Serikali yawataka waganga wakuu kuhamasisha matone ya Vitamin A kwa watoto

NA OR-TAMISEMI

WAGANGA wakuu wa halmashauri zote nchini wamehimizwa kuhamasisha utolewaji wa matone ya Vitamin A kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Hatua hiyo imetajwa kuwa, itasaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuzuia vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinavyosababishwa na ulaji duni wa vyakula mchanganyiko.

Rai hiyo imetolewa Februari Mosi, 2023 na Afisa Lishe kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Bi.Asiatu Mbwambo wakati wa kikao kazi cha timu ya usimamizi shirikishi kutoka OR-TAMISEMI na watoa huduma wa kituo cha afya Matemanga kilichopo wilayani Tunduru.
Alisema, msingi wa lishe unaitaka watoto chini ya miaka mitano kula vyakula mchanganyiko lakini milo ambayo wanapewa watoto haikidhu makundi matano ya vyakula.

"Watoto wanatakiwa kula vyakula mchanganyiko, lakini milo yetu haikidhi aina ya vyakula kutoka makundi matano ya vyakula kwa hiyo matone ya Vitamin A yana vitamins zinazosaidia kuboresha afya na kuimarisha ukuaji wa mtoto.
"Upungufu wa Vitamin A mwilini unaweza kusababishwa na uwepo wa maradhi ingawa sababu kuu ni ulaji wa vyakula visivyo na Vitamin A ya kutosha,"amesema Mbwambo.

Amesema kuwa, utolewaji wa matone ya Vitamin A kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuboresha afya za watoto baada ya tafiti kuonesha kwamba upungufu wa Vitamin A kwa watoto huchangiwa pia na ulaji duni.

Mbwambo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wazazi na walezi wote wenye watoto walio chini ya miaka mitano kuhakikisha wanawapeleka watoto kupata matone ya Vitamin A katika kampeni zinazofanyika kila mwezi Juni na Desemba nchi nzima.
Amesema ni muhimu sana wazazi au walezi kuzingatia ulishaji wa vyakula mchanganyiko kutoka makundi matano ya vyakula ambavyo vina uwezo wa kuwapatia watoto virutubisho vya kutosha na kuwawezesha watoto kukua vizuri kimwili na kiakili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news