa msuli na wale baibui kwa mazingira ya watu wa Pwani wanaume huvaa barakashia. Huvaaji huo wa nguo huwa unakuwa na maana kwa mvaaji kwa wale wanaomtazama bila ya yeye kusema neno.

Mathalani watu wa pwani ni wavaaji wazuri wa baibui na barakashia, namna baibui inavyofungwa huwa ina tafsiri zake kwa sie tunaofahamu na hata uvaaji wa barakashia huwa unatafsiri zake kwa yule anayemtazama. Jambo hilo linafanywa makusudi kutoa ishara kwa yule anamtazama bila ya kusema neno lolote.

Hapa katika barakashia inatazamwa ile mianguko ilivyolalia kofia hiyo kama kwa mfano mshazali, kushoto, kulia nyuma au mbele. Mathalani nyumbani mgeni amekaribisha katika kiti cha mkunjo na baba alafu wanaongea barazani. Mama akaja kumsalimia mgeni.

Asalaam aleikum!

Aleikum salaam!

Nyumba heri?

Heri tu

Na mwezangu hajambo?

Hajambo.

Baba amekaa na mgeni kwenye vitu vya mkunjo kumbuka mama anasalimia kwa mbali mita mita saba hadi nane, gafla utaona baba anabadilisha kofia yake na kuilaza kwa mbele nakuibonyeza kidogo, hapo itakuwa kama imekaa vibaya hivi na mbonyezo kwa mbele, hapo baba anampa ishara mkewe kuwa huyu mgeni aletewa chakula. Utashangaa chakula kimeletwa mgeni anakula bila kelele. Mwanakwetu huoni ni utamaduni wa Waswahili katika mavazi yakihusishwa na chakula.

Leo mwanakwetu ana nini ?

Viongozi hao watatu wa Wizara hii wanaonekana wamevalia nguo za rangi ya samawati(bluu) Waziri amesuka Rasta za Yeboyebo, Naibu Waziri amesuka nywele mtindo wa Sunset na Katibu Mkuu kakata nywele katika mtindo brashi, suti zote ni za rangi ya samawati.

Hii rangi ya samawati ina nini? Tena hii ni samawati iliyokoza mwanakwetu. Rangi hii inayochukua sehemu kubwa ya ulimwengu ambayo ni bahari na anga, rangi hii inamaanisha maslahi ya wengi si rangi ya maslahi ya wachache, angalia anga lina jua linalomulika wote, mwezi unamulika wote na nyota pia, bahari ina maji yanayonufaisha wote kwa kitoweo bila uchoyo.

Angalia askari sare ya rangi hii huvaliwa wakati wakitunukiwa medali maana wao huenda vitani kupigana kwa ajili ya maslahi ya wengi, ndiyo kusema samawati ni rangi ya maslahi ya sote

Mwanakwetu kwa leo inatosha, nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news