Kwa nini ndoa ya Dokta Mwaka imemgharimu Alhadi Mussa Salum?

NA DIRAMAKINI

BAADA ya Januari 25, 2023 ndoa ya mtaalamu wa tiba mbadala, Juma Mwaka maarufu kama Dokta Mwaka na mkewe Queen Masanja kuvunjwa rasmi, ndoa hiyo imeendelea kutikisha zaidi huku Alhadi Mussa Salum akipoteza kazi

Ndoa hiyo ilivunjwa baada ya kikao cha Kamati ya Masheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa sheikh wa mkoa, Alhadi Mussa Salum kuketi kwa dharura na kuridhia maombi ya Queen kutaka apewe talaka.

Aidha, leo Februari 2, 2023 Baraza la Ulamaa limetemgua uteuzi huo wa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum na kumteuwa Sheikh Walid Omar kukaimu nafasi hiyo.

Akisoma taarifa iliyosainiwa na Katibu wa baraza hilo, Hassan Chizenga leo Februari 2, 2023, Mjumbe wa Baraza hilo, Issa Othman amesema, uamuzi huo umetokena na kikao chao cha Februari Mosi na 2, mwaka huu jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt.Abubakar Zubeir bin Ally.

“Baraza la Ulamaa katika kikao chake kilichofanyika Februari 1 na 2 jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt.Abubakar Zubeir bin Ally limetengua uteuzi wa Sheikh Alhad Mussa Salum kama Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia leo Februari 2, 2023,” amesema.

Ameendelea kusema kuwa Mufti na Sheikh Mkuu, amemteua Sheikh Walid Alhad Omar kukaimu nafasi ya Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia leo Februari 2, 2023.

Hayo yamejiri ikiwa Januari 27, 2023 Baraza la Ulamaa lilikutana kwa dharura kwa ajili ya masuala mbalimbali na miongoni mwa masuala hayo ni kuhusu suala hilo katika Ofisi ya Qadhi ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Baraza la Ulamaa kupitia kikao hicho lilitengua uamuzi wa Kamati ya Masheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam iliyovunja ndoa ya Juma Mwaka marufu kama Dokta Mwaka na mkewe, Queen Masanja ikieleza uamuzi huo ni batili

“Baraza la Ulamaa leo tarehe 27/01/2023 limekutana kwa dharura kwa ajili ya masuala mbalimbali na miongoni mwa masuala hayo ni kadhia iliyotokea hivi karibuni katika Ofisi ya Qadhi ya Mkoa wa Dar es Salaam. Kadhia ambayo inamuhusu Dokta Mwaka na mkewe Queen.”

“Ndoa ya bwana Juma Mwaka Juma ‘Dr Mwaka’ na Mkewe Bi Qeenie Oscar Masanja haijavunjika na kwa hivyo kwa kuwa kuna malalamiko yaliyopelekwa katika Ofisi yo Qadhi, malalamiko hayo au kesi hiyo iendelee katika ofisi ya Qadhi na Baraza la Ulamaa linafuatilia kwa karibu juu ya namna shauri hilo na mengine yanayoendelea kwa ajili ya kuchunga nidhamu katika Baraza,”iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news