Rais Ruto aguswa na mchango wa mashirika ya kidini Kenya

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa William Samoei arap Ruto amepongeza jukumu kubwa linalotekelezwa na mashirika ya kidini katika utoaji wa huduma za kijamii nchini humo.

Mheshimiwa Rais Ruto amesema, Serikali inathamini mchango wa mashirika ya kidini katika utoaji wa huduma za afya, elimu pamoja na masuala mengine, na imejitolea kuendelea kushirikiana nayo.

Picha na Ikulu.

Akizungumza alipokutana na wawakilishi wa afya na elimu wa mashirika ya kidini Jumanne iliyopita katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto aliahidi kwamba serikali itashirikiana na taasisi hizo kutoa huduma za afya kwa ufanisi na kwa gharama nafuu pamoja na elimu husika.

Viongozi hao waliongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Jackson ole Sapit, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki la Mombasa, Martin Kivuva, Askofu Robert Lang’at wa Kanisa la Africa Gospel Church na Mratibu PCEA, Thigu Mutahi.

"Taasisi zinatoa huduma ya afya kwa asilimia 40 nchini Kenya na lazima ziwe msingi katika mpango wetu wa Huduma ya Afya kwa Wote,"alibainisha Rais Ruto.

Pia Rais Ruto alitaja wajibu muhimu wa vikundi vya kidini na viongozi walio nao katika kufundisha maadili shuleni na vyuoni hasa katika taasisi wanazozifadhili.

Rais Ruto alidokeza kwamba uwakilishi wa mashirika ya kidini katika uendeshaji wa taasisi za elimu ni muhimu na unathaminiwa na Serikali.

Aidha, Rais Ruto aliwataka viongozi wa dini kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, pombe na tabia mbaya zinazowaathiri vijana.

"Katika masuala ya kijamii, juu ya mambo ya maadili,mna nguvu zaidi kuliko Serikali. Pombe na dawa za kulevya zimeingia katika jamii yetu na zinaumiza vijana na viongozi wetu,”alibainisha Mheshimiwa Rais Ruto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news