Mwalimu Makuru:Maboresho ya sheria kandamizi kwa vyombo vya habari ni afya kwa tasnia na Taifa

NA DIRAMAKINI

"Ukishavibinya vyombo vya habari maana yake umewapa wananchi hofu, hata kama Serikali ikifanya jambo jema wananchi hawatalipokea kwa mtazamo mzuri na pia jambo zuri lolote ambalo Serikali ikifanya wananchi hawataamini.

"Kwa sababu hawawezi kukiamini, kwani mawazo yao kama hayaheshimiwi na hayana sehemu wapi yasikike kisa yanakosoa hamuwezi kwenda pamoja baina ya Serikali na wananchi na hii ni hatari katika utawala bora;

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph ameyasema hayo katika mahojiano na DIRAMAKINI wakati akizungumzia kuhusu umuhimu wa kuwa na vyombo huru vya habari ambavyo vitawajibika kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla nchini.

"Kinachofanyika kwa sasa, Serikali inakwenda vizuri kwa sababu ipo katika hatua ya kufanya maboresho kwa sheria ambazo zilikuwa kandamizi kwa vyombo vya habari, dhamira ni kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya maoni yao na uhuru wao wa kusema kusikika na pia Rais anataka wananchi tuishi kwa kufuata sheria asiwepo mtu mkubwa ambaye yeye ndiye atakuwa juu ya sheria.

"Kubinya vyombo vya habari na watu kujieleza maana yake inatafsirika kwamba baadhi ya watu wako juu ya sheria, lakini kwa hatua hii ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan inaleta dhamira njema katika kukuza uhuru wa habari na kujieleza nchini."

Mwalimu Makuru ameyasema hayo ikiwa, tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka juzi katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mwalimu Makuru amesema, Rais Dkt.Samia anathamini na kuheshimu maoni na mawazo ya wengine kwa ustawi bora wa wananchi, ndiyo maana anahakikisha licha ya wananchi kuwa na nafasi ya kusema pia wanapata muda wa kufanya kazi kwa bidii kwa ustawi bora wa jamii na Taifa lao.

"Rais Dkt.Samia ameona sheria kandamizi kwa vyombo vya habari vinaleta chuki na kushindwa kufikia maendeleo. Ndio maana uhuru unakuja na maendeleo, na ndio maana tulipopata Uhuru tulipata Uhuru wa bendera Uhuru wa kisiasa ukaja Uhuru wa kiuchumi sasa haiwezi kupata uhuru wa kiuchumi.

"Kama watu wamebinywa wamefumbwa, kwa hiyo ili uongozi uwe thabiti lazima ukosolewe watu watoe maoni yao. Mawazo yanayokinzana ndio yanayoleta maendeleo, kwani yanapokinzana katika kuleta mafanikio yanatija.

"Vyombo vya habari vikiminywa umeminywa ajira na maendeleo. Pia vyombo vya habari vinapominywa vinakosa soko, kwani vinapata jambo muhimu la kusema, lakini vinaogopa kwamba vitavunja sheria, kwa hiyo hakuna watu watakaonunua magazeti hayo au kusikiliza tv au radio maana yake vyombo hivyo vimeajiri watu ambao wanalipwa na pia vinaposhindwa kuripoti kwa uhuru kero za wananchi bali viripoti maneno ya viongozi wanavyotaka maana yake vitakuwa havitendi haki.

"Ni kwa kutowasemea wananchi kwa kuogopa uchochezi. Kwa hiyo kuminya uhuru wa vyombo vya habari ni kuminya maendeleo yao na fursa ya Serikali kukusanya kodi kupitia maduhuli yatolewayo.

"Soko pia litakosekana kwa vyombo vya habari vya ndani,wananchi wanataka habari zinazowagusa wao na maisha yao ya kila siku, maendeleo yao na mikakati yao. Kwa hiyo usipowapa uhuru vyombo vya habari pia unaua sekta binafsi.

"Injini ya kupeleka mbele na kukuza sekta binafsi ni pamoja na vyombo vya habari kuwa huru, ajira nyingi zipo kwenye vyombo vya habari, watu wangapi wanatembeza magazeti na kupata pesa? Ni wengi, lakini magazeti yasipokuwa na maana hayatauzika na kukosa soko kutokana na kutoripoti kwa uhuru kero zao na mawazo yao.

"Pia, uhuru unapokosekana wa vyombo vya habari kuna chuki kwa wamiliki wa vyombo hivyo na pia wasomaji na watazamaji utakuta mtu anasema gazeti fulani sio zuri la kusifia tu na pia wengine watasema chombo fulani kinaandika uchochezi, kwa hiyo zile sheria hata upande wa serikali ungewabeba kwa muda.

"Lakini bomu lingelipuka kwa sababu wananchi walichukia zile sheria na vyombo vya habari kwa sababu waliona havisemi, kumbe vimebinywa na wananchi wenyewe wamebinywa. Sasa Mheshimiwa Rais anachokifanya ni kuvipa uhuru,wananchi waongee pasipokubanwa kwa aina yoyote.

"Afya ya nchi bila kuwa na vyombo madhubuti vya habari vilivyo huru kusema yale ambayo wananchi wanayataka kwa uhuru na uwazi ili yafanyiwe mabadiliko kwa lengo la kuleta tija hakuna maendeleo ya kweli,"amefafanua Mwalimu Makuru.

Kwa sasa,Serikali inatarajiwa kuwasilisha Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya 2016 katika vikao vya Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloendelea jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news