Ofisi ya Rais-Utumishi yarejesha tabasamu kwa wenye mahitaji

NA JAMES MWANAMYOTO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama, amesema watumishi wa ofisi yake wametoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wenye uhitaji katika Kituo cha Matumaini Mihuji na Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo inayotunza wazee na watoto ili kujenga matumaini ya wahitaji hao na kuwawezesha kutimiza ndoto za maisha yao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimpatia zawadi mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo cha Matumaini Mihuji jijini Dodoma alipokitembelea kituo hicho kwa lengo la kutoa msaada wa kijamii.

Mhe. Jenista amesema hayo wakati akikabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa wenye uhitaji katika kituo cha matumaini Mihuji jijini Dodoma.

Mhe. Jenista amesema, msaada walioutoa unaunga mkono malezi kwa wenye uhitaji kwani wanaamini kuwa watoto wenye uhitaji ndio watumishi wa umma na viongozi wa baadae, hivyo msaada huo ni sehemu ya kuchangia ujenzi wa msingi mzuri wa watoto hao kuwa watumishi wa umma na viongozi wa baadae watakaotoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi mafuta ya kupikia ikiwa ni sehemu ya msaada uliotolewa na watumishi wa ofisi yake katika kituo cha Matumaini Mihuji jijini Dodoma.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, jamii isipowasaidia wenye uhitaji watakosa mwelekeo na hapo baadae hakutakuwa na rasilimaliwatu itakayotekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE ambayo inajenga ari ya kila mtanzania kushiriki katika ujenzi wa taifa pamoja na kuandaa rasilimaliwatu itakayokuwa na tija katika utoaji huduma kwa wananchi.
Sehemu ya watoto wenye uhitaji katika Kituo cha Matumaini Mihuji wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza nao kwenye kituo hicho jijini Dodoma kwa lengo la kutoa msaada wa kijamii.

Aidha, Mhe. Jenista amesema, msaada wa vitu uliotolewa na watumishi wa ofisi yake katika Kituo cha Matumaini Mihuji na Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo imetokana na michango binafsi ya watumishi na si fedha ya Serikali.

“Michango iliyokusanywa imetuwezesha watumishi wote kuacha familia zetu na kuja kuwafariji wenye uhitaji, niwahakishie hakuna mtumishi yeyote aliyesalia nyumbani kwake wakati wa zoezi hili muhimu la kutoa faraja kwa wahitaji,” Mhe. Jenista amefafanua.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akikabidhi kiroba cha unga ikiwa ni sehemu ya msaada uliotolewa na watumishi wa ofisi yake katika Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo inayotunza wazee na watoto. Kulia kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro.

Akikabidhi msaada kwenye Nyumba ya Amani na Furaha inayotunza wazee na watoto Hombolo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amesema msaada alioukabidhi kwa niaba ya watumishi wa ofisi yake japokuwa ni mdogo lakini ni sadaka inayojitosheleza na kuongeza kuwa, watumishi wameguswa kwasababu wanathamini mchango wa wazee ambao wakati wakilitumikia taifa walijituma kwa moyo na uzalendo katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Kituo cha Matumaini Mihuji, Sista Elizabeth John amewashukuru watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuwatembelea na kutoa msaada utakaosaidia malezi ya watoto katika kituo chao na kuahidi kuwa misaada hiyo itatumika kama ilivyokusudiwa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akiwapatia zawadi watoto wanaolelewa katika Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo alipokitemebela kituo hicho kwa lengo la kutoa msaada wa mahitaji ya vitu mbalimbali jijini Dodoma.

Mmoja wa watoto anayelelewa katika Kituo cha Matumaini Mihuji Bi. Elizabeth Francis, amemshukuru Mhe. Jenista na watumishi wa ofisi yake kwa msaada walioutoa na kuahidi kuendelea kuwaombea ili waweze kutekeleza vema majukumu yao ya kulitumikia taifa.

Naye, Msaidizi wa Kituo cha Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo Sista Maria Radiance amesema, sadaka iliyotolewa na watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika kituo chao itasaidia malezi ya wazee na watoto kituoni hapo na kuongeza kuwa ujio wa watumishi hao ni tendo la upendo ambalo linatokana na msukumo wa Mwenyezi Mungu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (Aliyekaa na watoto chini) akiwa katika picha ya pamoja na watoto wanaolelewa katika kituo cha Matumaini Mihuji alipokitembelea kituo hicho kwa lengo la kutoa msaada wa kijamii.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeshiriki shughuli za kijamii kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na jamii yatakayokuwa na tija katika kupata mrejesho utakaoboresha huduma katika Utumishi wa Umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news