Serikali yawazawadia Watanzania Sports Arena Siku ya Valentine

NA JOHN MAPEPELE

LEO ikiwa ni siku ya wapendanao duniani (valentine) Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo imepokea kutoka Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) eneo la ekari 12 Kawe Jijini Dar es salaam litakalojengwa Ukumbi wa Kimataifa wa Kisasa wa Michezo (Sports Arena).
Akizungumza na wanahabari mara baada ya kukabidhiwa, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa aliyeambatana na Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi amesema, wizara inakwenda kulikabidhi eneo hilo mwezi Machi kwa Mkandarasi na ujenzi utachukua muda wa miezi 8 hadi 10 kukamilika.

Aidha, Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha sekta ya burudani na michezo zinakuwa sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa na wananchi wananufaika nazo.

Amesisitiza kuwa,watanzania wana kiu ya kuona Ukumbi wa Kimataifa wa michezo kama zilivyo nchi zingine unajengwa nchini Tanzania.
Amefafanua kuwa, kujengwa kwa ukumbi huo utabeba watu zaidi ya elfu 16 ambapo ni miongoni mwa Arena kubwa Afrika ambapo kwa sasa Arena kubwa ipo nchini Senegal inayochukua watu elfu 15.

"Arena yetu itachukua watu elfu 16 na tunategemea pia ichukue watu hadi elfu 20 ili Watanzania wapate nafasi kushuhudia matamasha mengi katika ukumbi huo."
Ameongeza kuwa,watanzania wamekuwa wakihoji kuwa tayari bajeti imepitishwa lakini hawaoni utekelezaji wa ujenzi wa ukumbi huo, lakini amewatoa hofu kuwa sasa Serikali inakwenda kuandika historia nchini kwa kujengwa kwa ukumbi huo wa Kimataifa."

Pia ameeleza Arena hiyo inatarajiwa kukamilika kwa miezi 8 hadi 10 ambapo utakuwa ukumbi wa Kimataifa barani Afrika.
"Tulipotoka hatukuwa na mipango mizuri hivyo tulivoingia na wasaidizi wangu tumehakikisha tunaenda kuongeza nguvu kubwa tutengeneze mipango,tutengeneze michoro na hatua zote tumekwisha kuzikamilisha."

Amewahakikishia Watanzania kuwa Wizara haitalala na itaendelea kukamilisha maagizo yote ya Mhe. Rais na Serikali yake katika kuimarisha sekta za Utamaduni Sanaa na Michezo ikiwa ni pamoja na kukamilisha mara moja ujenzi huo wa kimataifa hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news