TAJIRI MTOTO ALIYEFAULISHWA KWA DHARURA

NA MARTIN SHABOKA

WANAWAKE wawili wajawazito walikwenda hospitali kujifungua, kwa bahati mbaya wakati wanajifungua mwanamke mmoja akafa na mtoto aliye mzaa akawa hai, na yule mwanamke wa pili akapoteza fahamu baada ya mtoto kutoka, lakini sekunde chache baadaye mtoto huyo akafa.

Wauguzi wakakutana kwa dharura na kushauriana, na maamuzi yakawa hivi, yule mtoto aliyekufa awe wa mwanamke aliyefariki ili taarifa iandaliwe kuwa huyo mama na mtoto wake walifariki wakati anajifungua, na yule mtoto mzima wakamchukua na kumpa yule mwanamke aliyefiwa na mtoto.

Mama alifurahi sana baada ya kuzinduka, akampenda sana mtoto wake, lakini kasheshe ikawa kwenye ndoa yao, baba mtoto akaanza kuhisi mkewe alichepuka, maana mtoto hakuwa anafanana naye.

Ugomvi ulikuwa mkubwa kiasi kwamba mawifi na ndugu wa mwanaume wakashauri ndugu yao apime DNA, na mama kwa ujasiri akakubali.

Kipimo cha DNA kikaonyesha mtoto siyo wa mwanaume huyo na mama huyo akaambulia kuachwa na kufukuzwa kwa aibu kubwa.

Mama alimlilia Mungu huku akiamini kuwa kuna rushwa ilitembea ili kupindisha majibu ya DNA, lakini pamoja na yote akaendelea kumtunza mwanae kama single mother, akamsomesha mwanae kwa pesa ya biashara ndogo ndogo, hatimaye mtoto akamaliza form four kwa kupata division four ya ishirini na nane.

Kwa kuwa mama hakuwa na uwezo mtoto akajiajiri kwa kuanza kuosha magari na pikipiki kwa kuchota maji mtoni.

Kutokana na ucheshi wake biashara ilikua na kuongezeka, akaweka akiba na kufanikiwa kuboresha biashara yake,

Mungu akamsaidia katika biashara hiyo akapata marafiki waliomshauri vizuri, akasajili kampuni ya usafi na kuanza kusafisha hospitali ya wilaya, pole pole mtaji ukaendelea kukua akapata tenda ya kufanya usafi chuo kikuu na kwenye baadhi ya maofisi, akajikuta ameajili watu hamsini ambao wanamuita bosi.

Kama kawaida ya pesa siku zote hukuletea watu wenye pesa, huyu kijana siku moja akapata rafiki ambaye alimshauri juu ya biashara ya madini, na kwakuwa mtaji alikuwa nao, kijana akaingia front na kwenda kununua madini ya rubi Mpwapwa.

Baada ya miezi tisa siku moja alifanikiwa kununua jiwe kwa shilingi milioni nane na yeye akaliuza kwa Wathailand kwa dola elfu arobaini na tano za kimarekani.

Kumbuka hapo ana car wash, kampuni ya usafi, na sasa anauza madini. Kijana akanunua gari ndogo ya kutembelea na akajenga nyumba nzuri akiwa anaishi na mama yake na mdogo wake wa kike anayeitwa Joyce, ambaye huyu ndiyo alikuwa msimamizi wa kampuni ya usafi, na mama yake akisimamia car wash.

Katika kuhangaika na madini akapata taarifa kuwa rubi inapatikana kwa wingi Msumbiji, kijana akajitoa muhanga akaenda Msumbiji, akafanya shughuli hizi kwa miaka miwili na kufanikiwa kujenga nyumba nzuri na kununua magari, lakini kwa usalama wake akaoa mwanamke wa Msumbiji na kumfungulia Hotel.

Kijana maisha yakamnyookea akawa bosi mtoto, mama yake na dada yake hakuwatupa bali alihakikisha kila fursa anayoipata anawashirikisha.

Baba aliyemkataa na yeye hakuwa maskini, hivyo hakuwa na time nae kabisa, dogo nae akaamua kumtupa baba yake na kuangalia maisha yake.

Siku moja yule mama wa mtoto akiwa pale Car Wash akaja mwanamke wa makamu kidogo na kumsalimia, na baada ya salamu akajitambulisha kama nesi aliyemsaidia siku alipokuwa anajifungua, kisha akamuomba msamaha sana na kumwambia kuwa yule mtoto hakuwa wake, yeye mtoto wake alikufa ila mtoto huyo walimpa kwa sababu mama yake alikufa akiwa anajifungua hivyo wakaona ni vyema wampe yeye aliye hai ili mtoto asije akaishi kwa mateso.Mama akachanganyikiwa sana kwa taarifa hiyo.

ITAENDELEA....

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news