'Uthabiti wa vyombo vya habari umebeba majawabu mahususi'

NA DIRAMAKINI

UIMARA wa vyombo vya habari nchini umetajwa kuwa,umebeba majawabu mahususi ambayo ni tiba ya msongo wa mawazo, uponyaji wa kisaikolojia kwa wananchi ambao wanapowasilisha hoja zao zikapatiwa ufumbuzi iwe vijijini au mijini wanajisikia faraja zaidi.

Picha: Ericky Boniphace/AFP/Getty Images.

"Mtu anataka kusema, kuna maji yanakosekana,kuna kiongozi fulani anatesa wananchi ukanyamaza maana yake kumbinywa kwako kutamfanya huyo mtu apate msongo wa mawazo, lakini akisema kuna hatua zikachukuliwa na hata uponyaji wake utakuwepo kisaikolojia.

"Kwa sababu jambo atakalokuwa amelisema litakuwa limetolewa ufafanuzi. Kwa hiyo anachokifanya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kwamba nchi itajengwa kwa watu kuwa huru na kutoa maoni yao kwa ajili ya kujenga ambayo ni mazuri, lakini pia sheria zetu haziwezi kuwa nzuri kama watu hawana fursa ya kutoa maoni yao;

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph ameyasema hayo katika mahojiano na DIRAMAKINI wakati akizungumzia kuhusu umuhimu wa kuwa na vyombo huru vya habari ambavyo vitawajibika kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla nchini.

Pia, Mwalimu Makuru amesema kuwa, mawazo mazuri yatasaidia pia hata upatikanaji wa katiba bora nchini, kwani mawazo yao ndio yatachukuliwa na kuwezesha upatikanaji wa katiba yenye kujibu na kukidhi kwa usahihi mahitaji.

"Katiba safi ni ile ambayo imesikiliza makundi ya kila aina yakachakatwa, katiba ya nchi si ya vyama vya siasa ni mali ya Watanzania wote kwa hiyo lazima utengeneze uthabiti wa vyombo vya habari kuwa huru kwa sababu kuna kipindi tunaweza kujikuta wanasiasa wanaweza kuja na ajenda zao au mawazo yao ya kuwalinda na vyombo vikashindwa kuwa huru kusema yatapita.

"Lengo lake ni kutaka nchi iendelee, lakini nchi haiwezi kuendelea kama maono ya watu yatakuwa yamebinywa. Kutakuwepo sheria kandamizi ya kubinya uhuru wa mawazo baina ya mtu na mtu na pia wa kutoa maoni katika vyombo vya habari.

"Vyombo vya habari vinatakiwa viwe huru, viweze kufichua maovu, lakini lengo la Rais katika kufichua maovu ni kutaka Serikali iwajibike kwa wananchi wake. Kama Serikali isipokuwa ya kuwajibika watu watakuwa huru kukosoa uhuru wa kumweleza kiongozi aweze kujisahihisha.

"Lengo kubwa la Rais Dkt.Samia ni pamoja na kutaka viongozi wajisahihishe, yaani wao sio miungu hawakosei, anajua ni binadamu wanakosea kama sheria itakuwa imewakandamiza wananchi kuisema serikali yao na kuiambia kwa uhuru kwa kutumia demokrasia kwa kutumia vyombo vya habari maana yake viongozi watakuwa kama Wafalme jua, watakuwa na mamlaka ya kuwakandamiza wananchi na wananchi wataumia katika mioyo yao na kukosa furaha kwamba hawawezi kumuongea kiongozi wanamuogopa;

Mwalimu Makuru ameyasema hayo ikiwa, tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka juzi katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mwalimu Makuru ameendelea kufafanua kuwa, "anachokifanya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia anataka uwazi ndani ya Serikali, sasa uwajibikaji kwenye serikali lazima aachie uhuru na kutoa sheria kandamizi zilizokuwa zinavibana vyombo vya habari ili viweze kufichua na kusema bila mashaka yoyote yale kusudi visaidie serikali na watendaji wake kuwajibika kwa wananchi, lakini uhuru huo uwasaidie wananchi kuiambia Serikali wanapokwenda kinyume viongozi wasinyamaziwe ama kuachwa kimya.

"Lakini vyombo vikiwa huru vitafanya mijadala na watu mbalimbali na makundi mbalimbali ili kuboresha na kuhakikisha kunakuwepo ushirikishwaji na ujumuishwaji wa wananchi wote katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

"Rais anachokifanya ni kitu kizuri sana lazima uwape watu uhuru kuelezea matatizo yao na mambo yanayowasibu wanapenda waishi vipi waongozwaje, watoeje maoni yao, na huo wote ni uhuru,"amefafanua Mwalimu Makuru.

Mambo yalivyo

Vyombo vya habari vinatajwa kuwa na nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko chanya kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi katika ngazi ya jamii na Taifa popote pale duniani.

Mathalani katika nchi zinazoendelea kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vyombo vya habari vinaweza kuwa na jukumu muhimu katika kuendeleza ajenda ya maendeleo katika jamii ambazo zinakabiliana na hali ngumu ili kupata fursa za kujikomboa na hali ya uchumi.

Pia, vyombo vya habari vina nafasi kubwa kusaidia ukuaji wa uchumi kwa kuchochea masoko ya watumiaji ndani na nje ya nchi.

