Mtaji wa NHC wafikia trilioni 3.4/- kutoka trilioni 2.9/- mwaka 2019

NA GODFREY NNKO

MTAJI wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) umeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.9 mwezi Juni, 2019 hadi shilingi trilioni 3.4 mwezi Juni, 2022.

Hayo yamesemwa leo Februari Mosi, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea kuhusu ufanisi wa shirika hilo mwaka 2021/22 na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/23.

Mchechu amesema, mafanikio ya shirika hilo yanatokana na maadili ya msingi sita ambayo wamejiwekea ikiwemo weledi, ufanisi, uwazi, ubunifu, ushirikiano na uadilifu.

"Tumewaita hapa leo kwa ajili ya kutimiza maadili ya msingi matatu kati ya sita ya shirika. Maadili hayo yanayotufanya kuwajibika leo kwa wateja wetu na umma kwa ujumla ni weledi, ufanisi na uwazi ambapo tumekuja kuwaeleza matokeo ya ufanisi wa shirika lenu katika jitihada zake za kuwahudumia watanzania na kutengeza faida kwa mwaka wa fedha 2021/2022.Aidha, nitaeleza mwelekeo wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Shirika kwa mwaka wa fedha 2022/2023,"amefafanua.

Katika hatua nyingine, Mchechu amesema, mizania ya shirika imeendelea kuimarika na thamani ya mali za shirika kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha kuwa hadi kufikia Juni 31, 2022 zilikuwa shilingi trilioni 5.04.

Mchechu amefafanua kuwa, mizania hiyo imeendelea kukua mwaka hadi mwaka kwa wastani wa asilimia 12 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2019.

"Thamani hii inahusisha vitega uchumi vya majengo na ardhi ghafi inayomilikiwa na shirika ambayo bado haijaendelezwa ikiwa ni pamoja na miradi ya nyumba inayoendelea,"amebainisha.

Mbali na hayo Mchechu amesema, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kuongeza mapato yake hadi kufikia kiasi cha shilingi bilioni 257.47 mwaka 2022 kutoka shilingi bilioni 144.42 mwaka 2021.

"Mwaka 2021/22, mapato ya kodi yamepanda na kufikia shilingi bilioni 90.76 kutoka shilingi bilioni 89.23 mwaka 2020/21. Kadhalika, mapato ya mauzo ya nyumba yamepanda kutoka shilingi bilioni 29.33 mwaka 2020/21 na kufikia shilingi bilioni 121.95 mwaka 2021/22.

"Vilevile, mapato ya miradi ya ukandarasi yamekua kutoka shilingi bilioni 25.60 mwaka 2020/21 hadi kufikia shilingi bilioni 43. 98 mwaka 2021/22,"amefafanua Mchechu.

Pia amebainisha kuwa, shirika hilo limeendelea kuongeza faida kabla ya kodi na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 92.9 (2021:faida ya shilingi bilioni 93,966). Aidha, mwaka 2020/2021 faida ilishuka kutokana na kushuka kwa hali ya soko la nyumba nchini.

Hata hivyo, Mchechu amesema faida halisi inayotokana na shughuli za shirika iliongozeka hadi kufikia shilingi bilioni 60.7 mwaka 2021/22 kutoka shilingi bilioni 31.7 mwaka 2020/21.

Amesema, ongezeko hilo lilienda sambamba na ongezeko la majengo. "Kwa sasa, hali ya soko la nyumba imeanza kuimarika. Ni matarajio ya shirika kuwa mwaka wa fedha 2022/2023 litaendelea kupata faida kubwa,"amebainisha Mchechu.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu akizungumzia kuhusu kodi mbalimbali zilizolipwa serikalini amesema,shirika liliweza kulipa kodi mbalimbali inayofikia takribani shilingi bilioni 22.0 kwa mwaka 2021/2022.

"Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekuwa mlipaji wa kodi ikiwemo kodi ya majengo, kodi ya ardhi, na nyingine mbalimbali ukiangalia katika mapato ya property tax ya TRA nafikiri mlipaji mkubwa ni NHC.

"Hakuna anayelipa zaidi yetu. Kwa sababu sisi ndio wenye Nyumba nyingi, ukienda kwenye levies (ushuru) zinazotolewa na halmashauri kadhaa unakuta Shirika la Nyumba ni mlipaji mzuri wa kodi hizo na ni mmiliki wa nyumba nyingi kuliko mwingine katika mikoa au majiji mbalimbali, kwa hiyo ni wadau wazuri katika ujenzi wa nchi,"amefafanua Mchechu.

Aidha, amesema shirika limelipa gawio serikalini la shilingi milioni 750 kwa mwaka 2021/2022. "Gawio hili ni kiwango kinachopaswa kulipwa na shirika kila mwaka kutokana na maelekezo ya Msajili wa Hazina. Shirika limekuwa likichangia kila mwaka Gawio la Serikali na kulipa kodi za Serikali pamoja na kujiendesha lenyewe kibiashara bila ya kupata ruzuku kutoka serikalini,"amefafanua Mchechu.

Shirika la Nyumba la Taifa lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.45 ya mwaka 1962.NHC baadae liliunganishwa na iliyokuwa Msajili wa Majumba kwa Sheria Na. 2 ya mwaka 1990 ambayo ilirekebishwa mwaka 2005 ili kulifanya shirika lijiendeshe lenyewe kibiashara.

Malengo ya shirika kwa mujibu wa Mpango Mkakati wake (2015/16-2024/25) ni pamoja na kuwa msimamizi mahiri wa miliki, kuimarisha uwezo wa kiuendeshaji na udhibiti, kutumia kikamilifu rasilimali watu, kuwa kiongozi katika uendelezaji miliki, kuhuisha mikataba na mazingira ya kisheria na kujenga taswira ya shirika nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news