Rais Dkt.Mwinyi atoa wito kwa Puma Energy

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeitaka kampuni ya kimataifa, Puma Energy kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya mafuta ya ndege ili kuendana na soko la ushindani la kimataifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi (katikati) akisisitiza jambo wakati alipokuwa na mazungumzo na Ujumbe wa Kampuni ya Puma Afrika ukiongozwa na Kiongozi Mkuu, Bw.Fadi Mitri (wa pili kulia) walipofika Ikulu jijini Zanzibar,mazungumzo hayo yanahusu masuala mbalimbali ikiwemo biashara ya mafuta hapa Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati akizungumza na uongozi wa kampuni hiyo, Ikulu jijini Zanzibar.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, ongezeko la bei ya maputa kwa kampuni hiyo inaiathiri Zanzibar kwa baadhi ya kampuni kubwa za ndege kushindwa kutua nchini kwa hofu ya kukosa mafuta.

Aliishauri kampuni hiyo kushusha bei ili kuendana na soko la ushindani hasa kwa kampuni za usafiri wa anga na wadau wengine kwenye sekta ya usafirishaji.

Alisema, kuna mgogoro mkubwa kwenye sekta hizo uliosababishwa na kupandisha gharama za mafuta ya ndege, hali inayosababisha baadhi ya kampuni kubwa za ndege kununua Dar es Salaam na Mombasa, aidha, Dk. Mwinyi alieleza wanaoathirika zaidi ni kampuni ndogo za ndege zinazofanya safari zake za ndani baina ya Pemba, Tanga na Dar es Salaam.

Hata hivyo, aliwashauri Puma Energy kutoridhika na hali hiyo, badala yake wakubaliane na hali halisi ya soko la ushindani lilivyo ili kutoa fursa ya soko la biashara kwa kila mwekezaji.

Aliwaeleza kampuni hiyo endapo watashindwa kupungunguza gharama za mafuta na kukabiliana na ushindani wa kibiashara uliopo kwenye usafirishaji wa anga, Serikali tayari imeiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) kuangalia uwezekano wa kampuni nyingine kupewa fursa ya kuhudumia eneo hilo.

Alidha, alisema Serikali ina dhamira njema kwa wawekezaji wote pia inaunga mkono jitihada wanazozifanya kwa Serikali katika kuwahudumia watu na mazingira mazuri ya biashara, hivyo aliwataka wawekezaji kukabiliana na ushindani kwa kuleta unafuu kwa kila mmoja.

Pia Dk. Mwinyi alieleza Serikali imedhamiria kufanya uwekezaji mkubwa wa kuhifadhi mafuta ya kutosha ili kujiweka tayari na tatizo lolote, kupata utatuzi wa haraka.

Aliishauri Kampuni ya Puma Energy kuangalia fursa za uwekezaji wa eneo hilo kwa bandari ya Mangapwaji kuweka chemba ya kushushia mafuta na ghala la kuhifadhia mafuta ya ndege.

“Kwa hali tuliyonayo sasa likitokea tatizo lolole ingawa hatuombi litokee, hatutokuwa na uwezo wa kulitatua kwa vile hatuna hakiba,”alieleza Dkt.Mwinyi.

Alisema, Serikali inajipanga kuhifadhi mafuta ya ziada ili iwe na uwezo wa kukabiliana na changamoto itakayotokea kwa kuziba mianya ya athari za changamoto hizo.

Akizungumzia ujenzi mpya wa uwanja wa ndege wa Pemba, Rais Dkt. Mwinyi alisema Serikali imedhamiria kuweka uwiano sawa na mandhari ya kisiwa cha Unguja kwa uondoa utofauti wa maendeleo na uwekezaji baina ya visiwa viwili hivyo.

Alisema, tayari kuna wadau wengi wamejitokeza kuwekeza eneo hilo na kuwaeleza Puma Energy kuangalia fursa wa uwekezaji kwenye mradi huo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy kanda ya Afrika, Fadi Mitri aliiambia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba wana nia njema ya kuwekeza Pemba kwenye uwanja mpya wa ndege wa kimataifa kuwa wa kisasa na bora zaidi kwa Afrika nzima kuongoza kwa huduma za kimataifa na vifaa vyenye ubora wa uhakika.

Alisema, kampuni ya Puma Energy itawekeza kwenye miundombinu ya kisasa ya uwanja huo na ipo tayari kutoa huduma za ndege za kimataifa kwenye uwanja huo kama ilivyo kwa kampuni ya Dnata ambayo inatoa huduma bora za viwanja vya ndege vya kimataifa kupitia mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Alisema, licha ya Dnata kutoa huduma kwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume, Kisauni Unguja, alisema kwa kisiwa cha Pemba, kampuni yake ya Puma Energy iko tayari kuhudumia na wameahidi kwa Serikali kwamba wataunga mkono kwenye sekta hiyo.

Aidha, aliiahidi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuongeza ndege zaidi za kimataifa kuja moja kwa moja Zanzibar, alisema Puma Energy wanahudumia ndege zaidi ya 80 nchini Afrika Kusini. Hivyo, uwezo wa kuongeza ndege kufanya safari zake Zanzibar ni rahisi sana kwao.

Alisema, watashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuifanya Zanzibar kuwa kituo bora zaidi kwa wageni kufikia na rahisi kufikiwa kwa kufurahia uzuri wa mandhari na haiba ya visiwa vyake.

Kampuni ya Puma Energy yenye makao makuu yake nchini Singapore, inafanya kazi kwenye viwanja vya ndege zaidi ya 80 duniani kote pia ina vituo 740 kwa nchi 50 za Afrika, ni sehemu ya kampuni kubwa duniani ya Trafigura ambayo inafanya kazi kwa zaidi ya nchi 40 kutoka mabara matano ya Dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news