Ripoti nyingi zinabainisha kuwa, pale ambapo vyombo vya habari vinakuwa na uwezo wa kutekeleza vyema majukumu yake bila kuingiliwa au shinikizo la kutoka ndani au nje (vyombo vya habari huru), vina nafasi kubwa ya kutayarishaji ajenda mahususi.

Ni ajenda ambazo zinaweza kuboresha masuala ya utawala bora katika ngazi zote za uongozi kuanzia ngazi za chini hadi Taifa.

Vivyo hivyo,kuongeza uelewa wa raia kuhusu masuala ya kijamii, kuwawezesha kuwajibika kwa Serikali zao, kuzuia rushwa, na kuunda jukwaa la kiraia kwa ajili ya mijadala shirikishi kwa ustawi bora wa jamii na Taifa.

Mara kwa mara, wadau wa Sekta ya Habari nchini wamekuwa wakibainisha kwamba, sheria na kanuni kandamizi zinazozuia vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uhuru zinapaswa kurekebishwa ili waandishi waweze kutimiza wajibu wao kama mhimili wa nne usiorasmi wa dola.

Baadhi ya sheria na kanuni zinazolalamikiwa kuminya uhuru wa vyombo vya habari nchini ni pamoja na Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambayo, pamoja na mambo mengine, inaruhusu Serikali kufungia magazeti.

Sheria hiyo pia inaweka sharti kwa gazeti kuwa na leseni ambayo inapaswa ihuishwe kila mwaka. Pia, inaweka sharti kwamba ili mtu afanye uandishi wa habari Tanzania ni lazima awe na elimu ya kiwango cha stashada au shahada ya uandishi wa habari au taaluma inazohusiana nazo.

Kingine kinacholalamikiwa ni Kanuni za Mawasiliano na Kielektroniki na Posta, Maudhui ya Mtandaoni ambazo pamoja na kuipa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kufungia redio, runinga na vyombo vya habari vya mtandaoni kwa kukiuka maadili, pia zinaweka sharti kwa vyombo vya mtandaoni kuwa leseni inayohuishwa kila mwaka ambayo gharama yake imekuwa ikilalamikiwa na wadau.

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imekuwa rafiki mkubwa wa vyombo vya habari, kwani mwanzoni mwa mwaka jana Serikali ilichukua hatua ya kuyafungulia magazeti manne ya MwanaHalisi, Mawio, Mseto.

Sambamba na Tanzania Daima huku Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye akibainisha nia na utayari wa Serikali wa kuyafanyia kazi maoni na mapendekezo ya wadau yanayolenga kuboresha sheria na kanuni zinazoongoza uandishi wa habari Tanzania.

Uamuzi wa kuyafungulia magazeti hayo ulitangazwa Februari 10, 2022 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari na kutoa leseni za magazeti hayo.

"Agizo la Rais ni sheria, natoa leseni kwa Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima, kwa sababu mambo haya ni vizuri tutoke kwenye maneno twende kwenye matendo, tufungue ukurasa mpya.

Wanasemaje?

Hivi karibuni, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda alibainisha kuwa, kama angekutana na kiongozi wa juu angemshauri mambo kadhaa kuhusiana na vyombo vya habari.

"Kumekuwa na lugha ambayo inatumika kwenye vyombo vya dola, wanatumia lugha kwamba sisi hatufanyi kazi kwa kusikiliza vyombo vya habari, hii mara nyingi imekuwa inatumika, kuna jambo zito na jamii au mhusika anarejesha hilo jambo, mhusika anatoa rejea ya chombo cha habari, basi mara nyingi viongozi wa dola huwa wana lugha kama hiyo kuonesha kwamba sisi hatufanyi kazi kwa kuzingatia vyombo vya habari.

"Kwa hiyo mimi kama ningekutana na kiongozi wa juu ningemshauri kwamba vyombo vya habari visitazamwe hivyo, bali viongozi wavitazame vyombo vya habari katika ujenzi wa taifa ambalo ni huru, lenye utawala bora, utawala wa haki. Kwa hivyo vyombo vya habari vina nafasi kubwa.

"Ni muhimu sana vikaangaliwa kama ni nyenzo muhimu sana katika taifa huru na kutenda haki.Vile vile ningemshauri kuhakikisha kwamba anaweka msingi imara wa sheria ili hii tasnia ya habari iepukane na sheria zinazopunguza uwezo wao wa kufanya kazi kwa maana ya sheria kandamizi, ili kuhakikisha kwamba hiyo sekta ya habari inapumua kutoka kwenye hayo mazingira ambayo yamejitokeza katika maeneo mengi,"alifafanua Sheikh Ponda.

Hoja ya Sheikh Ponda imebeba ujumbe mahususi ikizingatiwa kuwa, vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuifikia jamii kubwa kwa wakati mmoja iwe ni redio, runiga, magazeti au mitandao ya kijamii.

Pia, vyombo huru vya habari vina nafasi kubwa sana ya kukuza na kupasa sauti ya makundi yaliyotengwa au yasiyofikika kwa haraka huko vijijini.

Utafiti wa hivi karibuni umeonesha kwamba vyombo vya habari hasa redio vinahudumia idadi inayoongezeka ya vijana, vijijini na vikundi vya watu wasiojua kusoma na kuandika barani Afrika (BBC, 2006).

Kwa sasa,Serikali inatarajiwa kuwasilisha Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya 2016 katika vikao vya Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloendelea jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news